Mwabukusi Mwamba Sana Auweka Njia Panda Uchaguzi TLS

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa
Mwabukusi Mwamba Sana Auweka Njia Panda Uchaguzi TLS
 Mwabukusi

 Mwabukusi Mwamba Sana Auweka Njia Panda Uchaguzi TLS

Sakata la uchaguzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) limeendelea kuchukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Steven Kitale kufungua shauri la mapitio ya kimahakama dhidi ya TLS.


Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, jana Jumatano, Julai 10, 2024, Kitale amesema katika shauri hilo namba 16018/2024, lililofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, mbele ya Jaji Athuman Matuma, ameiomba Mahakama impe ruhusa kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama pamoja na amri ya muda ili kuzuia mkutano mkuu wa mwaka (AGM) 2024.


Mkutano huo unatarajiwa kufanyika mwezi ujao jijini Dodoma.


Ametaja hoja nyingine katika maombi yake ni kuweka zuio la mchakato wa uchaguzi, kupinga uamuzi wa kamati ya rufaa ya uchaguzi kumuengua wakili Boniface Mwabukusi kuwania urais wa TLS na kusimamisha uchaguzi huo hadi uamuzi wa maombi hayo utakapofanywa.


“Shauri hili linalenga kuonyesha umuhimu wa uwazi na ufuataji wa sheria katika mchakato wa uchaguzi, lengo ni kuhakikisha kila mmoja wetu anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Hakuna anayepaswa kuwa juu ya sheria,” amesema Kitale.


Kitale amebainisha mbali na kuenguliwa kwa Mwabukusi, hoja nyingine zitakazojadiliwa katika shauri hilo ni pamoja na kupandishwa kwa ada ya usajili wa washiriki wa mkutano mkuu wa TLS kutoka Sh118,767 na Sh100,000 kwa washiriki wa mtandaoni hadi Sh200,000, uamuzi ambao amedai haukupitishwa na baraza la uongozi la chama hicho.


"Nimeamua kufungua kesi hii baada ya kuona kuna ukosefu wa uwazi hasa kwenye masuala ya uchaguzi na mkutano mkuu wa mwaka. Tuliona ni muhimu kudai haki ya kupata nyaraka muhimu zinazotakiwa kisheria ili kila mwanachama aweze kushiriki kikamilifu na kwa haki," amesema Kitale.


Kwa mujibu wa Kitale, uamuzi wa viongozi wa TLS na kamati ya rufaa ya uchaguzi kutofuata taratibu unaweza kuleta madhara sio tu katika uendeshaji wa shughuli za chama, pia kutaathiri imani ya wanachama kwa uongozi wa chama hicho.


"Nimeomba Mahakama itoe amri ya kutupa nyaraka zinazohitajika na pia kusitisha shughuli zinazoendelea hadi haki itakapotendeka. Tunahitaji kuwa kitu kimoja na kushirikiana kuhakikisha chama chetu kinajiendesha kwa mujibu wa sheria na kanuni zetu," amesema.


Kitale amesema tayari wajibu maombi ambao ni TLS TLS, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wameshapelekewa wito na wanatakiwa kuwasilisha kiapo kinzani Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza. Shauri hilo litasikilizwa Julai 15, 2024 mbele ya Jaji Athuman Matuma.


Amesema barua ya kumuomba Mkurugenzi Mtendaji wa TLS kuthibitisha uhalali wa Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ilitiwa saini na watu wanne, akiwemo yeye mwenyewe, Irene Mwakyusa (Mjumbe wa Baraza la Uongozi Kanda ya Kusini), John J.R Nyange (Mjumbe Baraza la Uongozi Kanda ya Mzizima), na Edward Heche Suguta (Mwenyekiti wa Mawakili Vijana - AYL).


"Katika barua yake, Mkurugenzi Mtendaji alijibu kwamba hana mamlaka hayo badala yake mamlaka hayo anayo Rais wa TLS, kitu ambacho siyo sahihi.

Kutokana na hivyo, tunaona haki itapatikana mahakamani, naamini kesi hii italeta mabadiliko chaya ndani ya TLS na kurejesha imani kwa wanachama wetu. Tayari mawakili zaidi ya 100 wamekubali kuungana kusimamia shauri langu," amesema Kitale.

_________

LOVE STORY YA UTANIKUMBUKA NEYLA Ipo tayari ni maandishi na Sauti !, Kuisoma yote Bonyeza HAPA Lipia tsh 1000 Tu mtandao wowote,au Tembelea www.makapedia.com

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad