KESI YA MPINA DHIDI YA SPIKA, MWANASHERIA MKUU KUSIKILIZWA LEO
Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, leo Jumanne, Septemba 24, 2024 imepanga kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhanga Mpina, dhidi ya Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi hiyo ya Kikatiba inayosikilizwa na Jaji Awamu Mbagwa, ilifunguliwa mahakamani hapo Julai 25 na kwa mara ya kwanza ilitajwa mahakamani hapo Agosti 28, 2024.
Mpina amefungua kesi akipinga utaratibu uliotumika kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge, akidai haukuwa halali na pia ni kinyume cha sheria na kanuni za Bunge.
Katika maombi yake, Mpina anaomba Mahakama hiyo ipitie na kuona uhalali wa uamuzi ambao Bunge hilo wa kumsimamisha kutokuhudhuria vikao 15 vya Bunge hilo.
Katika kesi hiyo, Mpina anawakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongoza na Mpare Mpoki, akishirikiana na Dk Rugemeleza Nshala, John Seka, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore na Edson Kilatu.
Kwa upande wa wajibu maombi katika shauri hilo ni Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pauline Mdendemi.
0 Comments