Ishu nzima ya Muharami kudakwa iko hivi... Serikali yanena

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



BAADA ya kukosekana mazoezini na kambini kwa wiki zaidi ya mbili, jana yamefichuka makubwa ya aliyekuwa Kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultan ‘Shilton’ (40). Ni miongoni mwa watuhumiwa 11 wa dawa za kulevya waliotajwa jana na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), ambapo ilieleza kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na biscut 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Mbali na kocha wa makipa wa Simba, wengine waliokamatwa ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi Seif na John John maarufu Chipanda(40) ambaye jukumu lake ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy

Wengine ni Said Matwiko mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu mbonde(54) mkazi wa Kisemvule, Rajabu Dhahabu (32)) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24) mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi(24) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa kongowe

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya alisema watuhumiwa waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine walikamatwa maeneo mbalimbali nchini.


Alisema tukio lingine DCEA imemkamata Abdulnasir Haruon Komba (30) mkazi wa Kaloleni Jijini Arusha akiwa na biscut 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni pamoja na Hassan Ismail(25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha anayesadikiwa ndiye mtengenezaji wa biscuti hizo zenye dawa za kulevya hizo.

“Ukamataji huu unafanyika kufuatia operesheni endelevu tunazozifanya katika maeneo mbalimbali nchini, mwanzo tulikamata mtu mmoja hadi kufikia idadi hiyo na watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika,” alisema Kusaya.

Mwanaspoti limedokezwa kuwa Shilton alikamatwa takribani wiki mbili zilizopita akiwa kwenye kambi ya timu hiyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam akiwa kwenye majukumu ya kazi timu hiyo ilipokuwa ikijiandaa na moja ya mechi za Ligi Kuu huku mmiliki wa Cambiasso yeye alikamatwa wiki tatu zilipopita kwa mujibu wa mtu wa karibu wa kituo hicho ambaye ameomba hifadhi ya jina licha ya kubainisha kwamba, majukumu mengine ya klabu yanaendelea kama kawaida licha ya bosi wao kukamatwa.


Cambiasso ni moja ya akademi za soka zilizojipambanua kwa muda mrefu, ikiwa na historia ya kuibua na kuendeleza vipaji, miezi ya karibuni imecheza mechi kadhaa na kirafiki na klabu mbalimbali ikiwamo za Simba na Yanga, lakini mwezi Julai iliandaa mashindano yao ya Cambiasso U20 na kualika timu za Barani Ulaya.

SIMBA WAFUNGUKA

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu alisema; “Watu watulie, kocha Muharami alikuwa kwa muda Simba,” alisema Mangungu jana akifichua zaidi kwamba kocha huyo alikuwa Simba kwa muda.

“Alikuwa kwenye benchi letu kwa mechi kadhaa, ikiwamo ya Malawi (Simba walicheza na Nyassa Big Bullets) na kwenye mechi na Angola, lakini yule ni kocha wa Cambiasso, kilichotokea ni masuala yake binafsi,” alisema Mangungu.

MATUKIO KAMA HAYO MICHEZONI

Tukio kama hilo limewahi kuikumba familia ya michezo mwaka 2008, baada ya timu ya taifa ya ngumi za ridhaa kukamatwa nchini Maurtius wakituhumiwa kula njama na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine ilipokwenda kuweka kambi kujiandaa na Olimpiki ya msimu huo iliyofanyika China.


Bondia Emmilian Patrick aliyekuwa amefuzu Olimpiki na kocha Nassor Michael waliachiwa huru miaka kadhaa baadae, wakati bondia mwingine, Petro Mtagwa aliyekwenda kama msaidizi wa mazoezi ‘Sparing patner’ na wengine wawili, wakihukumiwa kifungo cha miaka 15 nchini humo tangu Agosti 20, 2016. Hapa nchini, aliyekuwa rais wa Chama cha Ngumi, Alhaji Shaban Mintanga pia aliachiwa huru.

Septemba 2013, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Joseph Kaniki na bondia, Mkwanda Matumla walikamatwa nchini Ethiopia kwa wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya wakiwa uwanja wa ndege wa Bole, Addis Ababa wakiajiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ethiopia wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa. Kaimu Balozi wa Ethiopia Samuel Shelukindo alithibitisha tukio, wanamichezo hao walihukumiwa miaka saba na nusu jela.

WADAU, SERIKALI ZANENA

Nassor Maiko alisema matukio hayo michezoni yana athari kubwa akitolea mfano yeye alipokamatwa nchini Maurtius akiwa ndiye mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania.

“Hadi kuachiwa huru ni Mungu tu, mimi ndiye nilikuwa mkuu wa msafara kwenye ile safari, lakini hadi tunakamatwa hotelini sikujua chochote, alianza kuachiwa Emmilian, kisha baadae mimi kwa kuwa hatukuwa na hata cha kujitetea mahakamani, wenzetu walibaki kule na hadi sasa wantumikia kifungo.


“Ila ninachoweza kusema matukio haya si mazuri, yanachafua taswira ya michezo inapobainika ni kweli tukio hilo limetendeka,” alisema Nassor kocha na bondia wa zamani wa timu ya taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini, Ally Mayay alisema sakata la kocha wa makipa wa Simba na wenzake japo mpaka sasa bado ni tuhuma, lakini kwa viogozi linapaswa kuwaamsha na kuwakumbusha suala la maadili kwa watu wanaodili nao. “Hilo ni suala binafsi, lakini linapogusa wadau wa tasnia fulani kuna mguso fulani, hivyo niwakumbushe tu viongozi na wadau wengine kwenye michyezo kuzingatia maadili na watu inayodili nao.”


Mwanaspoti
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad