Harmonize Atupa Vijembe Kwa Diamond Platnumz
Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize mnamo Jumamosi jioni alionekana kutupa vijembe kwa aliyekuwa bosi wake katika WCB, Diamond Platnumz kuhusu wizi wa kofia yake.
Siku chache zilizopita, kofia ya kijani ya Diamond iliibiwa alipokuwa akipita katikati ya mashabiki wake mjini Dodoma, Tanzania na ikabidi atume walinzi wake kumfuata aliyeichukua.
Jumamosi, Konde Boy naye pia alitangamana na mashabiki wake katika mji wa Kahama, Tanzania na alikuwa na kofia yake kwa muda wote bila mtu yeyote kujaribu kuiiba.
Katika kile kilichoonekana kama shambulio kwa Diamond Platnumz kutokana na wizi wa kofia yake hivi karibuni, bosi huyo wa Kondegang alisema, "Hakuna mtu anayeweza kuiba kofia yako wakati wanakupenda kweli."
Kwa kauli yake hiyo, Konde Boy alionekana kupendekeza kuwa anapendwa zaidi na mashabiki , tofauti na aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.
Mapema mwezi huu, msako mkali wa kumtafuta shabiki aliyenyakua kofia ya msanii Diamond Platnumz ulianzishwa baada ya mwimbaji huyo kuagiza hatua ichukuliwe.
Diamond kwenye video zilizosambaa mitandaoni alikuwa akiongozwa nawalinzi wake katikati ya umati wa mashabiki wakati kofia yake ya kijani kibichi ya besiboli iliponyakuliwa kutoka kichwani mwake.
Bosi huyo wa WCB alikuwa ameinama chini huku akijaribu kukwepa kundi la watu na dakika chache baadaye, kofia ile ilitoweka na akaangalia huku na kule kwa mshangao.'
Katika video iliyosambazwa mtandaoni, mtu angeweza kuona mkono wa mwanamume akichukua kofia kwa nyuma huku akimshika mwimbaji huyo kwa mkono mwingine.
Mkanganyiko uliotokana na tukio hilo ulienea. Kisha aliongozwa hadi kwenye gari lake ambako alilalamika vikali kuhusu kuibiwa kwa kofia yake.
Kisha akamwamuru mlinzi wake mmoja, Onesmo amtafute mwizi huyo na kumrudishia mali yake ya thamani.
"Onesmus hakikisha kwamba kofia inapatikana. Ina nguo nyingi zinazolingana," Diamond alidai.
Katika video nyingine, mwanamume mmoja aliibuka kukabidhi kofia kwa mwimbaji huyo huku akieleza jinsi ilivyokuwa kazi rahisi kumpata mwizi huyo.
Diamond alikuwa akitembelea duka la Airtel mjini Dodoma kabla ya kuelekea kwenye tafrija. Kofia ya kijani inatoka kwa timu ya mpira wa vikapu ya Boston Celtics ya Marekani.
Mashabiki walimkejeli staa huyo wa bongo fleva kwa kujishughulisha sana na kofia. Kulikuwa na picha zake zikisambazwa mtandaoni huku wanamtandao wadadisi wakiuliza ni gharama gani kwa mwimbaji huyo kuumizwa kiasi cha shabiki kuiba.