Akizungumza jijini, Dar es Salaam jana, Ummy alitolea ufafanuzi kuhusu ugonjwa huo na kuongeza ndani ya wiki moja, kumekuwa na ongezeko la wagonjwa 11 na kufanya jumla ya wagonjwa kufikia 32, ingawa idadi ya vifo haijaongezeka.
Alisema majibu kuhusu ugonjwa huo yanatokana na uchunguzi wa awali uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) na kwamba serikali imechukua nafaka kadhaa zinazopatikana mkoani Dodoma ili kuzipeleka Atlanta, Marekani kwa uchunguzi zaidi.
“Tulitoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo Juni 19 mwaka huu ambao ulipatikana wilaya za Chemba na Kondoa, kulikokuwa na wagonjwa 21 na vifo saba, hata hivyo mpaka kufikia juzi wagonjwa waliokumbwa na ugonjwa huo wameongezeka na kufikia 32 na idadi ya vifo imebakia saba,” alisema Ummy.
Alisema katika jitihada za kutambua kiini cha ugonjwa huo, Wizara imepeleka jopo la wataalamu huko Dodoma ili waweze kushirikiana na wenzao walioko huko kufanya uchunguzi wa kina wa ugonjwa huo.
Alisema sampuli mbalimbali za damu, haja ndogo, haja kubwa, vinyama vya ini na sampuli za vyakula, zilipelekwa katika maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali, maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na maabara ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Vile vile sampuli nyingine kesho zitapelekwa Marekani katika maabara ya Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC) kilichopo Atlanta kwa uchunguzi zaidi,” alisema Ummy.
Aidha alisema, “kuna uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa huu umesababishwa na ulaji wa chakula kilichokuwa na sumukuvu na kuleta madhara, ili kuwa na uhakika na jambo hilo Wizara yangu inasubiri matokeo ya vipimo vya damu na haja ndogo vilivyopelekwa katika Maabara ya CDC matarajio yetu ni kupata majibu hayo katika kipindi kisichozidi wiki moja.”
Alisema tangu ugonjwa huo ulipoibuka, wagonjwa 12 wametibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na 18 wametibiwa Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.