Ticker

6/recent/ticker-posts

Siri Nzito Sana Nyuma Saluni za Kiume za Kisasa
Dar es Salaam. Ni yapi unayajua kuhusu saluni za kiume maarufu ‘Barbershop,’ ambazo mbali na kuwanyoa nywele kichwani wateja, pia huwasinga sehemu mbalimbali za mwili (massage).

Mwandishi wa habari hii amefuatatilia huduma hiyo kwa siku kadhaa katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Awali, akizungumza na Gazeti la Mwananchi kuhusu yanayotendeka ndani ya saluni za kisasa, Israel Joachim anasema, “niliwahi kwenda saluni, lengo halikuwa kunyoa nywele, bali nifanyiwe ‘massage,’ kweli nilifanyiwa tena na msichana, haikuwa rahisi kuvumilia, kuna maeneo hatarishi nilikuwa nashikwa na huyo dada akaniambia kama hali ni mbaya nijiongeze.”

Anasema baada ya kuingia kwenye saluni hizo kupata huduma, alichokutana nacho, hakimtoki kichwani kwa kuwa mbali na kulainisha misuli na kupunguza uchovu, vyumba vilivyomo saluni vina ushetani mwingi.


“Nilijiuliza nijiongeze na nini, kumbe alitaka (mtoa huduma mwanamke) nimpatie Sh30,000 anisaidie kuondoa hali niliyokuwa nayo, sikuwa na ujanja, nilitekeleza takwa lake sababu sikuwa na la kufanya kutokana na hali yangu,” anasema Joachim.

Hata hivyo, Mwananchi imebaini baadhi ya vyumba hivyo ni kichaka kipya cha biashara ya ngono na inaelezwa asilimia 80 hadi 90 ya wanaume wanaokwenda huko hufuata huduma hiyo ya ngono, ingawa huzuga kwa kuanza kwanza na huduma ya ‘massage.

“Wanaanza na huduma ya kwanza kwa sababu ile ya pili hawana uhakika kama inatolewa pale, kwa baadhi ya watu niliowauliza kwa nini wanakwenda kule wanasema wale wanawake wanaotoa huduma hizo wana uwezo mkubwa wa kuwaandaa wanaume kushiriki ngono,” alisema Ramadhani Masenga, mtaalamu wa saikolojia kutoka Mental Health Hygiene Institute ya Dar es Salaam.


Safari kuelekea saluni yaanza

Ni Jumatano saa 9:30 asubuhi natoka nyumbani Tabata huku nimevalia suruali nyeusi, shati la mikono mifupi na viatu vya wazi, safari yangu ni kutafuta huduma ya saluni za kiume ili mbali na kunyoa nipatiwe huduma ya ‘massage.’

Nilidodosa huku na kule na haikunichukua muda mrefu nilimpata kijana ambaye kiumri sichelei kusema ni rika langu (31), nilijitambulisha kwake naye aliniambia jina lake ni Stalin Mshubira.

Nilimueleza hitaji langu la kutafuta eneo la kufanyiwa ‘massage’ na kunyolewa hapo hapo, huku akionyesha kuwa na uelewa wa mambo yanayotendeka ndani ya saluni hizo.

Alitabasamu na kuniambia napaswa kuwa makini huko ninapokwenda kwa kuwa sitaweza kutoka salama.


Nilionyesha ujasiri na kumwambia anielekeze nia yangu ni kunyoa na kufanyiwa ‘massage’ na si vinginevyo, alicheka tena na kunielekeza nitafute magari yanayokwenda Mwenge niombe nishushwe Sinza na hapo nitakuwa nimefika.

Kwa kuwa mimi si mwenyeji sana Dar es Salaam, jiji lenye raha na karaha, nilichukua bodaboda iliyonifikisha hadi yalipo magari ya Mwenge na nilipanda na kuanza safari yangu huku nikimuomba kondakta anishushe Sinza na baada ya muda nilifika eneo husika.

Ni kama eneo hilo ni maalumu kwa ajili ya kunyoa, zipo saluni nyingi ambazo ni rahisi kuzitambua kutokana na maandishi makubwa yaliyoandikwa ‘Barbershop’, majengo yakiwa kando kando ya barabara.

Bodaboda atafuta chimbo

Nilijifanya sijaona chochote na hapo nilimtafuta dereva bodaboda ambaye nilisikia akiitwa kijiweni kwake kwa jina moja la Ally, nilimuomba anielekeze saluni ambayo ningefanyiwa ‘massage’, kunyolewa na huduma nyingine.


Dereva wa bodoboda aliniuliza ni aina gani ya ‘massage’ nahitaji, kwa kuwa sikuwa na uelewa na mambo hayo, nilimjibu ya mwili mzima na kunyoa nywele kichwani, alitabasamu kama ilivyokuwa kwa Stalin, kijana wa kwanza kunielekeza nitakapopata huduma hiyo.

Nilitamani Ally anifahamishe kuhusu huduma zinazotolewa saluni za kiume, na nilipomuuliza kuhusu hili alisema kama ninahitaji ‘massage’ ya viwango (ya kulala na mwanamke) kwa wakati huo, nimpatie Sh2,000 anipeleke.

“Hata mimi naendaga ila sio kila siku, ukifika wanakuja wanawake watano wanasimama mbele yako unaambiwa umchague atakayekufanyia ‘massage’ na hapo kama unafanya ‘half body massage’ anaweza kukuambia Sh30,000, kwa kuwa utahitaji na huduma nyingine mwambie una Sh20,000 (punguzo) ili na yeye umpatie Sh20,000 (jumla Sh40,000) kwa ajili ya kulala naye maana sio poa huko,’’ alisema Ally.

Nilitoa Sh2,000 mfukoni na kumkabidhi Ally kisha akaanza kunipeleka katika chimbo lake la mara kwa mara huku nikiendelea kumdodosa mambo yanayomfanya kupenda ‘massage.’

Alinieleza ni urahisi kuwapata wanawake anaowasifia kufahamu namna ya kucheza na maumbile ya mwanamume.


Eneo ‘limejificha’

Ni mwendo wa dakika 10 kutoka kituoni hadi kufika eneo hilo ambalo kijiografia limejificha. Ally alinionyesha nyumba niliyohisi kuna familia inaishi humo kwa kuwa hakukuwa na bango lenye kuonyesha uwepo wa shughuli ya ‘massage’ ndani.

Japo nilisimama kwa mbali nilisikia sauti ikinikaribisha ndani, nilipofika mlangoni alitoka dada aliyenikaribisha na kunichukua kunipeleka wanakotoa huduma hiyo, huku kukiwa na wanawake wengine wanne waliovalia mavazi yenye kuusisimua ubongo wa mwanamume ambaye hakuzoea mazingira hayo.

Mshangao wa ghafla ulinipumbaza macho yangu huku nikiulizwa na dada aliyenipokea nimchague mtu wa kwenda naye na aina ya ‘massage’ niitakayo.

“Hapa huduma zetu ni kuanzia Sh20,000 ambayo utafanyiwa mgongo peke yake, Sh50,000 utafanyiwa mwili mzima,’’ anasema dada huyo.

Nilishtuka kwa kuwa si rahisi kwangu kuruhusu kupapaswa mwili mzima na mtu ambaye si mke wangu, nilitupa macho yangu kwa wanawake waliokaa kwenye viti kila mmoja akionekana kuwa na vazi lenye kuonyesha maungo.

Mmoja wa wanawake wale alinikonyeza akimaanisha nimchague, nilimfuata na kuongea naye kwa sauti ya chini kama atakubali kulala na mimi baada ya ‘massage.’

“Hilo tu usijali, ila utapaswa kuongeza Sh30,000,” alisema dada yule.

Nilimkubalia nikamuomba nikanyoe kwanza ndipo nirejee, aliniomba namba zangu lakini nilimuondoa wasiwasi awe na amani kwa kuwa ningerejea na kumchukua yeye.

Mguu kwa mguu hadi saluni

Baada ya kutoka katika nyumba ‘iliyojificha’ inayotoa huduma ya ‘massage’ nililazimika kutafuta usafiri kwenda saluni za kiume, nilitembea kwa miguu na baada ya dakika tano niliiona saluni kando mwa barabara, kwa kuwa nilikuwa upande mwingine nilivuka barabara.

Nilipoingia ndani nilimkuta mzee mmoja ambaye ni sawa na baba yangu tayari amekwisha kupata huduma na alikuwa akijiandaa kutoka, kushoto kwangu walikaa wanawake wawili, mmoja mweupe mrefu mwenye umbo jembamba na mwingine mweusi mnene.

Kuna kijana wa kiume ndani ya saluni hiyo, alitoa ishara kwa wanawake wale wanisikilize na aliamka mmoja mweupe na kunikaribisha, bila kusita nilimueleza nahitaji ‘massage.’

Alifungua chumba kingine cha ndani huku bado baba yule akiwa amekaa akiniangalia usoni, nilitii sauti ya dada yule aliyeniambia niingie ndani ya chumba kile.

Ndani ya chumba

Nikiwa nawaza ni mara yangu ya kwanza kusikia na kwenda kufanyiwa ‘massage,’ sauti ya kijana (Stalin) aliyenionya nitakapokwenda kufanyiwa huduma hiyo niwe makini, ilinijia kichwani.

Nilijisemea, “mwanakulitafuta mwanakulipata,” mbele yangu ndani ya chumba kile kulikuwa na kitanda kirefu kisichowezesha mtu kulala na kugeuka mara mbili. Mbali na uwepo wa kitanda hicho kulikuwa na chumba kingine kwa ajili ya kuoga.

Dada yule aliingia ndani ya chumba kile na kufunga mlango tukabaki wawili na kunitaka nivue nguo zote na maongezi yetu mimi (mwandishi) na dada muhudumu wa saluni yalikuwa hivi.

Dada: Hee! Mbona hukuvua nguo?

Mwandishi: Kwani napaswa kuvua nguo zote si shati tu, maana nilisema nusu ‘massage.’

Dada: (anacheka) Kwani ni mara yako ya ngapi kufanyiwa ‘massage’ saluni.

Mwandishi: Ni mara ya kwanza.

Hata hivyo, nilivua shati huku maongezi yetu yakiendelea, alinielekeza nilale kwa tumbo, hatua niliyoifanya na baada ya muda akiwa na mafuta ya nazi mkononi alianza zoezi lake hilo.

Kupitia maswali yangu nilianza kumdodosa kufahamu kazi hiyo kama aliisomea.

Dada: Nimeishia kidato cha nne na hii kazi sikuisomea, kazi nilianza mwaka jana, kabla ya kazi hii nilikuwa nauza maduka ya nguo.

Mwandishi: ilikuwaje ukahamia kufanya kazi hii.

Dada: Ni maisha tu nimeamua kubadili mfumo.

Mwandishi: Sasa kwa kazi hii unapewa Sh ngapi?

Dada: Sh5,000 kama kamisheni, ukipata wateja wawili unapata Sh10,000 na kuna wakati mwingine nakosa kabisa ila wastani naweza kupata Sh5,000.

Baada ya muda alibadili mkao wake na mfumo wake aliokuwa akitumia awali kwa ajili ya ‘massage’ hatua iliyobadili hali ya mwili wangu na hapo nilizungumza naye kuhusu hatua ya kupata huduma ya ziada.

Japo alinikatalia akiniambia haiwezekani, baada ya muda aliniuliza kama najishughulisha na kazi gani na nilipomwambia mimi ni daktari, alionyesha furaha na hali ya kukubaliana na ombi langu.

Aliniambia kama sina Sh50,000 basi asingeweza kuniruhusu nifanye chochote kwake, nilimuomba walau apunguze maana hali yangu ilikuwa taabani kwa kuwa, kwa wakati ule ningeweza kumpatia Sh20,000, alikataa na kuniambia kwa hela hiyo labda anichezee maungo yangu tu bila kufanya chochote.

Baada ya muda nilibadili mawazo na kumwambia nitaongeza na ningempatia Sh30,000 kwa ajili ya ‘massage’ malipo ya huduma na Sh30,000 ya nyongeza kwa huduma nyingine.

Alikubali na kuniambia basi kwa kuwa kiasi cha fedha nilizokuwa nazo hazikutosha nitapaswa kutumia kondomu na alivuta mkoba wake na kuitoa huku akinielekeza chumba cha pili ninachoweza kupata ‘fidia ya fedha’ zangu endapo ningezitoa.

Wasiwasi ulinijaa na kumwambia basi nitahitaji bila kutumia kondomu na hapo aliniambia gharama yake sitaweza kuimudu kwa kuwa nimeonyesha ubahili huku nikihitaji vitu vizuri.

Maajabu mengine

Baada ya kuonyesha kuhitaji kuondoka kwa dharura kwa kuwa nimepigiwa simu, aliniambia naweza kumpatia Sh10,000 ili anifanyie ‘massage’ sehemu nyeti, (huku akitamka kiungo hicho).

Aina hiyo ambayo kwangu ni mara yangu ya kwanza kuisikia ilinishtua angewezaje kufanya hiyo, aliniondoa wasiwasi kuwa amezoea kazi hiyo. Aliniambia anaweza kuja nyumbani wakati wowote nitakapomuhitaji kwa ajili ya ‘massage’ lakini kwa kuwa ananifuata nitapaswa kumlipa Sh100,000. Nilimshukuru kwa huduma yake na hapo nilifunga safari kutafuta eneo lingine ambalo ningepata huduma kama hiyo.

Safari yangu mguu kwa mguu nilifika Kinondoni na kuulizia huduma hiyo kwenye moja ya saluni zilizopo eneo hilo na nilikaribishwa na wanawake wawili.

Mmoja kati yao nilimfuata na kumuuliza kama ningepata huduma nyingine kwake japo hakutarajia swali hilo, alinikaribisha na kuniambia mteja ni mfalme.

Basi nilimuomba nikatoe fedha kwa wakala kwa kuwa kiwango nilichokuwa nacho ni kidogo na hapo ndipo nilipopata mwanya wa kutoweka.

Mtaalamu anena kuhusu ‘massage’

Ofisa Mfiziotherapia Mkuu wa Idara ya Utengamao na Tiba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Abdallah Makalla anataja aina mbili za ‘massage’ kuwa zipo za starehe na zile zinazotumika kimatibabu.

Anataja ya kimatibabu kuwa, hufanyika kwa watu wenye changamoto ya misuli, magonjwa mbalimbali, hasa wenye maumivu ya mgongo, wachezaji na wenye mawazo na wenye kukakamaa misuli.

“Massage ya starehe mara nyingi hufanyika kwenye saluni na maeneo mengineyo, sasa kwa jumla fani hii inamuhitaji mtu mwenye elimu ya massage.”

Anasema sio kila mtu anafaa kwa ‘massage’ kwa kuwa ina madhara, huku akizungumzia watu wenye uvimbe kuwa endapo watafanyiwa mzunguko wa damu huongezeka na uvimbe kusambazwa.

Mtu mwenye homa pia, Makalla anasema hapaswi kufanyiwa huduma hiyo pamoja na wenye magonjwa sugu, isipokuwa mtaalamu ataamua kufanya baada ya kugundua aina ya msuli wenye matatizo na akashughulikia nayo.

“Sasa hapo ni kwa mtu anapokwenda hospitali akakutana na Mfiziotherapia atajua ni aina gani ya msuli na kushughulika nayo hata kama ana tatizo sugu,’’ anaeleza Makala.

Kuhusu ‘massage’ za starehe Makalla anasema hizo zinapaswa mtoa huduma kuwa na elimu ya kawaida ya namna ya kufanya na aina ya watu wasiopaswa kufanyiwa akitaja wenye vidonda, magonjwa ya ngozi na mwenye tatizo la muda mrefu.

“Changamoto tuliyonayo tunadhani kila mtu anafaa kufanyiwa ‘massage’ na imefika wakati tunatumia vile vifaa vya kufanyia ‘massage’ ambavyo watu wanaweka majumbani mwao, inaweza kuwa na madhara kama hujui ina tatizo gani,” anaeleza.

‘Massage’ na ngono

Makalla anasema upo uwezekano wa mtu kufanyiwa ‘massage’ na kutoshiriki ngono na anayemfanyia, akibainisha hali ya ngono kwa mtu hutokea kichwani na ni mtazamo wa mtu.

Anaonyesha ilipo changamoto ya ‘massage’ za starehe kuwa, mikono hupita juu ya mwili na kuamsha au kusisimua hisia.

“Ufanyaji wa hivyo huwa haiendi ndani, inashughulika juu ya ngozi, sasa huyu mtu anapata hisia kama sio mwaminifu anafanya ngono na yule anayemfanyia endapo atashindwa kudhibiti hisia zake,” anasema Makalla.

“Hata kwa wanandoa, wanafanyiana na zinawaamsha hisia, ni sehemu ya kuwafanya wawe pamoja, ila kwenye saluni na hizi sehemu ambazo hawana elimu ya ‘massage’ wanasababisha kufanyika kwa ngono ijapokuwa si kwa wote.’’

Mtaalamu wa saikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Ramadhan Masenga anasema ‘massage’ ni tiba ya kumfanya mtu afikirie vizuri na kuweka sawa misuli.

“Kutokana na aina yetu sisi, pengine ingependeza mtu afanyiwe aidha na mke wake au mume wake lakini kutokana na utofauti huo, athari zinakuwepo kwa sababu wanaume wengi wanapoenda kushiriki hizo ‘massage’ kwa wanawake wanatengeneza hisia za kushiriki ngono kwa muda mrefu.

“Sasa wanaposimamisha muda mrefu wale wanaotoa hizo huduma wanamwambia tuende na huduma ya pili kwa sababu huduma ya kwanza ameikamilisha,” anasema Masenga.

Pia, anasema hata eneo ambalo ni maalumu pekee kutoa huduma ya ‘massage’ mwanamume anapaswa kujizuia kwa muda mrefu kupata hisia za kushiriki ngono.

Anasema athari atakayopata mtu anapojizuia, ni kuwa na mawazo ya muda mrefu ya kutaka kushiriki ngono na misuli yake ya uume huchoka kutokana na kutofanya tendo hilo.

“Mhusika hawezi kutoka hapo akafika nyumbani anafikiri vizuri, haiwezekani, kwa sababu kwa wanaume anapojisikia kufanya ngono uwezo wa akili kufanya kazi hushuka,” anaeleza mwanasaikolojia huyo. “Hivyo kuna hatari hata kama huyo mwanamume atatoka bila kushiriki ngono, mwanamke yeyote atakayekutana naye mtaani atamtongoza, si kwa sababu anampenda, ni kwa sababu ana kiu inayomuhitaji kuikata.

“Mwanamume anapokuwa na kiu ya ngono, macho yake yanamuona kila mwanamke anafaa bila kujali umri wake, muonekano au athari yeyote ile,” anasema.

“Hata kama mtu huyo atajizuia kufanya ngono na hana mke, yapo matukio matatu yatatokea ndani ya wiki hiyo, mosi kutafuta mpenzi haraka ili akidhi haja yake, pili anaweza kujichua awe sawa, tatu atakwenda kuota ndoto nyevu nyevu kwa sababu hali yake ya ndani inakwenda kupiga kelele.”

Anasema athari za kisaikolojia hutofautiana baina ya mtu na mtu kutokana na utamaduni, huku akiweka bayana kuwa Afrika imekopa utamaduni huu kwa mataifa ya nje.


Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments