MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imehairisha kesi namba 37 ya mwaka huu, ya mlalamikaji kuiomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama la wananchi kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo. Anaandika Josephat Isango … Jopo hilo la majaji linaongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo pamoja na Lugano Mwandambo na Aloysius Mjujulizi limeahirisha kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mgombea ubunge Viti Maalum kupitia Chadema, Ammy Kibatala.
Kesi hiyo sasa itasikilizwa kesho saa 3 asubuhi baada ya upande wa serikali kudai kuwa walikuwa hawajamaliza kujibu hoja au kuweka pingamizi sababu walipokea notisi ya walalamikaji muda wa jioni hivyo hawakujiandaa.
“Mheshimiwa Jaji, tunaomba tupewe muda kwani tulipokea nyaraka hizi muda wa kazi ukiwa umekaribia kwisha hivyo hatukujiandaa, tunaomba tupewe muda kama ikiwezekana tulete majibu saa 8:30 Mchana leo kama mahakama itaona inapendeza,” alisema Wakili wa Serikali Obadia Kameya.
Kabla Majaji hawajatolea uamuzi ombi hilo walimshauri Wakili wa mlalamikaji, Peter Kibatala kubadilisha mashtaka na kumshtaki Mkurugenzi wa Uchaguzi kwani ndiye mtendaji mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuangalia katiba Ibara ya 74, kifungu kidogo cha 7, inayosomeka “Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake yaliyoainishwa katika ibara hii, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao, na mtendaji wake mkuu atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge.”
Baada ya marekebisho hayo, kesi hiyo iliyovutia watu wengi iliahirishwa mpaka kesho saa 3
Mawakili upande wa mlalamikaji ni Peter Kibatala na Omary Msemwa, huku upande wa walalamikiwa ambayo ni Mwanasheria Mkuu na Tume ya Uchaguzi ni Obadia Kameya na Alecia Mbuya.
Katika kesi hiyo, mgombea huyo ambaye pia ni mpiga kura mwenye maslahi na uchaguzi mkuu ujao, ameomba mahakama kwa mujibu wa kifungu hicho sura ya 343 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ifafanue kuhusu haki za wapiga kura.
Mlalamikaji anaitaka mahakama iseme na kutafsiri kifungu hicho kinamaanisha nini kuhusu haki hiyo kufuatia kauli iliyotolewa na NEC pamoja na Rais Jakaya Kikwete kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Aidha, anaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa Rais na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuzuia wananchi kukaa kwa utulivu umbali huo ama la.
MWANAHALISI ONLINE
Kilichojiri Mahakamani Muda Huu Kesi ya Wapiga Kura Kukaa Mita 200
October 20, 2015
Tags