Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limethibitisha kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Lissu, likieleza kuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi yanayolenga kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza na wanahabari Aprili 10, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, amesema Lissu alikamatwa mnamo Aprili 9 katika mtaa wa Soko Kuu, wilayani Mbinga, na kwamba kwa sasa anaendelea kuhojiwa na maofisa wa polisi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Lissu anatuhumiwa kutoa matamshi ambayo yanaweza kuashiria uvunjifu wa amani na kuyumbisha utaratibu wa kikatiba wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu kama inavyotarajiwa na Watanzania.
Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuepuka kauli au matendo yanayoweza kusababisha taharuki na kuharibu amani, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria.