Jeshi la Polisi mkoani Tanga linafanya uchunguzi wa vifo vya watu watatu waliokutwa wakiungua moto kwenye gari aina ya Toyota IST lenye namba T. 305 EAL katika msitu wa hifadhi ya Korogwe Fuel uliopo Wilaya ya Handeni.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Almachius Mchunguzi amesema walipokea taarifa ya kuungua kwa gari katika hifadhi hiyo jana Septemba 23, majira ya saa 3:45 usiku.
Baada ya askari kufika eneo la tukio, walikuta gari hilo linaungua moto huku pembeni yake kukiwa na miili miwili ya jinsia ya kike ikiwa imeungua moto na ndani ya gari, kiti cha nyuma, ulionekana mwili mwingine ambao umeungua moto hadi kupoteza sura na haujabainika ni wa jinsia gani.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi ili kubaini watu hao walioteketea kwa moto ni akina nani, nini kiliwatokea kabla ya umauti wao na waliofanya tukio hilo ni watu gani ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani,” amesema ACP Mchunguzi katika taarifa yake kwa umma.
0 Comments