MTU WA MPIRA: Yusuf Bakhresa amerudi sawa, ila afumue uongozi uliopo



 
NCHI imezizima kwa mtetemo wa kurejea kwa Yusuf Bakhresa katika majukumu ya kuiongoza Azam FC. Yusuf ni ‘chizi wa mpira’ kweli kweli. Kurejea kwake kwa kishindo kumewashtua watu wote wanaomfahamu.

Baadhi ya watu wanajiuliza, kwani alikua wapi siku zote? Alikuwepo lakini hakuwa katika nafasi ya maamuzi kwenye timu. Alikuwepo kama sehemu ya wamiliki tu. Lakini sasa amerejea rasmi.

Yusuf ndiye alikuwa msimamizi wa timu wakati inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2014. Yeye ndio mwenye maamuzi yote. Azam ilikuwa tishio kweli kweli.

Watu walikuwa wakimwogopa Yusuf Manji na pesa zake pale Yanga, lakini Yusuf huyu wa Bakhresa alimnyoosha. Ni mtu hatari sana kwenye soka letu.


 
Ni ngumu sana kushindana na Yusuf Bakhresa akitaka lake. Huyu ndiye alimsajili Frank Domayo akiwa wa moto pale Yanga na hakujali wala nini.

Hao wachezaji wawili wa Ivory Coast, Kipre JR na Tape Edinho waliosaini Azam walikuwa wakitakiwa na Yanga ya GSM, lakini Yusuf akapindua meza. GSM walishazungumza nao lakini Yusuf alipokwenda kila kitu kikabadilika.

Huyo Isah Ndala alikuwa akitakiwa na Simba na walishazungumza naye kila kitu. Nini kimetokea baada ya Yusuf kuingilia kati? Amesaini Azam mapema tu, Simba imebaki mdomo wazi.


Hii ndio Azam mpya chini ya Yusuf. Anaweza kushindana na mtu yoyote. Yusuf ana maamuzi ya soka na analielewa vyema sana.

Kwanza ameanza kwa kurejesha baadhi ya watu ambao amewahi kufanya nao kazi kwa mafanikio pale Chamazi. Nasikia anaweza pia kumrejesha Jemedari Said pale Chamazi. Kwa kifupi amepania.

Kwa nguvu ya Yusuf sasa ninaamini Azam inaweza kumpata mchezaji yeyote inayomtaka sokoni. Haijalishi anatakiwa na Simba ama Yanga, lakini sasa Azam wakiamua wanamsaini.

Pamoja na yote kama Yusuf anataka kufanikiwa zaidi ndani ya timu hiyo anapaswa kuwaondoa viongozi waliokuwepo katika nafasi zao. Hawa wanaweza kumkwamisha.


 
Hasa nafasi ya Mtendaji Mkuu inahitaji damu mpya. Huyu aliyepo sasa amechoka. Pia amefeli katika mambo mengi sana katika miaka yake mitano ya nafasi hiyo.

Mfano usajili wa msimu uliopita. Azam ilisajili nyota lukuki kama Edward Charles, Paul Katema, Charles Zulu, Yvon Mballa na wengineo ambao wana uwezo duni na hawajawa na mchango wowote wa maana pale Chamazi.

Katika eneo la magolikipa Azam imekuwa na tatizo kila siku. Kila mtu aliona kuwa shida ipo kwa kocha wa makipa, Idd Abubakar, lakini watendaji hao waliendelea kumlea tu.

Makipa wa Azam wakawa ovyo kweli kweli. Yule Mathias Kigonya alikuja fundi, ghafla uwezo wake ukapotea. Yule Salula aliluja mtamu, eti leo hajui kudaka tena. Yaani inachekesha sana. Lakini Watendaji waliokuwepo wakaendelea kumlea kocha wa makipa kwa sababu ya ushkaji tu. Mwishowe timu inaumia.


Ni mpaka majuzi Yusuf alipoamua kumleta Mkufunzi mpya kutoka Hispania. Yaani mpaka mmiliki wa timu kaona tatizo na kulifanyia kazi lakini watendaji wapo tu. Hawa siyo watendaji wazuri. Wapo kwa maslahi yao na wanafurahia kusafiri na timu tu wapate posho. Ila hawana uwezo mkubwa wa kumsaidia Yusuf.

Kama Yusuf anahitaji mafanikio kweli aweke watendaji wapya. Hii itampa nguvu hata ya kushindania ubingwa wa Ligi. Aweke watendaji ambao wanamsikiliza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad