Sintofahamu gharama za ARV nchini 
Dar es Salaam. Imefahamika kuwa kila mwathirika wa virusi vya Ukimwi anayetumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo (ARV) hutumia dawa zenye thamani mpaka Dola 58.20 ambazo ni wastani wa Sh135,780 kwa kila mwezi.

Hii ni kwa mujibu wa mahesabu ya bei ya dawa ya kiwandani, inamaanisha kuwa kulingana na idadi ya waathirika wanaotumia dawa za kufubaza makali ya VVU nchini ambao ni 1,507,686, ikiwa Tanzania itagharamia fedha za kununua dawa, itahitaji Sh204.713 bilioni kwa mwezi mmoja pekee.

Hayo yameibuka siku moja tangu gazeti hili lichapishe habari kuhusu ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Ukimwi (Unaids) iliyobainisha kuwa wafadhili waliotunisha mfuko wa kushughulikia Ukimwi, malaria na kifua kikuu (Global Fund) wameanza kuelekeza fedha nyingi kwenye maeneo mengine ambayo yamesababisha mdororo wa kiuchumi.

Wataalamu wamesema kuwa gharama hizo ni kwa ajili ya dawa za ARV pekee kwa mwezi, huku kukiwa na gharama nyingine za vipimo na afua nyingine, ikiwemo ushauri na kuonana na wataalamu wa afya, mbali na huduma nyingine za kukinga na kuelimisha jamii juu ya ugonjwa huo.


 
Meneja mwandamizi wa programu kutoka shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (Egpaf) la nchini, Dk Juma Songoro aliliambia Mwananchi kuwa mgonjwa mmoja hutumia Dola za Marekani 58.20, sawa na Sh135,780 kwa mtu mzima na Dola 9.50 sawa na Sh22,163 kwa mtoto mdogo kwa ajili ya dawa za kufubaza makali pekee.

Gharama hizo ndizo hutumika kimataifa, imeelezwa kuwa huendelea kupungua kutoka kiwandani mpaka kumfikia mlaji kutokana na ufadhili mbalimbali.

Hata hivyo, Mkuu wa kitengo cha habari serikalini Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Nadhifa Omary aliliambia Mwananchi kuwa mgonjwa mmoja anayetumia dawa za kufubaza makali ya VVU hutumia kiasi cha Dola za Marekani kati ya 112 mpaka 120, sawa na Sh 261,296 hadi Sh279,960 kwa mwaka.


Akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2022/23, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hadi kufikia Desemba 2021, Tanzania ilikuwa na jumla ya watu 1,795,905 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya Ukimwi, kati ya hao 1,507,686 walikuwa wameanza kutumia dawa za kufubaza makali.

Alisema wanaotumia dawa kinga ya PreP ni walengwa 13,285 na kwamba Serikali ilitenga Sh26.608 kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.

Kwa kuzingatia ushahidi mpya uliotathmini faida na hasara, Julai 22, 2019 Shirika la Afya Duniani (WHO), katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi, lilipendekeza matumizi ya dawa za Dolutegravir (DTG) kama njia ya kwanza na ya pili ya matibabu inayopendekezwa kwa watu wote ambapo vidonge vya siku 30 hugharimu Dola 58.20.

Mapendekezo

Katika kupambana na hali hiyo, wadau wamependekeza Serikali iweke mfumo rafiki wa uwazi utakaotoa ripoti ya kila mwaka kuhusu mapato na matumizi ya fedha zinazoshughulikia VVU, ikiwemo kutengeneza mfumo utakaokusanya rasilimali fedha za ndani kushughulikia janga hilo.

Akitoa maoni yake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Taifa wa wanawake wanaoishi na VVU Tanzania (NNW+), Veronica Lyimo alisema ili wadau hata mtu mmoja mmoja na sekta binafsi wachangie ni vema kuwe na uwazi katika rasilimali fedha, namna ya utendaji kazi, kuboresha kwenye mapungufu ili kuondokana na hali ya utegemezi kutoka kwa wafadhili.

Lyimo alisema kuna haja ya kuboresha bajeti inayotengwa na Serikali, kutunisha mfuko wa kupambana na VVU na vyanzo vingine vya mapato kutoka sekta binafsi na wachangiaji wa mfuko, ili kuwe na mfuko ambao wafadhili watajitokeza.

Kwa upande wa Meneja wa Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (ATF), Peter Kivugo alisema bado hakuna mwamko wa uchangiaji wa mfuko huo, juhudi mbalimbali zinaendelea na hivi karibuni waliingia makubaliano na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na wamekuwa wakifanya nao kazi.

______

Usikose Elimu ya pesa ni muhimu mno,na zaidi ukilipia Tsh 1000 ebook hapo Chini unaweza kushinda Tsh Laki moja bofya HAPA 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Below Post Ad