Simba na Yanga ni timu zilizokamilisha usajili wa idadi ya nyota 12 wa kigeni, Wekundu wakinasa mastaa saba wapya wanaoungana na watano waliosalia kutoka kikosi cha msimu uliopita, wakati Wananchi wameongeza silaha tano mpya zinazoungana na wengine saba waliosalia kikosi kilichopita.
Katika dirisha la usajili lililo wazi kwa sasa hadi Agosti 15, imeshusha mabeki wawili akiwamo wa kushoto, Valentin Nouma na yule wa kati, Chamou Karabou, viungo Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha pamoja na washambuliaji Joshua Mutale na Steven Mukwala.
Nyota hao wanaungana na kipa Ayoub Lakred, beki Che Fondoh Malone, kiungo Fabrice Ngoma na washambuliaji Willy Onana na Freddy Michael.
Hivyo kama kocha Fadlu ataamua kuanza na kikosi kitupu cha wageni basi atamkosa beki wa kulia tu, lakini mziki mzima utakuwa umekamilika kwa kuanza na Ayoub aliyeongeza mkataba wa mwaka mmoja, huku kushoto akiwa na Nouma na mabeki wa kati watasimama Che Malone na Karabou.
Eneo la kiungo Simba itaweza kuanza na Ngoma akisaidiwa na nyota watatu wapya Debora, Okejepha na Joshua Mutale, wakati safu ya ushambuliaji itakuwa chini ya Jean Ahoua na Steven Mukwala wakati Freddy ataanzia benchi kabla ya kuingizwa baadae kuliamsha.
Kwa Yanga, inayoshikilia mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo, imesajili beki Chadrack Boka,viungo Clatous Chama aliyekuwa Simba na Duke Abuya aliyekuwa Singida BS, huku eneo la ushambuliaji kukiwa na Prince Dube kutoka Azam FC na Jean Baleke aliyewahi kuwika na Simba.
Nyota hao wanaounga na kipa Diarra Djigui, Yao Kouassi, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz KI na Kennedy Musonda waliokuwapo msimu uliopita, hivyo kama Gamondi ataka kujibu mapigo ya Fadlu ya kushuka na nyota wa kigeni watupu, basi ni eneo la beki ya kati ndio atakuwa na mapengo kwani haitakuwa na namba nne wala tano, baada ya Gift Fred kutemwa kikosini.
Langoni Yanga itaanza kama kawaida na kipa namba moja, Djigui Diarra, beki wa kulia akiwa ni Yao, huku kushoto akisimama Boka, lakini italazimika kuwaingiza Bakar Mwamnyeto, Dickson Job au Ibrahim Bacca, kucheza beki ya kati.
Kwa eneo la kiungo Gamondi ana mashine za maana kama Aucho, Maxi, Pacome, Chama na Abuya, japo atalazimika mmoja kumuanzisha benchi ili kupata uwiano mzuri, huku katika eneo la mbele la ushambuliaji anaweza kumtumia Aziz KI na Dube, huku Baleke na Musonda kuanzia benchi au kinyume chake, kwani katika eneo hilo kama ilkivyo kwa kiungo kumejaa mafundi watupu wa kumrahisishia mambo.
CHAMA LA WAZAWA KWA KILA TIMU
Hapa sio Yanga wala Simba wote wamekamilika na hakuna haja ya makocha kuahangika kama ilivyokuwa kwa vikosi vya nyota wa kigeni watupu. Tuanze na Yanga, hapa Gamondi anaweza kuanza na Abubakar Khomeiny au Aboutwalib Mshery, huku beki wa kulia akisimama Kibwana Shomari na kushoto kuna Nickson Kibabage wakati mabeki wa kati anaweza kumgtumia Job na Bacca, huku Mwamnyeto akasubiri.
Viungo atakuwa na machaguo yua kutosha kwani ana Jonas Mkude, Mudathir Yahya, Denis Nkane ambaye huenda hapa atapata nafasi baada ya kusugua sana benchi na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, huku Aziz Andambwile akisubiri nje wakati washambuliaji watakuwa ni Clement Mzize na Farid Mussa.
Kwa upande wa Simba huko ndiko kuna balaa zaidi, kwani Kocha Fadlu anaweza kuanza langoni na Ally Salim au Hussein Abel, wakati beki wa kulia akiwa Shomary Kapombe, Kelvin Kijiri au David Kameta ‘Duchu’, huku kushoto kuna nahodha Mohamed Hussein ‘Tshabalala na kati wakiwa Abdulrazack Hamza na Hussein Kazi.
Safu ya kiungo itakuwa chini ya Yusuph Kagoma, Mzamiru Yassin, Ladack Chasambi, Awesu Awesu huku Omary Omary akisubiri nje na kule mbele wataanza Kibu Denis na Edwin Balua na Valentino Mashaka itabidi asubiri benchi ama kinyume chake kwani wote wanaonekana ni moto mkali.
KAMA WAKIHITAJI MSETO NI BALAA
Kama makocha wote wawili wataona jahu kuanza na vikosi vya wachezaji wa sampuli moja, basi hapa watafanya mseto wa maana unaozalisha kikiosi kikali zaidi na balaa ndipo linaweza kutokea kama inavyokuwa siku zote zinapokutana timu hizi za Kariakoo zilizotawala soka la Tanzania Afrika Mashariki.
Timu zote zinaweza kuwa na vikosi vizito zaidi endapo zitachanganya wazawa na wale wa kigeni na kila moja ikawa na mziki mzito utakaosumbua ndani na nje na hapo Kwa Mkapa siku ya Nane Nane moto utawaka kwelikweli, kwani zote sasa zinaweza sasa kupangwa bila tatizo kuanzia langoni hadi mbele.
Yanga ya Gamondi inaweza kuanza na mziki huu, Diarra, Yao, Kibabage, Bacca na Job kama ambavyo walianza juzi dhidi ya FC Augsburg, huku eneo la kiungo akasimama Aucho, Andambwile,Mudathir au hata Mkude wawili kati ya hao, kisha juu yao akacheza Chama, Maxi wakati mbele kukiwa na Aziz Ki na Baleke au Dube. Usisahau benchi kutakuwa na mashine nyingine za maaana kama Pacome, Mzize, Musonda na Abuya.
Kwa upande wa Simba sasa hapo Fadlu atalipanga jeshi kwa kikosi kitakachoundwa na Ayoub, Kapombe, Tshabalala, Che Malone, Karaboue, huku viungo wakiwa Ngoma, Kagoma, Mutale na Okejepha wakati eneo la mbele litakuwa na Mukwala na Ahoua.
Mashine nyingine kama Freddy, Kibu, Balua, Chasambi na wengine zitasikilizia pale watakapoiunuliwa ili kwenda kuwapokea wenzao.
Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA