
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kurejea kwa huduma za usafiri wa treni za SGR hivyo safari zimerejea na kuendelea kama kawaida baada ya awali safari hizo kusimama kufuatia ajali ya treni ya Electric Multiple Unit (EMU) maarufu kama treni ya mchongoko.
TRC limewaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliojitokeza na pia linawashukuru kwa uvumilivu wao na kusisitiza kuwa huduma bora kwa wateja wake ndiyo kipaumbele cha Shirika hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abuubakar Kunenge amesema ajali ya Treni ya Umeme ya SGR (EMU) iliyotokea asubuhi ya Oktoba 23,2025 katika Kituo cha Ruvu Mkoani Pwani imejeruhi Watu 13 ambao hata hivyo hali zao zimeimarika na wameruhusiwa kuendelea na safari.
RC Kunenge amesema tayari safari za Treni ya SGR zimerejea kama kawaida na Abiria wote waliokuwepo kwenye Treni iliyopata ajali wamesafirishwa kuelekea Dodoma.
Kunenge akiwa na Kamati ya usalama ya Mkoa huo, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Profesa Godius Kahyarara pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mhandisi Machibya Shiwa, walifika kwenye eneo la ajali mapema kuwajulia hali Abiria hao pamoja na kuzimamia taratibu nyingine.
