Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema mwili wake bado una risasi moja licha ya kutolewa nyingine 15, huku akiweka bayana kuwa kitu anachokikosa zaidi ni kazi yake ya ubunge.
Mwanasheria mkuu huyo wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari mara baada ya kufika nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, pia aligusia faraja aliyoipata baada ya kutembelewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Lissu aliyelazwa Hospitali ya Nairobi tangu Septemba 7 na ambaye huenda akahamishiwa nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi, ametoa kauli hiyo wakati akihojiwa na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Azam, Baruan Muhuza.
“Hali yangu ya afya inaendelea vizuri bado nipo hospitali maana yake bado ni mgonjwa lakini niwaeleze Watanzania na wananchi wote wanaofuatilia afya yangu kwamba naendelea vizuri sana,” alisema na kuongeza,
“Hivi tunavyozungumza sina jeraha la risasi, risasi 16 ziliingia mwili mwangu na saba zilitolewa na madaktari hapahapa (Nairobi) na moja ipo bado kwenye mwili wangu lakini sina majeraha ya risasi na hali ni nzuri kuliko nilivyoletwa, nililetwa vipandevipande.”
Hiyo ina maanisha kwamba risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya shambulio hilo alipofikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General).
Huku akionyesha mkono wake wa kulia alisema, “Nilipigwa risasi hapa, upande huu na ikatokea hapa. Madaktari wanasema kwamba ilichakaza kabisa mfupa ilikopita, hakukuwa na mfupa. Ilibidi waungeunge kwa hiyo kuna chuma kinachounganisha mfupa wa huko mbele na nyuma kwenye mkono huu.”
Pia, aliukunja na kuunyoosha mkono wake wa kushoto na kusema kuwa hawezi kuunyoosha sawasawa kwa sababu kwenye kiwiko alipigwa risasi iliyosambaratisha mfupa.
Alikumbuka Bunge
Lissu ni miongoni mwa wabunge wanaoibua hoja nyingi na kuibana Serikali bungeni, jambo ambalo aliliweka bayana katika mahojiano hayo na kusisitiza kuwa ndicho kitu anachokikosa zaidi.
“Mimi napenda kazi ya ubunge. Kuna watu wanapenda ubunge kwa sababu una pesa na manufaa, unaitwa mheshimiwa na unakuwa wa kwanza kwenye foleni, hukai katika foleni. Mimi napenda ubunge, mle ndani (ukumbi wa Bunge) yale mapambano ya kisiasa na kiitikadi, unamkaba waziri mpaka anakosa pa kukimbilia,” alisema.
Aprili 4, 2015 Lissu alitoa hoja 22 za kupinga vifungu vya Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 na kusababisha kikao cha 14 cha Bunge kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6:15 usiku.
Mvutano wa kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na mawaziri ulianza saa 12:30 hadi saa 5:30 usiku na baadaye Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.
Katika mahojiano hayo na Azam Lissu alisisitiza, “Hakuna kazi ninaimisi kama ya ubunge bungeni, niende ofisini kwangu nijiandae nikasome ili kesho nikizungumza Watanzania wasikie, ndio kazi ninayoipenda.”
Alisema kitendo cha kulazimika kukaa miezi mitatu hospitalini, kulala kitandani muda wote kinamfanya akose mapambano ya bungeni, “Mtu akisema hii ni kutafuta kiki nafikiri aidha hanifahamu au akili zake haziko sawa.”
Kuhusu viongozi waliomtembelea alisema, “Makamu wa Rais alikuja wakati wa kumuapisha Rais Uhuru Kenyatta na kabla ya hajaondoka alitafuta nafasi ya kuja kuniona hospitali. Nilifurahi sana kwa uungwana. Ukiwa mgonjwa hakuna kitu cha faraja kama kupata mtu wa kukujilia hali. Aliniambia kwamba ametumwa na Rais John Magufuli kuja kunitazama, nikamjibu kamwambie Rais namshukuru sana kwa kukutuma kuja kuniona.”
Wanaohama upinzani
Kiongozi huo pia aligusia hamahama ya wanasiasa na kubainisha kuwa wapo wengi walioondoka lakini Chadema bado imebaki imara.
“Watu kwa sababu mbalimbali, aidha hawajui, wanasahau au wanajisahaulisha na historia yetu ya zama za vyama vingi,” alisema.
Alibainisha kuwa mbunge wa kwanza kuhama Chadema alikuwa Dk Aman Walid Kabourou ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa chama hicho, baadaye makamu mwenyekiti na mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya chama hicho.
“Aliondoka lakini aliishia wapi? Alihamia CCM kwani Chadema ilikufa? Said Arfi, alikuwa makamu mwenyekiti wa Chadema na mbunge wa Mpanda Mjini alirudi CCM je, Chadema ilikufa? Dk Willbroad Slaa alikuwa mbunge kwa vipindi vitatu mfululizo aliondoka je, Chadema ilikufa,” alihoji.
Chanzo: Mwananchi
Tundu anasema.
ReplyDeleteAlisema kitendo cha kulazimika kukaa miezi mitatu hospitalini, kulala kitandani muda wote kinamfanya akose mapambano ya bungeni, “Mtu akisema hii ni kutafuta kiki nafikiri aidha hanifahamu au akili zake haziko sawa.”
Tundu inaashiria Madawa yana mkosesha laha na Amani.
Ugua Pole .... Dua na sala zetu juu yako.
Lini Utarudi Muhimbili.