WAKATI straika wa KRC Genk, Mbwana Samatta akifunga bao moja kati ya 3-0 dhidi ya Oostende, pia alitupia mawili ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi Stvv, lakini kuna jambo aliambiwa na baba yake ambaye alienda Ubelgiji kumpa sapoti.
Baba wa staa huyo anayejulikana kwa jina la Ally Pazi Samatta, aliliambia Mwanaspoti baada ya kurejea nchini kwamba kila wakati humwambia mwanawe anapopewa nafasi ya kucheza ajue kocha kuna kitu cha kiufundi kakiona kwake.
“Nimekaa Ubelgiji mwezi mzima. Kwa hiyo mechi alizofunga nilikwepo uwanjani, jambo kubwa ninalomwambia kila ninapoongea naye kila nafasi anayopata ya kupangwa kwenye timu aichukulie kama hataipata tena na uzuri amejifunza mambo mengi kutokana na sehemu mbalimbali alizopita.
“Mojawapo ya mechi alizofunga nilimwambia kapambane kwa ajili ya timu pia kunipa furaha ya kuwepo uwanjani. Mbwana sio muongeaji sana akacheka, akasema mzee nitahakikisha natimiza haja ya moyo wako na akafanya hivyo kweli. Nilimwambia vile kumpa moyo, kwani kila siku nawafurahia watoto wangu,” alisema.
Alisema kuna wakati wachezaji wanachoka, lakini haimanishi viwango vyao vimeisha, hivyo anaona ni jukumu lake kuhakikisha kijana wake anapambana hadi dakika ya mwisho.
“Ndio maana namwambia kwamba nguvu yake kubwa anapaswa kuionyesha uwanjani bila kujali mashabiki wanamjaji kitu gani kwa nyakati tofauti. Ninachokipenda kwake amekomaa sana kimtazamo na amekuwa akinionyesha zaidi ya kile ninachomshauri,” alisema.
Mbwana ambaye alikuwa akikumbana na changamoto ya namba kwenye kikosi hicho kabla ya kuondoka kwa Paul Onuachu katika dirisha dogo la mwezi Januari, mwaka huu na kwa sasa ndiye mshambuliaji wa kutegemewa kwenye kikosi hicho.