SUALA la mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi, Mohamed Dewji (Mo), kukabidhiwa Simba limefikia patamu baada ya viongozi wa matawi kuutaka uongozi kupeleka mapendekezo ya mchakato huo baraza la wadhamini la klabu hiyo haraka ili mpango huo ukamilike.
Mo alishaweka wazi kuwa anataka kuweka hisa ya asilimia 51 na kilichobaki ni mchakato wa kubadili katiba ili zoezi hilo likamilike kwa muda mwafaka.
Kutokana na umuhimu wa mabadiliko hayo, hivi karibuni uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi ulikutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuangalia namna ya kumaliza jambo hilo haraka iwezekanavyo.
Rais wa Simba, Evans Aveva, juzi alikutana na viongozi wa matawi wa Dar es Salaam, ambapo suala kubwa walilolizungumza ni namna ya kuwafunga Yanga Februari 25, mwaka huu lakini suala la Mo nalo likajitokeza, ambapo viongozi hao wakitaka kujua kinachoendelea.
Licha ya wajumbe waliokaa katika kikao hicho hawakutaka kuweka wazi mambo waliyoyajadili, lakini kuhusu suala hilo la Mo, viongozi hao wa matawi walimbana Aveva na mwisho wakakubaliana kuwa uongozi upeleke mapendekezo ya mchakato katika baraza la wazee ili wakae na wanasheria wao kujadili suala hilo waone kama litakuwa na faida kwa klabu.
“Hakuna anayekataa mabadiliko, lakini lazima Wanasimba wote kwa kauli moja tukubaliane, hatutaki mtu anung’unike ndiyo maana tumeshauriana na uongozi wakutane na baraza la wazee ili jambo hili tulimalize vema,” alisema mmoja wa waliohudhuria kikao hicho.