Salma Kikwete Aonya Wasioandikisha Watoto

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Salma Kikwete Aonya Wasioandikisha Watoto
MKE wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Salma Kikwete, ameshauri serikali kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao hawawaandikishi watoto wao wanapozaliwa kupata vyeti kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Mama Salma alitoa ombi hilo mwishoni mwa wiki, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu barani Afrika, ambayo kitaifa yalifanyika katika Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama, Kibiti mkoani Pwani.

Sherehe hizo zilizoadhimishwa kwa mara ya kwanza barani Afrika, ziliambatana na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa wanafunzi 200 wa shule hiyo, vilivyotolewa na Wakala wa Usajili na Udhamini (Rita).

Salma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), alisema kutomsajili mtoto ni kumnyima haki ya msingi na kuinyima serikali taarifa muhimu za maendeleo, na kwamba wazazi ambao watoto wao hawakupata huduma hiyo wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo.

“Kama hawatawapeleka watoto wao kusajiliwa nafikiri ni vyema kuchukua hatua kali zinazostahili ili kumsaidia mtoto asije akapata matatizo baadaye, kwa kuwa utambulisho wa mtoto ni haki yao na hawastahili kunyimwa kwa kuwa hahitaji kulipia zaidi ya mzazi au mlezi kumpeleka mtoto kituo cha kuandikisha,” alisema Salma.



Alisema mzazi anaweza kumsajili mtoto na kupata vyeti katika ofisi za watendaji kata na vituo vya tiba, ambavyo ni rahisi kwa wananchi kufika, na kuwataka watu kuitikia wito na watoto wao kupata vyeti.

“Huduma imepelekwa kwenye maeneo wanayoishi halafu ni ya bure, hakuna sababu ya mzazi kushindwa kumwandikisha mtoto wake na akifanya hivyo anamnyima haki ya msingi,” alisema.

Mama Salma ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema kuwa matumani ni kuwa Watanzania wote watapata huduma ya kusajiliwa kwenye matukio muhimu ya maisha yake, na hivyo kuwa na matukio halisi kwa kadri ya mpango kazi.



Alisema changamoto kubwa ni wananchi kufikia huduma ya usajili kwa kuwa hutembea umbali mrefu kutoka vijijini hadi wilayani na kwamba ndicho kikwazo kikubwa katika usajili wa matukio hayo muhimu.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Rita, Emmy Hudson, alisema usajili wa matukio muhimu ya binadamu husaidia nchi kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Alisema wameamua kutumia maadhimisho ya siku hiyo kutoa vyeti kama njia ya kuhamasisha wananchi umuhimu wa kuwa navyo na kwamba mwendelezo wa juhudi mbalimbali za kuboresha mifumo ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu kwa nchi za Afrika.



Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Rita, Prof. Khamis Dihenga, alisema wameshusha huduma za usajili wa matukio muhimu ya binadamu hadi ngazi ya kata na kwa kupitia mfumo maalum kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa wakati huo huo na kupewa cheti na wameshaifikia mikoa 11.

Alisema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ilibainisha kuwa asilimia 13 ya Watanzania ndiyo wenye vyeti vya kuzaliwa na kwamba kwa kasi ya Rita wamefikia asilimia 25, lengo likiwa kila Mtanzania kusajiliwa.

“Tunataka kila mtoto anayezaliwa kupata cheti kabla ya kutoka hospitalini, tunataka ifike mahali Mkuu wa Wilaya au ofisa yeyote anaweza kuangalia taarifa za watu wake kupitia kanzi data, itasaidia kupanga shughuli za maendeleo na kupeleka huduma kwenye maeneo husika,” alisema.

Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwajuma Mbuguni, alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 337 wa kidato cha kwanza hadi cha sita, ambao wanalipiwa ada kwa asilimia 100 na wahisani mbalimbali ikiwamo taasisi ya Wama na wanatoka maeneo yote ya nchi.

Alisema kati ya wanafunzi hao, 30 pekee ndiyo wanalipiwa ada na wazazi wao na sifa zinazotumika kuwachagua ni walio na wazazi, lakini wanatoka familia duni, mazingira hatarishi na yatima.



Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa shule, maendeleo ya kitaaluma ni mazuri kwa kuwa matokeo ya kidato cha nne kati ya wanafunzi 85, saba walipata daraja la kwanza, 32 daraja la pili, 27 daraja la tatu na 17 daraja la nne huku mmoja akipata sifuri.

Aidha, matokeo ya kidato cha sita wanafunzi 10 walipata daraja la kwanza, 23 daraja la pili, 18 daraja la tatu na kushika nafasi ya 26 kimkoa na kitaifa nafasi ya 117 kati ya shule 543.

Mbuguni alisema kati ya wanafunzi 44 wameendelea na masomo katika vyuo vikuu mbalimbali nchini na saba wataenda kusoma stashahada.
----

Utamu wa audio book ya SIRI YA PADRE NA MKE WANGU hauna mfano, sikiliza Sehemu ya 1 bure, Sehemu ya 2 Tsh 2000 tu

Nusu ya mapato ni kwa ajili ya wagonjwa wasiojiweza, Lipia uburudike huku ukitoa sadaka Safi,ni www.makapedia.com au bofya kitabu hapo chini:



 

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mama Salma mmm mmmm naona picha yako mambo si mabaya ni gym? Au diet? Au vyote?

    ReplyDelete

Top Post Ad