Nauli SGR zawaibua wamiliki wa mabasi, wachumi

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa

 

Nauli SGR zawaibua wamiliki wa mabasi, wachumi

Baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kutangaza nauli ambazo zitatumika katika treni ya kisasa (SGR), wamiliki wa mabasi, wachumi na wananchi wametoa mitazamo yao na namna inavyoweza kurahisisha huduma.


Pia, wachumi wameeleza kuwa kuanza kwa treni hiyo kutaongeza ushindani na kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na kurahisisha usafirishaji abiria na mizigo.


Hayo yamesemwa baada ya Latra kutangaza bei mpya za treni hiyo ambapo kwa daraja ya kawaida, mtu mmoja atalipia Sh31,000 hadi Dodoma huku mtoto wa kuanzia miaka 12 akilipia nusu ya bei zote zilizopangwa kulingana na umbali wa kituo husika.


Tangazo hilo la bei lilitolewa Juni 10, 2024 ikiwa ni siku chache kabla ya treni hiyo kuanza kufanya kazi Julai mwaka huu kama ambavyo ilikuwa imeagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan.


Mbali na Dodoma, Latra imezitaja bei hizo ambapo anayekwenda Pugu atalipa Sh1,000, Soga Sh4,000, Ruvu Sh5,000, Ngerengere Sh9,000, Morogoro Sh13,000, Mkata Sh16,000, Kilosa Sh18,000, Kidete Sh22,000, Gulwe Sh25,000, Igandu Sh27,000, Dodoma Sh31,000, Bahi Sh35,000 na Makutupora Sh37,000.


Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), John Priscus amesema nauli zilizotajwa ni shindani lakini ubora wa huduma ndiyo utakaomfanya mwananchi kuchagua aina ya usafiri anaotaka kutumia.


“Haiwezi kutuondoa sisi bado kuna vitu mteja anavihitaji, kila mtu ana njia yake, sehemu anayoshukia mtu, urahisi wa upatikanaji wa huduma husika hivyo si rahisi kuua biashara yetu,” amesema Priscus.


Ametolea mfano wa uwepo wa baadhi ya nchi ambazo zina mtandao wa reli karibu kila eneo na lakini bado kuna mabasi yanayotoa huduma kwa wananchi wake kutokana na treni kushindwa kufika sehemu hizo.


Kuhusu vituo vya kushukia abira alilolisema Priscus huenda ikawa ni shida kwa wale wanaoshukia katika vituo ambavyo treni hiyo haisimami jambo ambalo linaweza kuwafanya kutafuta usafiri mwingine kwa ajili ya kurudi baada ya kushukia mbele au kuhitaji usafiri kwenda mbele zaidi.


Wachumi wazungumza


Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi alisema kuanza kwa treni hiyo kutaongeza ushindani katika huduma za usafirishaji hasa katika kipindi hiki ambacho abiria wanaongezeka kila siku.


“Pia, ukiangalia barabara zetu zina msongamano hivyo itakuwa tofauti na treni lakini uwepo wake hauwazuii watoa huduma wengine,” amesema Dk Olomi.


Amesema wamiliki wa mabasi bado watakuwa na chaguo la kuendelea kutoa huduma wakati wakiangalia hali ya soko na kwa sababu wanatumia barabara wanao uwezo wa kuhamisha uelekeo wa mabasi yao ili wasijiendeshe kwa hasara.


“Sidhani kama Serikali italeta ushindani usiokuwa wa haki, hiki ni kitu kilichokiwa katika mpango kwa muda mrefu, wamiliki wa mabasi walikuwa wanajua na baadhi waliendelea kununua mabasi, badala yake ni kitu kitakacholeta unafuu kwa uchumi,” amesema Dk Olomi.


Amefafanua kauli hiyo kwa nadharia kuwa moja ya kichocheo cha uchumi ni kuwezesha wengi kusafiri kwa wakati mmoja kwa urahisi.


Jambo hilo mara zote huakisiwa katika namna ambayo watu huweza kutumia muda ambao wangeupoteza barabarani katika safari zao kuuhamishia katika shughuli za kujiingizia kipato.


“Na hii inaweza kupunguza watumiaji wa ndege hasa safari za kwenda Dodoma wakahamia katika treni maana kupata ndege ya Dodoma ni kazi,” amesema.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja amesema mara zote katika shughuli za usafirishaji kila mtu kuna aina ya usafiri na ndivyo itakavyokua kwa watu waliokuwa wakikosa usafiri wa treni ambao wanaupenda kupata walichohitaji.


“Kwa wananchi ni jambo zuri na kutakuwa na ushindani katika utoaji wa huduma bora, faida kunwa inayoonekana ni ongezeko la huduma za usafirishaji kwa abiria na mizigo,” amesema Profesa Semboja.


Alisema suala hilo litakwenda kuchochea ukuaji wa uchumu kwani gharama zitapungua katika baadhi ya maeneo.


“Lakini tukumbuke tu, SGR siyo ya Dodoma, lengo lake ni kuinganisha Tanzania na nchi za jirani hivyo ni jambo zuri,” amesema.


Wananchi wazungumza


Wakati wachumi wakiyasema hayo, Zubeda Msangi alilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kusimamia kikamilifu ratiba watakaokuwa wanazipanga ili kuepuka kukosa wate.


“Kuna saa za watu wa Afrika, saa 2:00 asubuhi unaambiwa ndiyo mnaondoka mnaondoka saa 3 asubuhi, au mnaambiwa saa 11 asubuhi mnaondoka saa 1 asubuhi hii huwa inakera ndiyo maana watu huwa wanaangalia wapi kuna unafuu unaoendana na ratiba zao walizopanga,” amesema Zubeda.


Daud Maganga yeye amesema usafiri huo ni rahisi kwa watu wanaoshukia katika vituo vikubwa na siyo wa barabarani.


Kwa mujibu wa taarifa ya Latra, nauli zilizotangazwa zimepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi kwa kuzingatia umbali kwa kilomita ikiwa ni kutimiza maombi yaliyopelekwa TRC.


_________

LOVE STORY YA UTANIKUMBUKA NEYLA Ipo tayari ni maandishi na Sauti !, Kuisoma yote Bonyeza HAPA Lipia tsh 1000 Tu mtandao wowote,au Tembelea www.makapedia.com

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad