MAWAKALA, KAMPUNI ZA AJIRA ZAPIGWA STOP

Serikali imetoa miezi miwili kwa mawakala binafsi wa huduma za ajira kuacha mara moja kuajiri na kukodisha wafanyakazi, vinginevyo sheria kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa kampuni zinazokodisha wafanyakazi na kusababisha usumbufu kwa wahusika hasa kwa kupata malipo ya chini.

Kamishna wa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira, Saul Kinemela alisema agizo hilo linatekelezwa kuanzia Februari 28 hadi Aprili 28, mwaka huu.

“Wakala binafsi wa huduma za ajira, inajumuisha mtu binafsi, kampuni, taasisi au chombo chochote kinachotoa huduma ya kuunganisha watafuta kazi na waajiriwa bila wakala wa huduma za ajira kuwa sehemu ya mahusiano ya kiajira,” alisema Kinemela.

Aliongeza: “Ukodishaji wa huduma haujapigwa marufuku bali kilichopigwa marufuku ni ukodishaji wa watu.”

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha wizara hiyo, Ridhiwani Wema alisema baada ya Serikali kutoa tamko la uendeshaji wa mawakala hao, Januari 27, mwaka huu, jumla ya kampuni 56 ziliwasilisha maombi ya kuwa mawakala wa kuwaunganisha watu na ajira.

Alisema kampuni au wakala hao wametakiwa kuwasilisha baadhi ya nyaraka ambazo ni katiba ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli, hati ya usajili ya kampuni, leseni ya biashara na namba ya usajili wa malipo.

“Kama watashindwa kuwasilisha vitu hivyo ndani ya miezi miwili tuliyotoa, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad