Katibu Mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna ametaka kujiuzulu kwa wanachama wa chama hicho ambao wameteuliwa na Rais William Ruto kujiunga na baraza lake la mawaziri.
Akizungumza siku ya Alhamisi Julai 25, 2024 kupitia kituo cha runinga cha Citizen TV, Sifuna amesema kuwa wanachama hao wanne wa ODM hawakupendekezwa kujiunga na serikali ya Ruto na uteuzi wao hauwakilishi wadhifa wa chama hicho.
Kinara huyo wa kisiasa amedai kuwa wajumbe hao wanapaswa kuwasilisha barua zao za kujiuzulu kabla ya kwenda kuchunguzwa bungeni.
"Je, tulijua watu walikuwa wakijadiliana na Ruto, ndio tulijua. Ni kitu kinafanywa rasmi kupitia miundo ya chama, hapana. Je, tuliidhinisha uamuzi wa watu hawa wanne kujiunga na serikali, hapana. Sio uamuzi wa ODM” Amesema Sifuna.
Sifuna ameendelea kudokeza kuwa uteuzi wa wanne hao pia haukuidhinishwa na kinara wa chama Raila Odinga ambaye anaaminika kuwa katika mazungumzo na serikali ya Ruto, na kuendeleza serikali ya mseto.
Amesema ikiwa mkono wa Raila ulihusika katika mapatano hayo yaliyokisiwa, kungekuwa na usawa wa kijinsia katika uteuzi huo.
"Hata rais mwenyewe hakuwahi kusema alishauriana na Raila. Hajawahi kusema alishauriana na ODM alisema tu majina ya watu aliowateua na ni haki yake kama Rais" alibainisha Sifuna.
Wakati akitangaza kundi la pili la walioteuliwa kwenye Barazalake la Mawaziri, Rais Ruto aliteua wanachama wa ODM John Mbadi, mbunge aliyependekezwa katika wizara ya Hazina, Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi kwenye Nishati, aliyekuwa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Bluu), na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya (Ushirika).
Hii ilikuwa takriban saa 24 baada ya Sifuna kufafanua kuwa ODM haikuwa ikijadiliana kuhusu makubaliano yoyote ya muungano au kushawishi kuteuliwa na serikali ya Ruto.
Ripoti kwamba Ruto alimpa Odinga nafasi tano za Baraza la Mawaziri licha ya kutofautiana ndani ya upinzani kuhusu kushirikiana na serikali pia zilivumishwa.
Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA