Serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) yaliyotolewa kwenye tamko la Mkutano wa Dharura wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 31 Januari 2025.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo, Februari 2, 2025, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda, serikali imesisitiza kuwa RDF inalinda mipaka ya nchi dhidi ya vitisho na inawalinda raia, wala hailengi kushambulia raia kama inavyodaiwa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa SADC imetuma kikosi cha kijeshi cha SAMIDRC kusaidia vita vya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dhidi ya raia wake, hususan wapiganaji wa M23 na jamii yao, ambapo wengi wamekimbilia Rwanda na mataifa jirani kama wakimbizi.
Aidha, serikali ya Rwanda imesema kuwa DRC inalenga kuishambulia Rwanda na kupindua serikali yake, jambo ambalo Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, amekuwa akilitangaza mara kwa mara hadharani.
Rwanda imesisitiza kuwa SAMIDRC, kwa kushirikiana na wanajeshi wa Burundi, kundi la waasi la FDLR na mamluki wa Kizungu, wamekuwa sehemu ya mzozo huo na wanazidisha hali ya mgogoro badala ya kuleta utulivu.
"Taarifa za hivi karibuni kutoka Goma zinaonyesha ushahidi wa maandalizi ya mashambulizi dhidi ya Rwanda, ambayo yamepangwa kwa kushirikiana na vikosi vya kigeni vinavyopigana mashariki mwa DRC, vikiwemo FDLR. Malengo yao hayakuwa tu kushinda M23, bali pia kuishambulia Rwanda," inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Rwanda imeendelea kusisitiza hitaji la suluhisho la kisiasa kwa mgogoro huo na inakaribisha pendekezo la kufanyika kwa mkutano wa pamoja kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa kudumu.