Barabara ya Kulipia Kibaha Mpaka Morogoro mbioni

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa


Dar es Salaam. Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, David Kafulila amesema mchakato wa ujenzi wa barabara ya kulipia kutoka Kibaha hadi Morogoro uko katika hatua za mwisho na kufikia Februari 2024, mkandarasi atapatikana.

Kafulila alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini hapa.

Katika mahojiano hayo, Kafulila alisema tayari kampuni kadhaa zimeonyesha nia ya kujenga barabara hiyo ya kulipia kutoka Kibaha hadi Morogoro yenye urefu wa kilomita 130 kwa lengo la kupunguza msongamano.

Alisema China ni moja ya nchi zilizotoa kampuni nyingi zilizoonyesha nia ya kujenga kipande cha Kibaha kwenda Chalinze, Chalinze kwenda Morogoro na baada kutoka Morogoro kwenda Dodoma.

“Mpango wa Serikali ni kuunganisha haya majiji mawili Dar es Salaam na Dodoma kwa barabara za express way (barabara ya haraka), barabara ambazo ni mbili za kwenda na mbili kurudi.

“Kwa hiyo, kuna kampuni tisa ziliomba kwa ajili ya kipande cha Kibaha – Chalinze chenye urefu wa kilomita 78.9. Kampuni hizo zilifanyiwa mchujo zikabakia tano, kati ya hizo, nne ni za China. Unaweza ukaona namna China inavyoshiriki kwenye ushindani huu wa ubia,” alisema Kafulila.

Alisema Serikali ilianza kwa kukamilisha upembuzi yakinifu kwa kipande cha Kibaha – Chalinze chenye kilomita 78.9 na wakakiingiza sokoni kwa maana ya kutafuta wawekezaji, baadaye walipatikana, uthamini ukafanyika na wakatakiwa wapeleke maandiko yao ya mradi.


“Kwa sababu kazi ile inachukua muda mrefu, waliomba kuongezewa muda hadi Februari 2024. Ilitakiwa Novemba, mwaka huu wawe wamekamilisha lakini wakaongezewa muda hadi Februari, tunategemea kufikia mwezi huo watakuwa wamekamilisha maandiko yao ili waweze kushindanishwa na ipatikane kampuni itakayojenga barabara hiyo sasa,” alisema Kafulila.

Alisema upembuzi yakinifu kwa kipande cha Chalinze – Morogoro chenye urefu wa kilomita 85 umekamilika, nayo imepelekwa sokoni kwa ajili ya kumpata mwekezaji.

Alisisitiza kwamba hiyo haizuii walioomba kwenye kipande cha kwanza kuomba pia kipande cha pili.

“Tunatafuta wawekezaji waje...aje yeye mwenyewe na andiko lake la mradi au ashiriki kwenye ushindani, zote ni taratibu za kisheria ambazo zinatumika kupata wawekezaji ndani ya nchi yetu, lakini ni utaratibu unaotumika duniani kote kupata wabia,” alisema.

Mchakato wa ujenzi wa barabara ya Dar es salaam – Chalinze – Morogoro ulianza tangu mwaka 2017 ambapo taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM kwa mwaka 2015 - 2017 ilieleza kwamba mtaalamu mwelekezi alikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na hatua za kumpata mwekezaji/mbia zilikuwa zinaendelea.

Uwekezaji katika umeme

Akizungumzia uwekezaji kwenye nishati, Kafulila alisema kipaumbele cha Serikali hivi sasa ni kutafuta wawekezaji wa kuzalisha umeme wa jua, upepo na vyanzo vingine ili kuongeza pia uzalishaji wa umeme ambao utakuwa na vyanzo tofauti.

Alisema kwa kufanya hivyo, nchi itaongeza uimara wa gridi badala ya gridi kutegemea chanzo kimoja.

Kamishna huyo alisema kampuni ya Uingereza ya Mazda, imeonyesha nia ya kuwekeza kwenye mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 210 ambao una thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 300 milioni.


“Ni utaratibu ambao mwekezaji atatumia gharama zake kujenga na kwenye hesabu zile ndiyo zitaamua atalipwa kiasi gani kulingana na gharama zile ukilinganisha na bei atakayopaswa kulipwa,” alibainisha kamishna huyo.

Alisema wameita pia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye miradi ya viwanja vya ndege, kwa ajili ya kujenga hoteli, kama ilivyo kwenye mataifa makubwa kama ya Ufaransa ambako ubia unafanyika kwenye viwanja vya ndege.

Kwa upande wa bandari, alisema Bandari ya Dar es Salaam iliingia ubia na kampuni ya DP World na sasa taratibu za utekelezaji zinaendelea. Alisisitiza kwamba ubia huo hauzuii ubia kwenye bandari zingine hapa nchini.

“Lengo ni kuhakikisha tunanufaika na sekta hii ya uchukuzi na kuifanya Tanzania inufaike na nafasi yake ya kijiografia. Kwa hiyo, kijiografia tunahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye bandari, viwanja vya ndege, barabara na reli ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchukuzi katika ukanda wa Afrika Mashariki.”

Alisema hamu ya wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta hizo, imetokana na mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika pamoja na utashi wa kisheria ambao Rais Samia Suluhu Hassan anaouonyesha kwamba nchi hii iko tayari kwa biashara.

“Ubia msingi wake ni kuharakisha maendeleo ya binadamu. Serikali haiwezi kuharakisha maendeleo kwa kutumia mikopo na kodi pekee,” alisema Kafulila wakati wa mahojiano hayo na Mwananchi.

_________

LOVE STORY YA UTANIKUMBUKA NEYLA Ipo tayari ni maandishi na Sauti !, Kuisoma yote Bonyeza HAPA Lipia tsh 1000 Tu mtandao wowote,au Tembelea www.makapedia.com

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad