Tume Yamtaja Makonda Matumizi Mabaya ya Madaraka

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa

Dodoma. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imemkuta na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda aliyeagiza mwananchi mmoja kukamatwa na kuwenda rumande saa 96 bila kufunguliwa mashtaka.

Pia imesema, Makonda alipoitwa mbele ya tume kuwasilisha utetezi wake alikaidi.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Julai 19, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora kwa mwaka 2022/23.

Amesema tume ilipokea malalamiko dhidi ya Makonda katika uchunguzi wa kutoa amri ya kukamatwa na kuwekwa ndani ya mahabusu ya polisi mkazi mmoja wa Arusha (hakutajwa jina).

Amesema Tume baada ya uchunguzi imebaini amri iliyotolewa na mkuu wa mkoa haikuwa halali na haikuzingatia aina ya makosa na taratibu ulioainishwa kisheria wa utekelezaji wa mamlaka hayo na kwamba mwananchi huyo hakuwa muhusika wa madai ya msingi, ambayo Makonda aliyatumia kushughulikia suala lililokuwa mbele yake.

“Ilibainika pia kuwa mkuu wa mkoa huyo alivuka mipaka ya majukumu yake kwa kushughulikia na kutoa maamuzi katika suala ambalo lilipaswa kufuata mkondo wa kisheria wa kimahakama kwa kuwa madai hayo yangeshughulikiwa kama shauri la daawa,” amesema Jaji Mwaimu.

“Aidha, hata kama kulikuwa na viashiria vya makosa ya kijinai, njia sahihi ingekuwa ni kulielekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.”

Amewataka viongozi wa umma kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao na si kujichukulia sheria mkononi.

Jaji Mwaimu amesema tume pia imebaini kutozingatiwa kwa haki za mtuhumiwa kwa kuwekwa mahabusu kwa saa 96 (sawa na siku nne) bila ya kufunguliwa mashtaka.

“Pamoja na kuitwa kutoa maelezo mbele ya tume ili kuwasilisha utetezi wake, mkuu huyo wa mkoa (Makonda) alikaidi kufika mbele ya Tume,” amesema Jaji Mwaimu.

Amesema lakini hilo halikuweza kuzuia tume kutekeleza majuku yake kwa sababu ni taratibu tume inapowaita wahusika katika kutoa ile haki ya kusikilizwa, kwamba mtu ametoa, kwa hiyo tume ni lazima itoe fursa ya wewe kusikilizwa pia unasemaje kuhusu tuhuma zinazokukabili.

“Kwa hiyo, ukikataa kufika mbele ya tume na kutoa maelezo, haituzuii tume kuendelea kufanya shughuli zetu na kukamilisha uchunguzi,” amesema Jaji Mwaimu

Jitihada za Mwananchi kumpata Makonda kwa simu yake ya mkononi hakupatikana kujua kwa nini hakwenda na kuhusu tukio hilo tanjwa

Jaji Mwaimu amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23 tume imepokea malalamiko 1,524 ambapo ilihitimisha jumla ya malalamiko 789 na kufanya malalamiko yaliyoendelea kuanzia Julai 1, 2023 kuwa ni 885.

Katika hatua nyingine, Jaji Maimu amesema uchunguzi dhidi ya madai ya Mbunge wa Babati (CCM), Pauline Gekul na wenzake kudaiwa kuwafanyia vitendo vya ukatili na udhalilishaji vijana wawili waliokuwa wafanyakazi wake, hayakuweza kuthibitishwa.

Amesema tume hiyo ilifanya uchunguzi wa tuhuma hizo zinazodaiwa kufanywa na Gekul aliyedaiwa kutenda kosa hilo Desemba 2023 kwa Hashim Philemon na Michael Marishamu kwa kuwaingizia chupa sehemu ya haja kubwa ili waseme ukweli, kuhusu kumwekea sumu kwenye chakula na kuweka vitu vya uchawi kwenye hoteli yake ya Paleii Lake View.

Mwenyekiti huyo amesema baada ya uchunguzi, tume kwa kuzingatia maelezo ya watu mbalimbali waliohojiwa na vielelezo ambavyo tume imevipitia haikubaini suala hilo kufanyika.

“Hata hivyo tume ilibaini walalamikaji walizuiliwa kwa muda mrefu wakati wakihojiwa na mlalamikiwa kuhusu tuhuma za kutaka kumwekea sumu (Pauline Gekul) pamoja na kupeleka madawa ya kishirikina katika hoteli yake na hivyo kusababisha walalamikaji kukosa haki yao ya kuwa huru,” amesema Jaji Mwaimu.

Source: Mwananchi 
_________

 Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad