Leo kwenye safu ya Dakika 5 ya Mwanaspoti tupo na msanii wa muziki wa Bongofleva, Gift Stanford ‘Gig Money’, ambaye hivi karibuni amekutana na majanga baada ya watu wasiojulikana ‘kuhaki’ akaunti yake ya YouTube na kushusha baadhi ya vitu vyake alivyoposti kwenye akaunti hiyo ambayo sasa hawezi kuingia na kuitumia.
Gigy amelizungumzia suala hilo na kusema sio mara ya kwanza kufanyiwa kitendo hicho na kwamba kwa sasa ameamua kuachana nalo hivyo “ikirudi au isiporudi ni sawa tu”.
“Nimechoka kila siku mimi tu, wana-hack akaunti, natumia pesa nyingi kuwalipa watu wa kuirudisha, kisha inavamiwa tena! Kwanini? Nimechoka. Sasa hivi wala sijali na wala sitaki kumjua aliyefanya hivyo, nimeamua kuacha hili jambo, sina muda wa kulifuatilia kwa bashasha, nafuatilia kimyakimya tena nikiwa na muda ikirudi sawa, isiporudi sawa tu pia,” amesema mwimbaji huyo wa ngoma ya ‘Kiki ni Gigy’.
Gigy Money hapendi nini?
“Mimi sipendi kuitwa chizi, nalichukia sana hili jina, mimi sio chizi wanaoniita chizi wao ndio machizi sababu hawanielewi mimi ni mtu wa namna gani? Mimi nina akili timamu sitaki watu wanihukumu na kuniona kama sijielewi, kuna muda napenda kuchangamsha watu, yaani napanga kabisa kufanya jambo fulani kwa nia ya kutrendi tu basi. Utakuta kuna vitu huwa navifanya kwa makusudi kabisa na natrendi sana mjini. Sio kwamba sielewagi nini nafanya, nakuwa naamua tu.”
Vipi bifu lako na Zuchu limekwisha?
“Sitaki kuzungumzia mtu au watu waliotoka kichwani kwangu, ngoja nikukatize kwanza, sitaki kumzungumzia Zuchu wala Diamond Platnumz najua unachotaka kuuliza hivyo sitaki, mimi sasa hivi nakuwa mbali na watu waliopo kwenye uhusiano, nikijua mpo kwenye uhusiano nakaa mbali, siangalii kama ulishawahi nisaidia hapo nyuma, na haikuandikwa mtu akikusaida basi ndio uendelee kumnyenyekea milele, hata kama akikukosea basi unakaa kimya tu, saa hizi nina maisha yangu na watu wangu wengine wapya.
“Embu kwanza niulize habari ya Harmonize na Ali Kiba, ni watu wangu wa nguvu sana sina bifu nao hata mmoja kati ya hawa, nawapenda na wananipenda sana, na wapo wasanii wengi tu wananipenda.”
Uko kwenye uhusiano?
“Mimi hata sijui kama nipo kwenye uhusiano, maana mpenzi niliye naye sasa haeleweki, mara tupo pamoja mara hatupo pamoja, kiufupi liuhusiano langu halieleweki au siko kwenye uhusiano.”
Unapenda mwanaume wa namna gani?
“Napenda mwanaume anayenijua tabia yangu, yaani Gigy Money wakati mwingine ndio na wakati mwingine sio. Pia napenda awe na pesa, kama huna pesa mwanaume usinifuate kabisa, kwa sababu nishavuka levo za kulea wanaume ambao hawana pesa, ving’asti kwa sasa nimewachoka”.
Unapenda nini kwenye maisha yako?
“Mimi napenda sana urembo kuliko kitu kingine, nipo radhi nilale na njaa lakini nitumie pesa kufanya urembo.”
Mara ya mwisho kutoa wimbo mpya ni lini?
“Miezi miwili iliyopita, nimetoa wimbo unaitwa ‘Shemeji’ na video yake, na sio kwamba nimeacha muziki kama watu walivyokuwa wanasema, ila kutingwa na majukumu mengine najikuta naupotezea muziki”.
Usingekuwa msanii ungekuwa nani?
“Nisingekuwa msanii ningekuwa mwanasheria na ndio maana kuna kipindi fulani nilirudi shule kusoma masomo ya jioni somo la sheria kwa sababu ndiyo kitu ninachokipenda.”
Ni kweli tofauti zako na baadhi ya wasanii wenzako zinatokana na kuzungumziwa?
“Kwanini mtu anizungumzie? Tena unakuta mtu ananizungumzia vibaya kwanini nimpende? Mimi nishaitwa teja, mnafiki nina roho mbaya, chizi, mpenda pombe, bangi ila nilikuwa nakaa kimya kwa sababu ukiangalia wanaonizungumzia ni watu wangu wa karibu, nilivyoona tabia hii inazidi ya kuzungumziwa ndio nikaanza na mimi kuwazungumzia matokeo yake mimi naonekana mbaya, mkorofi napenda uadui.
“Wapo wasanii wengi tu tumekosana sababu ya kuzungumziana mambo mabaya, waongee wao tu, nikiongea mimi aaaaa...nakosea, mimi nina akili timamu najitambua na kujielewa sana kuliko wasanii wengine”.
Shabiki wa timu gani?
“Mimi sina timu, sijui mpira, mimi ni bendera tu kufuata upepo, ndio maana leo unaniona Yanga, kesho Simba na timu nyingine, ila nawapenda wachezaji ni wazuri wananifaa kwenye uhusiano sina tu bahati nao.”
Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA