UDAKU SPECIAL

Latest Post

Msigwa: Chama cha Mapinduzi Kimechoka Polisi Acheni Kukisaidia
Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mchungaji Peter Msigwa amefunguka na kulitaka jeshi la polisi nchini kutokisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema wamuache yeye na CHADEMA wapambane kukiondoa chama hicho madarakani kwani kimeshachoka

Msigwa amesema kitendo cha polisi juzi kumkamata wakati akiwa kwenye majukumu yake ya kibunge kimemuudhi sana na kusema ni jukumu la Mbunge yoyote yule kuelimisha jamii, kuwapa habari wananchi pamoja na kuikosoa serikali.
"Mimi nilikuwa sifanyi uchochezi kazi ya Mbunge kuelimisha, kuhabarisha, kuikosoa, kuisimamia serikali na kuchochea maendeleo katika jimbo kwa hiyo kama Mbunge ninayo haki ya kuzungumzia Demokrasia na haki ya kuzungumzia mambo ya utawala bora, nina haki ya kuzungumzia haki za binadamu , kitendo cha polisi kunikamata juzi kimeniudhi sana hao polisi waniache mimi na chama changu tupambane na CCM, wasiisadie CCM kwani saizi imechoka ipo dhohofu yaani ipo taabani wanajaribu kuitetea CCM, wajitokeze CCM wenyewe wajibu hoja" alisema Msigwa
Msigwa aliendelea kusema kuwa yeye ni Mbunge ana haki ya kuikosoa serikali iliyopo madarakani hata kuichonganisha na wananchi ili wasiichangue tena mwaka 2020 anadai huo ndiyo wajibu wake kisiasa na ndiyo maana anakuwa mpinzani.

Mywether Aonyeshaya Jeuri ya Pesa Anunua Mjengo wa Bilioni 56
KWA watu wengi, kumiliki majumba Las Vegas na Miami ingetosha kuwafanya waone wameshamaliza kazi, lakini Floyd Mayweather yupo tofauti na wengi.

Bondia huyo Mmarekani ambaye hajawahi kupigwa katika pambano lolote kati ya mapambano yake 50 aliyocheza, anaendelea ku­furahia maisha ya kustaafu baada ya kumchapa Muiri­shi, Conor McGregor jijini Las Vegas.

Baada ya kumchapa McGregor katika raundi ya 10, inadaiwa Mayweather aliweka kibindoni zaidi ya pauni milioni 250 (Sh bil­ioni 752).

Bondia huyo ambaye amekuwa hajivungi ka­tika matumizi ya fedha na kufurahia jasho lake, amemwaga kitita cha pau­ni milioni 18.9 (zaidi ya Sh bilioni 56) kununua jumba kubwa la kifahari, katika eneo la watu wazito la Beverly Hills.

Kumbuka kuwa, Mayweather, 40, ana jumba jingine jijini Las Vegas, pia analo jingine Miami ambalo lina thamani ya pauni milioni 5.69 (zaidi ya Sh bilioni 17).

Jumba hili jipya alilonunua, lina vyumba sita vya kulala na mabafu kumi. Pia lina chumba maalu­mu cha sinema ambacho wanaweza kukaa watu 50 kwa raha kabisa, likiwa na mbwembwe nyingi zikiwemo mvinyo, bisi, chocolate na pipi.

Mayweather amecheza ngumi kwa miaka 21 na alistaafu Agosti 26 akiwa ameingiza fedha nyingi zaidi ya bondia yeyote yule kihistoria

Mmarekani huyo anadai kuwa yeye ndiye bondia wa kwanza kuingiza zaidi ya dola bilioni moja (zaidi ya Sh trilioni 2) katika mchezo huo mgumu zaidi.

Ukiachana na mkwanja aliotumia katika ku­nunua jumba hilo, inasemekana pia kuwa May­weather ametumia kiasi cha pauni 369,000 (zaidi ya Sh bilioni moja) kwa ajili ya kununua vitu vya ndani.


Afisa Wa Serikali Ajinyonga Hadi Kufa
Afisa mmoja wa serikali katika jimbo la Nandi nchini Kenya, Kevin Kamboi amejinyonga hadi kufa kwa kile kilichoelezwa kuhusishwa na tuhuma za uhujumu uchumi na rushwa nchini humo.

Kamboi ambaye alikuwa anafanya kazi katika Idara ya Afya kama Afisa Ugavi, aliacha ujumbe akieleza kuwa amepata msongo wa mawazo baada ya kutolewa amri na Gavana wa jimbo hilo, kuchunguzwa iwapo amehusika na vitendo vya uhujumu uchumi, huku akiwataja maafisa wenzake ndiyo waliostahili kubeba msalaba huo.
Kamanda wa Polisi wa jimbo la Nandi nchini Kenya, Peter Wambani amesema marehemu alimuomba mke wake akamuandalie kikombe cha chai huku akiendelea kutazama mpira sebuleni, lakini aliporudi hakumkuta mumewe na baada ya kumtafuta alikuta mwili wake ukining'inia kwenye mti karibu na banda la ng'ombe.
Tukio hilo limetokea huku baadhi ya maafisa wengine wa idara hiyo wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi, kutokana na kupotea kwa fedha za serikali.

Mfalme Mswati Ameoa Mke wa Miaka 19 Na Kuwa Mke wa 14
MFALME Mswati wa Tatu wa Swaziland kwa mara nyingine ameongeza idadi ya wanawake kwa kuoa mwanamke mwingine. Katika kuadhimisha Ngoma ya Umhlanga ambayo hufanyika kila mwaka kwa kumpa mfalme fursa ya kuchagua mwanamke wa kuoa, mfalme huyo hivi karibuni alimchagua Siphele Mashwama mwenye umri wa miaka 19 kuwa mkewe wa 14.


Msichana huyo ambaye ni binti wa waziri Jabulile Mashwama katika serikali ya nchi hiyo, alipewa manyoya maalum mekundu ya ndege anayejulikana kama emagwalagwala ambaye huhusishwa na sherehe hiyo maalum ya kifalme. Mswati ambaye ana umri wa miaka 49 huchagua wanawake waliovuka umri wa miaka 19.

Pamoja na talaka kupigwa marufuku katika nchi hiyo ya kifalme, Mfalme Mswati amewahi kuwataliki wake zake watatu. Siphele ambaye ni mhitimu wa Waterford Kamhlaba World University College, alifuatana na Mfalme Mswati alipohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni.
Habari hiyo ilifichuliwa na msimamizi wa sherehe za kifalme, Hlangabeza Mdluli, aliyethibitisha kwamba Mswati alikuwa amefuatana na mkewe huyo ambaye kwa umri ndiye mdogo zaidi.

Wake wengine wa Mswati.
Wake zake wengine ni pamoja na: Inkhosikati LaMatsebula, Inkhosikati LaMotsa, Inkhosikati LaMbikiza, Inkhosikati LaNgangaza, Inkosikati LaMagwaza (ameachika), Inkhosikati LaHoala (ameachika), Inkhosikati LaMasango, Inkhosikati LaGija (ameachika).

Wakiwa kwenye sherehe za mwaka.
Wengine ni: Inkhosikati Magongo, Inkhosikati LaMahlangu, Inkhosikati LaNtentesa, Inkhosikati LaNkambule, Inkhosikati Ladube na Inkhosikati LaFogiyane. Mfalme King Mswati, anayejulikana pia kama Ngwenyama, yaani simba, anasemekana kuwa na watoto zaidi ya 13 ambao ni pamoja na binti yake mkubwa zaidi aitwaye Sikhanyiso, Sibahle Dlamini, Makhosothando Dlamini, Majaha Dlamini, na Tiyandza Dlamini.

Mswati akikagua gwaride.
Wengine ni Sakhizwe Dlamini, Saziwangaye Dlamini, Bandzile Dlamini, Lindaninkosi Dlamini, Mcwasho Dlamini, Temtsimba Dlamini na Temaswati Dlamini, among others. Baba yake Mswati, Mfalme Sobhuza wa Pili, alioa wanawake 70. Mswati amekuwa akishutumiwa kwa kujilimbikizia utajiri wakati watu wake wengi ni maskini.
Hivi karibuni, nchi hiyo ndogo ilitumia kiasi cha Dola milioni 2.2 (sawa na Sh. bilioni 5) kwa kununua magari ya anasa aina ya BMW 740i na pikipiki 80. Magari hayo yalikuwa ni kwa ajili ya viongozi wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrikca (SADC) waliyoyatumia kwa ajili ya mkutano wa siku mbili.

Ukomo wa Umri wa Rais Pasua Kichwa Uganda
Kikundi cha wafuasi kindakindaki wa chama tawala cha NRM wakiwemo baadhi ya wenyeviti wa majimbo wameelezea pendekezo la kufuta Ibara ya 102 (b) ya Katiba ili kuondoa ukomo wa umri wa rais ni jaribio la kupindua sheria mama.

Wafuasi hao wanasema wazo la kuondoa ukomo wa umri wa mgombea urais linachochewa na uroho

Katika taarifa yao iliyosomwa jana na Dennis Sekabira, ambaye ni mwenyekiti wa Jimbo la Nakaseke Kusini, kikundi hicho kiliwaambia waandishi wa habari kwamba wanapinga msimamo wa wabunge wa chama hicho kwa sababu mradi wao huo hauna maslahi kwa amani ya nchi.

“Huu ni mwelekeo hatari na unahatarisha amani tuliyoifaidi nchini,” alisema Sekabira ambaye ameeleza kwamba kikundi hicho kina wajumbe 121 wa Halmashauri Kuu ya Taifa, chombo cha pili kwa ukubwa katika uongozi wa chama.

Mwenyekiti huyo alisema wajumbe hao hawaungi mkono juhudi za kuzuia maoni ya wengi dhidi ya kusudio la kuondoa ibara hiyo na kwamba inahitajika amani wakati wa kukabidhi madaraka.

“Tumeamua tusiinyime haki nchi yetu nafasi pekee ya kubadilisha mamlaka kwa amani,” alisema. “Badala ya kuhutubia suala la ukomo wa umri, wabunge wa NRM wanapaswa kujikita katika utekelezaji wa Ilani ya chama.”

Mwaka 2015 Waganda walibadili katiba kuondoa ukomo wa mihula kumwezesha Rais Yoweri Museveni kugombea muhula wa tatu na kuendelea na sasa ukiondolewa ukomo wa umri wa miaka 75, rais huyo mwenye umri wa miaka 73 sasa atakuwa huru kugombea tena mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77.

Hapatatokea Upelelezi  Kutoka Nje Uhalifu Unaofanywa Nchini Utapelelezwa na Vyombo Vyetu- Mwigulu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba amewataka wananchi nchini kuendelea kuwa na imani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini katika kulinda Raia na mali zao

Waziri Mwigulu akizungumza kuhusu watu wanaotaka wapelelezi kutoka nje na hatua wanazochukua juu ya watu wasiojulikana.

Waziri Mwigulu amesema kuwa kama yeye ndiye aliyepewa dhamana ya usalama wa Raia na mali zao katika wizara ya mambo ya ndani basi hapatatokea hata kakitongoji kamoja au kauchochoro ambacho kitaonekana kimeshindikana ndani ya nchi yetu, Ameyasema hayo akizungumza na wananchi wa kata ya Kinampanda wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Aidha Waziri Mwigulu amesema kuwa hata watu wanaoshambulia watu watashughulika nao mmoja mmoja hasa waliobeba jina la watu wasiojulikana, kwahiyo wananchi waendelee kuliaamini jeshi la polisi nchini wakati huu ambapo wanaendelea na kazi ya upelelezi wa kuwakamata watu wote waliohusika na mashambulio kwa Mbunge Tundu Lissu, Afisa mstaafu wa jeshi la wananchi na hakimu huko Mtwara kwani uchunguzi huo auna ukomo mpaka upate wote katika idadi yao waliohusika na mashambulizi.

Waziri mwigulu ameongeza kuwa nchi hii ni nchi huru inajitegemea na kuna watu wanasema wanataka vyombo vya nje vifanye uchunguzi, hawa watu wanao fanya uhalifu nchini, upelelezi utafanywa na watu wetu, watakamatwa na vyombo vyetu na watafikishwa katika vyombo vya sheria vya hapahapa  tunatakiwa kuamini vyombo vyetu, kama serikali tutashugulikano kwelikweli na si kama hatujaanza nao tunashughulika nao.

Watu Wawili Wauwawa katika Nyumba ya Kulala Wageni
UTATA umeibuka baada ya miili ya watu wawili waliouawa na watu wasiojulikana kukutwa katika nyumba ya kulala wageni mjini Tanga ikiwa haina nguo na imefungwa kamba za miguu na mikononi.

Katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedicto Wakulyamba miili ya watu wawili, wote wanaume, iligunduliwa jana majira ya saa mbili asubuhi na mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Bomai Inn iliyopo Kata ya Majengo jijini hapa.

Kamanda Wakulyamba aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa mhudumu wa nyumba hiyo ambaye hakumtaja kwa jina, alibaini kuwapo kwa miili hiyo alipotaka kufanya usafi ndani ya chumba hicho.

"Majira ya saa mbili asubuhi wakati mhudumu alipoingia ndani ya chumba hicho namba 303 kwa ajili ya kufanya usafi, alikutana na miili ya watu hao wawili wote ni wanaume ikiwa imelala chini, imefungwa kamba miguuni na mikononi," alisema.

Kamanda huyo alisema miili hiyo ni ya watu wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40 ambao hawakutambulika mara moja.

Alisema kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu za kitabu cha wageni cha nyumba hiyo ya kulala wageni, mtu anayeitwa Rashid Omari alijiandikisha kutumia chumba hicho siku hiyo.

Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Omari ni Msafa kwa kabila, mkazi wa Dar es Salaam na ni mfanyabiashara.

Kamanda Wakulyamba alisema miili hiyo haikuwa na jeraha lolote zaidi ya michubuko ya kawaida na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini sababu za mauaji hayo na waliohusika kuyatekeleza ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Vifo vya watu hao vimezua utata kutokana na waliouawa kutofahamika kwa wakazi wa eneo hilo, mazingira ya vifo vyao kuashiria mauaji, wauaji kutojulikana pamoja na kitendo cha uongozi wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuruhusu wanaume wawili walale chumba kimoja, kinyume cha taratibu za uendeshaji wa biashara hiyo.

"Watu wawili tena wanaume kuuawa ndani ya chumba kimoja na kusiwe na hata mtu aliyesikia kurupushani za mauaji hayo... inatia hofu kubwa na inawezekana kuna mpango maalum wa wauaji hao," alisema Asha Ramadhan, mmoja wa walioshuhudia tukio hilo la utoaji miili hiyo.

Hamza Issa, mkazi mwingine wa maeneo hayo, alisema huenda mauaji hayo yalipangwa na aliyelipia kutumia chumba hicho kabla ya kukutwa miili ya watu wawili.

Mkazi mwingine wa maeneo hayo, Anthon Aloys, alisema huenda maiti hizo ziliingizwa ndani ya chumba na mkodishaji chumba hicho baada ya watu hao kuuawa eneo jingine.

WATU WATATU
Matukio ya wanaume zaidi ya mmoja kuuawa wakiwa katika chumba kimoja cha nyumba za wageni yalififia kwa muda lakini si uhalifu ambao ni mgeni.

Machi 21, mwaka jana watu watatu walikutwa wakiwa wameuawa kwa kunyongwa katika nyumba ya kulala wageni ya Mexico, mjini Kyela mkoani Mbeya, ikiwa na majeraha ya kuunguzwa kwa moto.

Mganga mfawidhi wa Hosptali wa Wilaya ya Kyela, Dk. Francis Mhagama alikaririwa akisema maiti hizo za watu watatu zilikuwa zimenyongwa pamoja na majeraha ya moto.

Kwa mujibu wa kitabu cha wageni cha nyumba hiyo, majina ya watu hao yalikuwa Hassan Ally, Mariam Hassan na Adam.

Aidha, Agosti mosi, mwaka jana pia watu wawili walikutwa wamefariki katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam huku miili yao ikiwa imeungua moto.

Watu hao waliofariki walikuwa wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi walipokuja jijini walifikia hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.

Mtandao wa Whatsap Wafungiwa
Mtandao wa WhatsApp umeingia kifungoni nchini China ukiifuatia na Instagram, Twitter, Facebook, Gmail, Snapchat na Pinterest.

WhatsApp imeanza kufungiwa taratibu katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kwa mujibu wa taasisi inayoratibu masuala ya mitandao duniani, Open Observatory of Network Interference (OONI).

Mtandao wa Shirika la Utangazaji CNN unaripoti kuwa katika miezi ya hivi karibuni WhatsApp imekuwa ikipatikana kwa shida.

Mtandao huo ulianza kufungiwa taratibu wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa chama tawala cha Communist, utakaoanza Oktoba 19 mwaka huu.

Kwa kawaida nchi hiyo hudhibiti matumizi ya mtandao katika kipindi cha uchaguzi mkuu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

China inatumia mtindo wa Great Firewall katika kudhibiti matumizi ya intaneti ambayo hujumisha sera na teknolojia.

Serikali Kufanya Ukarabati Hospitali Aliyolazwa Tundu Lissu
Serikali imeahidi kupeleka Sh 500 milioni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa lengo kulifanyia ukarabati jengo la upasuaji ambalo pia lilitumika kumhudumia Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu baada ya kupigwa risasi nyumbani kwake Area D mjini.

Lissu alipigwa risasi Septemba 7 mwaka huu na kupelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya huduma ya utengemavu kabla ya kupelekwa Nairobi nchini Kenya ambapo hadi sasa anaendelea matibabu.

Akizungumza wakati alipoitembelea hospitali hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo amesema kuwa ukarabati huo unalenga katika kukarabati miundombinu ili kuendana na mahitaji ya mji wa Dodoma kwa sasa.

“Hatuwezi kuvumilia hili tunataka tulete fedha tuikarabati ili iendane na hali halisi ya mahitaji ukizingatia sasa hivi Dodoma ni mji mkuu.

Tunataka viongozi na wananchi waweze kutibiwa katika hali nzuri na ya kisasa zaidi ya hapa,”amesema.

Hatua hiyo ilifuatia Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Caroline Damian jengo hilo limekuwa likitumika kufanya upasuaji kwa wastani wa watu 500 kwa wiki.

“Kwa siku tumekuwa tukifanya upasuaji kwa watu kati ya 15 na 20, ili kukidhi mahitaji imebidi kubalisha vyumba vingine ambavyo havikuwa vya upasuaji kuwa vya upasuaji,”amesema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kiologwe amesema kwamba awali wakati jengo hilo linajengwa kuna aina ya upasuaji ambazo zilikuwa hazifanyiki mkoani hapa lakini sasa zinafanyika.

“Zamani kuna aina ya upasuaji ulikuwa haufanyiki lakini sasa unafanyika. Tuna madaktari wazuri wanaojituma lakini changamoto ipo katika miundombinu,”amesema.

Kuhusu ujenzi wa jengo la wakinamama  na watoto, Jafo amesema ameridhika na kazi inayoendelea bali amemtaka mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika Oktoba 20 ili lianze kutumika.

“Nimewapa maelekezo wahakikishe kuwa jengo hilo linakuwa na mfumo wa gesi ya oksijeni ili kuepuka wahudumu ama wauguzi kukimbizana na mitungi mara kunapokuwa na mahitaji ya kuokoa maisha ya mama na mtoto,”amesema.

Meneja Msaidizi wa Mradi huo, Mhandisi Frank Mabubu amesema jengo hilo limekamilika kwa asilimia 85 na kwamba ujenzi utakamilika Oktoba 20.

Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Lawataka Wananchi Kuchukua Tahadhari ya Ugonjwa Huo
Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha) limesema licha ya takwimu kuonyesha kwamba maambukizi ya VVU yanapungua nchini bado wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari.

Takwimu za Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) zinaonyesha maambukizi yalipungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2012.

Akizungumza leo, Mratibu wa Kanda ya Dar es Salaam wa Nacopha, Edna Edson amesema  wananchi wasibweteke na kupungua kwa maambukizi bali wachukue hatua kukabiliana na virusi.

Amewaeleza waratibu wanaopata mafunzo ya kusimamia ruzuku ya mradi wa Sauti yetu unaoendeshwa na baraza hilo kwamba elimu kwa wananchi ndiyo suluhisho katika kukabiliana na maambukizi mapya.

Amesema  mradi huo utatekelezwa kwenye halmashauri 46 nchini huku ukilenga kuelimisha jamii ili ione sababu za kutafuta ushauri na upimaji wa virusi vya Ukimwi.

“Mradi huu pia unalenga kuelimisha jamii ya watu wanaoishi na VVU ili kuongeza upatikanaji wa huduma na kuhakikisha wanaendelea kupata tiba,” amesema  na kulishukuru Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kwa kufadhili mradi huo.

Baadhi ya halmashauri utakakotekelezwa mradi huo ni pamoja na Temeke, Kilombero, Lindi, Korogwe Morogoro na Masasi.

Kwa upande wake, Daisy Majamba aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema kama hatua hazichukuliwi Ukimwi unaweza kuleta athari katika jamii na uchumi wa nchi kwa ujumla.

“Mradi huu na elimu itakayotolewa itamfanya kila mmoja wetu kupata uelewa na hivyo kujikinga na maambukizi,” amesema.

Ametaka uongozi wa baraza hilo kutekeleza mradi huo na kuhakikisha kwamba unawafikia walengwa ili jamii nzima ya watanzania iweze kunufaika.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nacopha, Deogratius Rutatwa aliwataka waratibu hao kuzingatia mafunzo ili ruzuku zitakazotolewa kwa ajili ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.

Jeshi la Polisi Kufanya Uchunguzi wa Maiti Zinazookotwa Baharini
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na askari wa majini wanaendelea na uchunguzi dhidi ya matukio ya mauaji yanayoendelea kutokea katika baadhi ya maeneno na kisha miili kutupwa kwen

Kamanda Mambosasa ametoa taarifa hiyo leo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, na kusema kwamba matukio hayo yanaonekana kudhamiriwa na watu wanaofanya hivyo kwani miili yote inakutwa imefungwa kamba.

"Jeshi la polisi tunaendelea na ufuatiiaji tukishirikiana na askari wa majini kwa sababu matukio haya yanatokea huko, kama kanda tunaendelea tena kwa uchunguzi wa hali ya juu, na hawa wauaji wanakuwa wanadhamiria kabisa kufanya hivyo. Ni vifo vya mashaka kwa kweli na yote inakutwa imefungwa hii inamaanisha huyo mtu anadhamiria", amesema Kamanda Mambosasa.

Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kuzungumzia miili mingine ambayo iliokotwa katika fukwe za pwani ya Msasani, na kusema kwamba miili ile haikujulikana ni kina nani na hakukuwa na mtu alikwenda kuripoti kupotelewa na ndugu yake, hivyo waliikabidhi Manispaa kuizika.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio mfululizo ya watu kuuawa na kutupwa baharini, na kisha miili yao kuokotwa ikiwa imefungwa kwenye viroba, ambapo jana miili mitatu imeokotwa huku mwili mmoja ukiwa umefungwa jiwe shingoni.