Kocha Gamondi |
Baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kujikusanyia pointi tatu juzi, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema hatarajii kupata ushindi wa mabao mengi katika kila mechi. Kwake, muhimu ni kupata pointi tatu.
Kauli ya Gamondi inakuja baada ya baadhi ya mashabiki kuanza kuzungumzia ushindi mdogo wa bao 1-0 katika michezo yao miwili ya hivi karibuni ya Ligi Kuu. Juzi usiku, Yanga ilishinda mchezo dhidi ya KMC kwa bao moja pekee, huku ushindi kama huo ukipatikana pia katika mchezo wa awali dhidi ya KenGold FC.
"Sio kila mchezo utakuwa na idadi kubwa ya mabao. Tunapaswa kuzingatia pointi tatu. KMC walicheza vizuri, na ingawa hatujafunga mabao mengi, ni furaha kupata pointi tatu, ambayo ndiyo muhimu zaidi," alisema Gamondi.
Aliongeza kuwa kila timu inajitayarisha kufanya vizuri, na hivyo wanapambana uwanjani. "Ikipatikana nafasi ya kufunga mabao mengi, tutafanya hivyo, lakini muhimu ni kupata pointi tatu. Ingawa hatujafunga mabao mengi katika mechi hizi mbili, tumepata pointi zote," alisisitiza.
Katika mchezo wa juzi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, KMC walijitahidi kuwabana Yanga, lakini walishindwa kuzuia timu hiyo kuondoka na pointi zote tatu.
0 Comments