Dkt. Tulia Ackson Alilia Bunge Jina Lake Kutumika Kutapeli Watu Mitandaoni Kuwa Anakopesha
Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema amechoka kutoa taarifa za utapeli mtandaoni na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa licha ya kuwepo kwa Mamlaka ya mawasiliano Nchini (TCRA) na Watanzania wanaendelea kutapeliwa.
Dkt. Tulia amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo ameshangazwa na jambo hilo kuendelea kushamiri Nchini na kufika hatua ya kutumia sura za Watu maarufu ikiwemo yake kutapeli mitandaoni kwa kutumia akili mnemba [Artificial intelligence (AI)].
“nikisema ni Watu wangapi hapa Nchini wametapeliwa kwa jina langu na napata hizo jumbe mpaka nimeshachoka kutoa taarifa kwasababu nawaza, utapeli nimesharipoti lakini unaendelea na haya matangazo yao hayawekwi kifichoni Watu wanatangaziwa kwenye mitandao ya kijamii na wapo wameweka namba za simu na wanapigia Watu simu sasa na sasa hivi kuna akili mnemba Mtu anasema umenipigia simu na nimeongea na wewe, sasa mimi Spika naweza kumpigia Mwananchi nakopesha hela?” Spika Dkt. Tulia Ackson
Akisisitiza jambo hilo Dkt. Tulia amesema taarifa za utapeli kama huo hazipo kwenye Mataifa mengine na kwanini Tanzania limeshindikana na kuna Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA).
Akijibu hilo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema kwasasa utapeli umepungua kwa asilimia 19 na amewaomba Watanzia kuacha kubonyeza link wasiozijua na kutotoa namba za siri za miamala kwa Watu wasiozifahamu huku akiitaja Mikoa ya Rukwa na Morogoro ikiongoza kwa utapeli mitandaoni.
Aidha, Jerry Silaa ameielekeza mitandao ya simu Nchini kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi ya kukabiliana na utapeli mtandaoni.