Chama cha Wananchi (CUF) kimedai kuna mipango inayofanyika ya kumvua ukatibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa sababu anaonekana kama kikwazo cha utulivu Zanzibar.
Katika taarifa iliyotolewa na chama hicho jana, ilidai kuna kikao cha chini chini ambacho kimeandaliwa na baadhi ya wajumbe wa upande mmoja wa CUF, kikiwa na lengo hilo huku upande wa pili ikipinga kikao hicho ambacho hakitambuliki kikatiba.
“Kwa mujibu wa katiba ya CUF Ibara ya 84 (1) ikisomwa pamoja na ibara ya 93 (1)(d) inaeleza kuwa; ...kutakuwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo itakutana mara moja kwa kila miezi miwili,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Mbarara Maharagande ilieleza mara ya mwisho kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji ya Taifa kilifanyika Februari 2, 2017 katika ofisi ndogo ya chama Vuga, Mjini Unguja.