Msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop nchini na mwanasiasa, Joseph Haule maarufu Profesa Jay amekanusha taarifa za kuzushiwa kifo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza na Mwanachi leo Jumatatu Septemba 9, 2024, Profesa Jay amesema ni mzima wa afya njema na haumwi hata mafua, hivyo taarifa hizo ni za upotoshaji, hazina ukweli zipuuzwe.
"Mimi niko salama kabisa na hapa nipo nyumbani kwangu nimetulia wala siumwi hata mafua. Naomba hizo habari za kifo kuhusu mimi zipuuzwe kabisa na watu waendelee kusapoti kazi zangu. Pia nawaomba Mwananchi mnisaidie kukanusha hili kwa mashabiki zangu, najua mna nguvu kubwa ya kunisaidia kwenye hili," amesema Profesa Jay.
Msanii huyo alianza kupata umaarufu katika tasnia ya muziki miaka ya 2000 kupitia nyimbo zake zenye ujumbe wa kijamii, kama vile Zali la Mentali, Ndio Mzee zilizokuwa na mashairi yenye kuelimisha na kufundisha.
Mbali na muziki, Profesa Jay alijiingiza kwenye siasa, akichaguliwa kuwa Mbunge wa Mikumi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 2015.
0 Comments