Ticker

6/recent/ticker-posts

Samia ataja hatua za kukabili ugumu maisha 
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuchukua hatua zinazolenga kumlinda mwananchi dhidi ya upandaji wa gharama za maisha uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

rais samia suluhu hassan.
Mkuu wa Nchi huyo alitoa kauli hiyo jana alipohutubia wananchi njiani katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tatu mkoani Mbeya.

Alisema moja ya hatua hizo ni kuweka ruzuku ya Sh. bilioni 100 ambayo kila mwezi serikali inaiweka kwenye mafuta.Rais alisema Tanzania ilikuwa na tatizo la mafuta ya aina mbili, yakiwamo ya kupikia ambayo Waziri wa Kilimo amefanya kazi nzuri na sasa yameshuka bei.

Kuhusu mafuta kwa ajili ya magari na mitambo, Rais Samia alisema ni tatizo la dunia nzima, yanaendelea kupanda bei duniani.

“Hatua tuliyochukua kama serikali ni kutafuta ruzuku ya kushusha bei ya mafuta, tungeachia yapande bei kama yanavyokwenda duniani, leo yasingenunulika. Serikali inatoka Sh. bilioni 100 kila mwezi kutoa ruzuku kwenye mafuta bei zibaki zilipo.


 
“Suala la mafuta mpaka huko duniani waache kupigana, mpaka huko duniani  waanze kushusha bei ndiyo tutapata unafuu, vinginevyo fedha mnazodai za barabara na umeme itabidi tukate tupeleke ruzuku kwenye mafuta kuzuia bei isipande,” alisema.

Rais Samia alisema kwenye mafuta serikali ipo macho na inajua na inajitahidi isipande kwa kiasi kile kinachopanda kwa wengine.

“Ukichukulia bei ya mafuta kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuna nchi ambazo mafuta hayanunuliki lakini marais wote tunajitahidi kila mmoja kwa njia yake kupunguza bei. Bei ya mafuta ni tatizo la ulimwengu mzima, tunajitahidi zibakie pale zilipo,” alifafanua.


MRADI WA MAJI

Akizindua mradi wa maji wa Shongo-Mbalizi ulioko katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani humo, Rais Samia aliwaagiza viongozi wa serikali kushirikiana na wananchi kuwashughulikia watu wote wanaoharibu vyanzo vya maji.

Alisema wananchi ndiyo walinzi wa kwanza wa vyanzo vya maji vilivyoko kwenye maeneo yao.

Mkuu wa Nchi alisema kazi ya serikali ni kuyachukua maji kutoka kwenye chanzo kwenda kuwanufaisha wananchi na hivyo lazima kuwe na ushirikiano baina ya pande hizo mbili kwenye ulinzi wa vyanzo vya maji.

“Mkiona watu wanakwenda kuharibu chanzo cha maji, washughulikieni kwa mujibu wa sheria ndogo ambazo mmejiwekea kwa kushirikiana na halmashauri yenu, maji haya ni kwa faida yenu, serikali kazi yetu ni kuyatengenezea mfumo,” aliagiza.


 
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh. bilioni 3.3, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga, alisema umejengwa na wataalamu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya.

Alisema mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo milioni nne mpaka lita milioni 12 kwa siku, una mtandao wenye urefu wa zaidi ya kilomita 45 na kutoka kwenye chanzo mpaka kwenye tangi ni kilomita 15.

“Kwa sasa wanatumia lita milioni nane pekee kutokana na mahitaji. Hili tangi lina uwezo wa kuchukua lita za maji milioni 1.5 kwa siku na huu mradi unahudumia watu zaidi ya 80,000 wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi,” alisema Sanga.

Alibainisha kuwa mradi huo umeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka chini ya asilimia 50 mpaka kufikia asilimia 95 na Mji wa Mbalizi hauna tena tatizo la maji.


Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza, aliishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo, akirejea hali ya awali kwamba wananchi wa Mji wa Mbalizi walikuwa wanapata shida kupata huduma hiyo.

Rais Samia anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mbeya ambapo leo atakuwa wilayani Chunya kabla ya kutembelea Halmashauri za Mbarali, Rungwe na Kyela.


Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments