Ateba Aanza na Bao, Simba ikibanwa Mbavu

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa

 


Straika mpya wa Simba, Leonel Ateba ameanza kufungua akaunti ya mabao katika kikosi hicho, baada ya jioni ya leo Jumamosi, kutupia bao katika sare ya 1-1 iliyopata timu hiyo mbele ya Al Hilal ya Sudan.


Katika mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, nyota huyo amefunga bao hilo dakika ya 25, likiwa ni la kwanza kwake tangu ajiunge hivi karibuni akitokea USM Alger ya Algeria kabla ya Al Hilal kulichomoa dakika ya 76 kupitia Serge Pokou.


Nyota huyo raia wa Cameroon, amecheza mchezo wa kwanza huku akibeba matumaini makubwa ya timu hiyo katika eneo la ushambuliaji lenye washambuliaji wakali akiwemo Mganda Steven Mukwala aliyejiunga pia na kikosi hicho msimu huu akitokea Asante Kotoko ya Ghana, Valentino Mashaka kutoka Geita Gold.


Ateba aliyecheza kwa takribani dakika 60 katika mchezo huo, kisha kutolewa kumpisha Valentino Mashaka, ni pendekezo la kocha Fadlu Davids, amepata nafasi hiyo ikiwa ni maandalizi kwa kikosi hicho kujiandaa na mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.


Katika mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kati ya Septemba 13-15, Simba itaanzia ugenini Libya kisha kumalizia nyumbani zitakaporudiana kati ya Septemba 20 hadi 22 na mshindi wa jumla atatinga moja kwa moja hatua ya makundi ya michuano hiyo ili kusaka ubingwa unaoshikiliwa kwa sasa na Zamalek ya Misri.


Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Cotonsport na PWD Bamenda, anakumbukwa zaidi mwaka 2023, alipoibuka Mfungaji Bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, yaliyomfanya kuitwa kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika mapema mwaka huu Ivory Coast.


Ateba alijiunga na USM Alger Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon, huku msimu uliopita nyota huyo alicheza jumla ya michezo 23, katika mashindano tofauti tofauti ambapo alifunga jumla ya mabao matatu na kuasisti saba.


Kocha Fadlu alihitaji aletewe straika mpya kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti 15 akiwatema kikosini Willy Onana na Freddy Michael Kouablan aliyesajiliwa dirisha dogo la msimu uliopita na kufunga jumla ya mabao tisa yakiwamo sita ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho na moja la Kombe la Muungano.

_________

 Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad