TUONGEE KISHKAJI: Kwa Kajala, Harmonize anapigania muziki wake au moyo wake?





 
HARMONIZE amerudiana rasmi na Kajala, lakini haikuwa rahisi, nguvu aliyotumia kumrudisha upande wake ilikuwa ni kama vile hakuna kitu kinaweza kwenda sawa kwenye maisha Konde Boy bila kuwa analala na kumka kitanda kimoja na Kajala.

Mwenyewe anasema, katuma sana watu wakamuombee msamaha kwa Kajala, katumia sana pesa kumnunulia zawadi ikiwemo migari mikubwa mikubwa na bling bling za bei mbaya.

Pia kakesha sana studio akiandika nyimbo za kumuomba msamaha Kajala, sio moja, sio mbili, akizichangaya anatoa albamu kabisa. Kaposti sana Instagram na kuandika maneno marefu kama katiba. Chawa wake pia wamepigia kampeni sana suala lake la kurudiana na Kajala, na ikamchukua miezi na miezi kabla ya Kajala kukubali kurudiana naye na sasa wanapeta tu, kila muda wako Instagram wanatupia tu-video twa mahaba, mara wanakula bata mbugani miksa kupiga picha na simba na chui, mara wako gym pamoja, mara Kajala anamuendesha wanarudi nyumbani, iliimradi tu muelewe kwamba wamerudiana na wako vizuri zaidi ya jana.

Lakini kwa nini Harmonize katumia nguvu yote hii? Je ni kwa sababu anampenda sana Kajala tu au ni kwa sababu pia anaupenda sana muziki wake?


 
Ninaposema anaupenda sana muziki wake ni kwa sababu Harmonize aliwahi kuwa pamoja na Kajala, ina maana kwamba anaelewa jinsi kuwa na mwanamke huyo kwenye mahusiano inavyoweza kuinua muziki wake kwani ukiachana na stori za Konde Boy kutoka Wasafi, hakuna kipindi kingine ambacho Konde Boy aliteka mitandao ya kijamii kama kipindi ambacho alikuwa kwenye mahusiano yake na Kajala.

Nikukumbushe tu, mara ya kwanza Harmonize na Kajala kuweka wazi uhusiano wao ilikuwa ni valentine day ya mwaka 2021 ambapo walipiga picha za pamoja wakiwa Zenji.

Na tukio hilo lilizua kasheshe kubwa mitandaoni baada ya baby mama wa Harmonize kuibuka na kudai kwamba, Harmonize alikwenda Zanzibar na mtoto bila kufuata taratibu kama vile kwenda pamoja na dada wa kazi ambaye anaweza kumuhudumia mtoto kipindi chote watakachokuwa Zanzibar.


Ikawa ni bonge moja la topic mitandaoni, wengine wakawa wanamtumia madongo Kajala na Harmonize kwamba kiki zinafanya wasijali afya ya mtoto, huku wengine wakimpiga madongo baby mama wa Harmonize anayejiita Shanteel kwamba anasumbuliwa na wivu.

Kisha, tukio lingine ni pale ambapo video za mahaba za Rayvaany akiwa na Paula ambaye ni mtoto wa Kajala zilipovuja, kisha Kajala akamtuhumu Mobetto kuwa ndiye aliyemkuwadia mwanae na kumlewesha.

Ambapo Kajala alikwenda kutoa taarifa polisi akisindikizwa na Harmonize, Harmonize ambaye baadae alikwenda kwenye mitandao ya kijamii na kuomba serikali imshughulikie Rayvanny kwa sababu Paula alikuwa bado ni mwanafunzi.

Ikazua bifu kubwa kati ya Harmonize na lebo nzima ya Wasafi inayomsimamia Rayvanny na matokeo yake, wote waliotajwa kwenye sakata hilo wakawa ndiyo mastaa Instagram kwa wiki kadhaa na Harmonize akiwemo.

Kisha, sakata lililosababisha kuachana kwao ndiyo lilimfanya Harmonize kuwa mfalme wa mitandao kabisa. Sakata linalodaiwa kuwa alimtaka Paula kimapenzi na kumtumia video za ajabu ambapo video hizo zilisambwa mitandaoni. Matokeo yake, Harmonize alikwenda kuwaripoti Paula, Kajala na Rayvanny na wote waliitwa polisi kwa mahojiano.

Ilikuwa ni sakata kubwa kiasi kwamba hakuna chombo cha habari kilichoacha kuripoti, hata vile ambavyo huwa haviripoti kuhusu maisha ya wasanii.

Kwa matukio kama hayo, ndiyo maana najilazimisha kukataa kwamba nguvu aliyotumia Harmonize kumrudisha Kajala kwenye mikono yake, inaweza kuwa ni kwa sababu anaupenda zaidi muziki wake.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad