Madereva wa Viongozi wa Serikali Waonywa




Iringa.Kamanda Polisi Mkoani Iringa, Allan Bukumbi amesema wapo baadhi ya madereva wa Serikali ambao wanaendesha kwa kiburi magari yao huku wakivunja sheria za usalama barabarani kwa sababu ya namba za STL, SM, PT na viongozi wanaowaendesha na sio taaluma.

Amesema baadhi ya madereva hao wanajiamini kuzidi kiwango huku wakifanya makosa licha ya kujua wazi kwamba wanavunja sheria za usalama barabarani na kuhatarisha maisha ya wengine.

Kamanda Bukumbi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya madereva wa Serikali ili kuwakumbusha utii wa sheria za usalama barabarani na udereva wa kujihami utakaosaidia kupuza ajali.

“Sisi madereva wa Serikali ndio wenye matatizo, baadhi yao wengi wanafanya vizuri. Yaani wao kinachowafanya waendeshe magari na kile kiburi cha kuvunja sheria ni kwasababu wanamuendesha kiongozi fulani au ofisa fulani,” amesema.


Kamanda Bukumbi amesema jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kuvunja sheria za usalama barabarani bila kujali anamuendesha nani.

“Kwa kuendesha gari bila utii unakuwa kwanza unamdhalilisha kiongozi unayemuendesha kwa sababu dereva anafanya hovyo hovyo hata kiongozi tunamtafsiri kwamba na yeye ni wa hovyo hovyo kwa sababu anapaswa kumsimamia dereva wake,” amesema Bukumbi.

Amesema kama dereva anavunja sheria na kiongozi wake anamuona lakini hachukui hatua maana yake anaidhalilisha nafasi yake, taasisi na idara anayofanyia kazi.


Awali, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mkoani Iringa, Mosi Ndozelo amesema hakuna dereva aliye juu sheria.

Amesema madereva wa Serikali wanapaswa kutii sheria zilizopo na kwamba wanaamini mafunzo hayo yatawabadilisha mtazamo.

“Wanaojiona wapo juu ya sheria kupitia mafunzo haya wataweza kubadilika, tunataka kuwabadilisha wenye mawazo mgando kwamba wakiendesha viongozi au magari ya Serikali basi wapo juu ya Sheria,” amesema.

Kwa upande wao baadhi ya madereva walisema sio wote wanaovunja sheria za usalama barabarani japo baadhi yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa kivuli cha viongozi au namba za magari wayayotumia.


“Binafsi najua natakiwa kuwa kioo na kwa kweli huwa sipendi kuvunja sheria, natumia udereva wa kujihami ambao naweza kuepusha ajali kwangu na wanaonizunguka,” amesema Mohamed Maghembe, derva wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini

💥NAFASI ZA AJIRA ZILIZOTANGAZWA LEO SERIKALINI

💥NAFASI ZA AJIRA ZILIZOTANGAZWA LEO SEKTA BINAFSI

💥NAFASI ZA INTERSHIP MAKAMPUNI MBALI MBALI

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad