Ticker

6/recent/ticker-posts

Mjane afukuzwa nyumba ya urithi, kisa kapata mchumba! 
Mjane afukuzwa nyumba ya urithi, kisa kapata mchumba!
FAUSTINA Kimamba mkazi wa Kijiji cha Mapili, Kata ya Ilela Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi,  ameiomba serikali imsaidie kupata stahiki zake, alizochuma na marehemu mumewe, Josephat Kanyongo anazodai amedhulumiwa na mtoto wake wa kumzaa.

Akizungumza hivi karibuni na HabariLeo Online, Faustina anasema aliishi na mume wake kwa miaka 20 na kupata watoto watano, lakini baada ya kufariki mumewe mwaka 2010, alikaa miaka mitatu na kupata mwanaume mwingine wa kuishi naye.

“Hapo ndipo matatizo yalipoanza, jamii zetu hazikuwa tayari nilete mwanaume mwingine kuishi naye katika ile nyumba ya marehemu, hapo ndipo matatizo makubwa yalipoanza,” alisema.

Akisimulia kisa kizima, alisema baada ya ndugu wa marehemu mume wake kupata taarifa kuwa anataka kuolewa na mume mwingine, walimchukua mtoto wake wa pili, Agustino Josephat aliyemzaa mwaka 1993 na kumshawishi amfukuze kwenye nyumba, ndipo mtoto huyo alipotekeleza amri hiyo.


 
"Mtoto wangu alikuja akaniambia mama nataka unipe godoro, nilipotoka nilikuta mtoto ameshabeba godoro, mimi nikaendelea kulala chini, badaye mtoto akaenda kujimilikisha mashamba, katika hekari 40 mimi alinipa heka 2, kwa kuwa nilikwenda kwa mtendaji wa Kata kulalamika,"alisema.

Mama huyo anasema baada ya mtoto wake kujimilikisha mashamba hayo, mengine aliyauza bila kuwashirikisha wenzake.

"Sehemu yoyote atakayouza, mtoto yeyote haruhusiwi kusema, nilikuwa nikizungumza wale upande wa baba yake wanasema ukienda kumshitaki ni wewe na sisi, akifungwa huyo mtoto utazaa na sisi,"alisema.


Alisema baada ya kupokea vitisho hivyo, aliogopa kwenda popote na ndipo alifukuzwa yeye na baadhi ya watoto wake wengine kwenye nyumba ya marehemu mume wake.

Alisema sababu kubwa ya kufukuzwa ni yeye kupata mwanaume mwingine wa kuishi naye, lakini mtoto wake mkubwa na ndugu wa marehemu mume wake walipinga vikali kwa madai ni kinyume na mila zao.

Licha ya kuondolewa katika nyumba hiyo, muda mfupi baadaye alipata pigo linguine kwani Yule mwanaume hakuendelea naye, hivyo akaamua arudi kwa wazazi wake.

Kutokana na hali hiyo, Faustina anasema baadhi ya watu wamemshauri asikae kimya, ndiyo sababu ameanza kupaza sauti na kuiomba serikali imsaidie angalau kurejesha baadhi ya mali ambazo bado hazijauzwa na mtoto wake, ikiwemo nyumba pamoja na mashamba, ili imsaidie kupunguza ukali wa maisha.


 
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mlele, Finner Soka watajitahidi kufuatilia changamoto ya Faustina na kuona namna ya kumsaidia, ili kupata stahiki zake na ikiwezekana kufikisha suala hilo katika vyombo vya sheria.

"Mahakama iamue kama alichuma mali na mume wake kwa miaka 20 moja kwa moja zile mali ni za kwake na watoto, haiwezekani mtoto akatoka akaenda kumfukuza mama yake,"alisema Finner.

Alisema tukio la Faustina linatoa picha kuwa, kuna vitendo vinavyoendelea kwenye ngazi ya jamii na havifiki kwenye ngazi zinazohusika.

"Kitendo cha mwanamke huyu kufukuzwa nyumbani inawezekana hakuwa na kauli kutokana na jamii kama hii, mume akifariki mwanamke haruhusiwi kuwa na uhusiano mwingine, ingawa mume akifiwa na mke wake jamii inaruhusu kuoa na kumleta palepale kwenye mji alioishi mke wake," alisema na kuongeza:


"Tunaweza tukamuunganisha na vikundi mbalimbali akapata mikopo kupitia ofisi ya maendeleo ya jamii akaendelea kujikimu," alisema.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele, Theresia Irafay amemtaka mwanamke huyo kufika ofisini kwake, ili kuona namna wanavyoweza kumsaidia, huku akitoa wito kwa wananchi wengine kuviona vyombo husika pale wanapofanyiwa vitendo ya ukatili wa kijinsia.

Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments