Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha pamoja na viongozi wengine wa Chadema Wilaya ya Mpanda, wamekamatwa na polisi leo , kwa kile kinachodaiwa kufanya kampeni katika kambi ya wakimbizi ya Katumba, wilayani Mpanda bila kuwa na kibali maalum.
Masha ambaye alikihama chama cha CCM hivi karibuni na kujiunga na Chadema amezungumza nasi na kusema ameshikiliwa katika kituo cha polisi cha Mpanda baada ya kufanya kampeni katika kambi hiyo.
“Nilikwenda kufanya kampeni katika kambi hiyo ambayo ina wakimbizi ambao mimi mwenyewe niliwapa uraia mwaka 2009,” amesema Masha na kuongeza:
“Kampeni zinafanyika kule lakini kwa sababu wanazojua wao wametukamata wakati hao wanaoitwa wakimbizi niliwapa uraia kwa amri ya Rais.”
Pamoja na Masha wengine waliokamatwa ni Mgombea ubunge jimbo la Nsimbo, Gerald Kitabu, Abraham Mapunda, Mwenyekiti wa Chadema, Mpanda. Katibu wa Chadema jimbo la Nsimbo, Stanslaus Selemani, Dalas Damian, Lameck Constantine Momose na Francisco Sylvester .
Kwa mujibu wa Masha, polisi wamewachukua maelezo viongozi hao wa Chadema kuanzia saa 9 mchana na wamemaliza saa 10 jioni.
“Tulikamatwa kuanzia saa 7:15 mchana tukachukuliwa chini ya ulinzi mkali wa polisi toka Katumba hadi Mpanda mjini na kuanza kuhojiwa,” amesema.
Akizungumza na mtandao huu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP Dhahiri Kidavashari amesema Masha amekamatwa leo saa 4 asubuhi akiwa na watu wengine sita kwa makosa ya kufanya mkutano bila kibali katika makazi ya wakimbizi.
Kamanda Kidavashari amesema viongozi hao wa Chadema walitumia uwanja wa kambi ya wakimbizi ya Kanoge na baadaye Katumba bila kuwa na kibali maalum baada ya kuona kuwa hakuna ratiba ya mkutano mwingine katika eneo hilo.
“Kufanya mkutano si tatizo, tatizo walifanya hivyo bila kibali, yale ni makazi ya wakimbizi wengine wamepewa uraia lakini wengine hawajapewa,” amesema.
Masha akamatwa na polisi kwa kufanya kampeni kambi ya wakimbizi
October 21, 2015