Ticker

6/recent/ticker-posts

Uteuzi Ma-RC, Ma-RAS wazua gumzo 
UTEUZI wa viongozi wa ngazi za mikoa, hususan wakuu wa mikoa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan jana, umezua gumzo kutokana na baadhi kung’ara tena akiwamo, Albert Chalamila ambaye amerejea kwa mara nyingine.

Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa huku wengine wakiondolewa kwenye nyadhifa hizo na katika wakuu wa mikoa, wanawake watano walichomoza hivyo kufanya idadi yao kuwa wanane sawa na asilimia 30.76.

Kutokana na uteuzi huo, watu walitoa maoni yao kupitia mitandao ya Twitter, Instagram na Facebook, wengi wakipongeza wakisema unalenga kuimarisha safu ya utendaji kazi wa Rais Samia.

Mmoja ya watu walioandika maoni kwenye ukurasa wa twitter wa Ikulu Mawasiliano,  aliandika: “Mlimtumbua Chalamila kwa nini na mmemrudisha kwa sababu zipi?” huku Mwinyi Salim akiandika: “Chalamila karudi kazini leo Ally Hapi kibarua kimeota nyasi.”

Naye Augustino Amando aliandika: “(Anthony) Mtaka alistahili kwenda Dar es Salaam na si Njombe, nimefurahi kuona Ally Hapi kaondolewa lakini sijafurahi Chalamila kurudi tena.”


 
Nicolaus Luhwago alisema: “Hii inatufundisha nini Watanzania? Ukitenguliwa kaa kimya wala kutoongea maneno mabaya, hongera sana Chalamila.” Huku Millanzi Marry akisema: “Viboko Kagera vitawahusu wale wazembe.”

Camel aliandika: “Wakati umefika wa kuangalia weledi katika kuwapa watu madaraka. Tujenge nchi hii kwa uchungu na maarifa makubwa, tujitahidi kuacha alama hasa kwenye kuwasaidia wananchi. Tumalize  umasikini, ujinga na maradhi, tusiweke siasa linapokuja suala la utendaji serikalini, tuwe wasikivu kidogo.”

Kwa takribani siku 412 tangu atenguliwe akiwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, Chalamila alikuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa mahubiri na kuimba nyimbo mbalimbali.


Miongoni mwa nyimbo hizo ni wa ‘Galilaya Yesu alitembea juu ya maji kwa uweza wa Mungu’. Picha nyingine ya video alionekana akiimba ‘Tukimaliza kazi tutavalishwa taji’.

Kauli yake ya kuwataka wananchi kujitokeza na mabango hata yenye matusi katika ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza, ilidaiwa kuwa sababu za kutumbuliwa kwake. Kauli hiyo ya Chalamila ilikuja siku chache baada ya Rais Samia kuonya tabia za ulipukaji kwa viongozi aliowateua.

MAONI YA WACHAMBUZI

Baadhi ya wachambuzi walitoa maoni yao akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Paul Loisulie, aliyesema walioteuliwa wameaminika kuleta hali mpya kwenye serikali.

“Waliobakizwa kwenye mikoa bado wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa kuwa wamemudu. Walioachwa huenda viatu vimewabana, kwa kuwa jukumu walilopewa huenda hawatimizi wajibu wao kama inavyotarajiwa na Rais na wananchi,” alisema.


 
Kuhusu Chalamila, alisema: “Chalamila aliondolewa kwenye nafasi na amerudishwa. Kwa  wakati ule ilionekana apumzike lakini kwa sasa ameonekana anafaa kurudi. Kwa ujumla, uteuzi huu unatafsiri mbalimbali lakini lengo ni kupata watu ambao watamsaidia kutekeleza ahadi kwa wananchi.”

Naye mchambuzi wa siasa, uchumi na jamii, Jawadu Mohamed, alisema Rais anapanga serikali yake vizuri ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

JINSIA YAZINGATIWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, alipongeza uteuzi uliofanywa na Rais Samia kwa kile alichosema ametekeleza kwa vitendo kile alichoahidi hasa kuongeza idadi ya wanawake.

“Katika nafasi hizi alizozitoa kwa wakuu wa mikoa, tunamshukuru kwa sababu wanawake wameongezeka japo kidogo. Tunachosisitiza, tunatamani vitu vya kudumu na endelevu vifanyike,” alisema.


Mchambuzi wa siasa , Gwandumi Mwakatobe, ambaye pia ni muumini wa harakati za kijinsia, alisema wanapozungumzia usawa wa kijinsia, hawazungumzii namba, bali mtu yeyote apewe nafasi kulingana na weledi, sifa na uwezo alio nao na si jinsi.

“Asiteuliwe mtu kwa sababu ni mwanamke. Ateuliwe  kwa sababu ana uwezo kuwazidi wengine. Tuangalie  anayefanya kazi pale ni kwa sababu ana sifa na uwezo wa kuleta matokeo mazuri na si kwa sababu ni mwanamke au mwanamume. Vigezo  vya maumbile visitumike kitumike kigezo cha weledi, sifa na uwezo alionao mtu,” alisisitiza.

UTEUZI USIKU WA MANANE

Alfajiri ya jana, Rais Samia alifanya uteuzi wa wakuu hao pamoja na makatibu tawala wa mikoa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia amefanya uteuzi huo wa watu wapya, kuwahamisha vituo vya kazi huku wengine wakitemwa.

WALIOTEMWA

Wakuu wa Mikoa waliotemwa ni Stephen Kigaigai (Kilimanjaro), David Kafulila (Simiyu), Robert Gabriel (Mwanza), Ally Hapi (Mara), Brigedia Jenerali Marko Gaguti (Mtwara), Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (Ruvuma), Meja Jenerali Charles Mbuge (Kagera), Dk. Binilith Mahenge (Singida) na Joseph Mkirikiti (Rukwa).


 
Kwa upande wa Makatibu Tawala wa Mikoa miongoni mwa walioachwa ni Prof.Faustine Kamuzora(Kagera),

WALIONG’ARA

Walioteuliwa ambao waliwahi kushika nafasi hizo na wamerejea baada ya kukaa benchi kwa miaka kadhaa na mikoa mipya kwenye mabano ni Fatma Mwasa (Morogoro) na Halima Dendego (Iringa).

Wengine waliong’ara na mikoa kwenye mabano ni Nurdin Babu (Kilimanjaro), Dk. Raphael Chegeni (Mara), Peter Serukamba (Singida), Kanali Ahmed Abbas Ahmed (Mtwara), Kanali Laban Thomas (Ruvuma) na Dk. Yahaya Nawanda (Simiyu) 

Kanali Ahmed, Kanali Thomas, Nurdin Babu, na Dk. Nawanda kabla ya uteuzi huo walikuwa wakuu wa wilaya za Kibiti, Nyasa, Longido na Tabora.

Kwa upande wa Ma-RAS, Kamishna Dk.Mussa Ali Mussa (Morogoro), Prof. Godius Kahyarara (Geita), Alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhandisi Leonard Masanja (Iringa), alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Tanesco mkoani Dar es Salaam, Toba Nguvila (Kagera) alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Elikana Balandya (Mwanza), alikuwa Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango, Prof. Siza Tumbo (Shinyanga), alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Dk. John Mboya (Tabora), alikuwa Kamishina wa Idara ya Bajeti katika Wizara ya Fedha na Mipango.

WALIOHAMISHWA VITUO

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amehamishiwa Njombe, Queen Sendiga amehamishiwa Rukwa akitokea Iringa, Waziri Kindamba amekwenda Songwe kutoka Njombe, Martine Shigella amepelekwa Geita akitokea Morogoro.

Wengine ni Omary Mgumba kutoka Songwe kwenda Tanga, Adam Malima (Tanga kwenda Mwanza) huku Rosemary Senyamule akihamishiwa Dodoma kutoka Geita.

Kwa upande wa Ma-RAS, Missaile Musa amekwenda Arusha akitokea Songwe, Rehema Madenge amehamia Dar es Salaam kutoka Lindi, Hassan Rugwa (Dar es Salaam kwenda Katavi), Ngusa Samike (Lindi kutoka Mwanza).

Wengine ni Msalika Makungu (Mara kutoka Tabora), Albert Msovela (Mara kwenda Kigoma), Rodrick Mpogolo (Katavi kwenda Mbeya), Zuwena Jiri (Pwani kutoka Shinyanga) Happiness Seneda (Iringa kwenda Songwe) na Rashid Mchata (Kigoma kwenda Rukwa).

WALIOBAKI VITUONI

Wakuu wa mikoa waliobaki vituoni ni Amos Makala (Dar es Salaam), John Mongella (Arusha), Mwanamvua Mrindoko (Katavi), Makongoro Nyerere (Manyara), Zainab Telack (Lindi), Juma Homera (Mbeya), Thobias Andengenye (Kigoma), Sophia Mjema (Shinyanga), Balozi Batilda Burian (Tabora) na Abubakar Kunenge (Pwani).

Ma-RAS waliobaki ni Dk. Fatuma Mganga (Dodoma), Karolina Mthapula (Manyara), Abdallah Malela (Mtwara), Judica Omary (Njombe), Willy Machumu (Kilimanjaro), Steven Ndaki (Ruvuma), Dorothy Mwaluko (Singida), Prisca Kayombo (Simiyu) na Pili Mnyema (Tanga).


Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments