Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kupitia East Africa Radio, Nsajigwa Senior amesema kuwa kauli anazozitoa Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi zitakuja kumpa wakati mgumu huko mbele pale ambapo timu yake itashindwa kufanya vizuri.
Ujumbe huo wa Nsajigwa unakuja baada ya Kocha Gamondi kueleza kuwa kwa kikosi alicho nacho hahofii mtu yeyote wala timu yoyote kukutana nao hata kama ni Barcelona au Real Madrid kwani kikosi chake kipo vizuri na wachezaji ni 11 tu uwanjani hata kama ni timu gani.
"Gamondi kauli yake inaweza kuja kumhukumu kwa sababu zifuatazo, (kauli ya kusema kwamba hata wamletee Real Madrid au Barcelona yuko tayari kucheza nao), kwanza ameongea kauli ile public na kwa watu ambao anaongea nao kuna makundi mawili, kuna wale ambao wanaelewa kile ambacho anakisema na kuna wengine ambao wanasikiliza tu lakini uelewa wao ni mdogo kuhusu mpira.
"Nakumbuka miaka ya nyuma kidogo kipindi kile Simba ipo kwenye form, Haji Manara alikuwa na tabia ya kusema hata aje Bayern, aje nani, kwa Simba hii kwa Mkapa hatoki.
"Lakini ikatokea Green Warriors wakamtoa. Kwa hiyo ikitokea hapa ghafla tu Yanga akafungwa na timu yoyote ya kawaida itakuja sasa kubadilika ile kauli, ooh ulituambia nini, aje Barcelona hapa ooh aje Madrid mbona umefungwa na huyu, ile presha wakati mwingine kwa viongozi huwa inapelekea walimu wanafukuzwa," amesema Nsajigwa Senior.