Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Bawacha), limesema iwapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson hatochukua hatua ya kuwaondoa Halima Mdee na wenzake 18 bungeni, watawahamasisha wanawake nchini nzima kupinga Katiba kuendelea kukanyagwa.
Pia, Bawacha limesema litahamasisha wanawake kupinga matumizi mabaya ya kodi za watanzania kuendelea kutumika kuwalipa watu wasio na sifa ya kuwa wabunge kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na Kaimu Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Sharifa Suleiman amesema wanatarajia kuona majibu ya Spika kwa kuchukua hatua mara kikao cha Bunge kitakapoanza kesho tarehe 30 Januari mwaka huu.
Amesema wanalaani vikali kitendo cha Spika Tulia kufumba macho na kushindwa kuwaondoa wanawake 19 bungeni wasio na chama cha siasa kinyume na katiba ya nchi.
“Mahakama Kuu katika hukumu yake ya tarehe 14 Desemba mwaka 2023 ilithibitisha kuwa maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema ya tarehe 27 Novemba 2020 ya kuwafukuza uanachama wanawake 19 yalikua halali.
“Kufuatia hukumu hiyo wanawake hao 19 wamewasilisha notisi yenye lengo la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu (japo kusudio la kukata rufaa haliwezi kuzuia utekelezaji wa hukumu).
“Pamoja na hukumu kutolewa na walalamikaji kuwasilisha notisi lakini Spika hadi sasa hajachukua hatua yoyote ya kuwaondoa Bungeni badala yake ameendelea kuwakumbatia kinyume na katiba ya nchi na hii inadhihirisha kuwa mhimili wa Bunge unashindwa kuheshimu maamuzi ya mhimili va Mahakama,” alisema.