AL-SHABAAB WAIZUNDUA TANZANIA ULINZI WAANZA KUIMARISHWA KILA MAHALI

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

TUKIO la kigaidi lililotokea nchini Kenya katika jengo la biashara la Westgate, limeizindua Tanzania na hivyo wamiliki wa majengo makubwa ya biashara likiwemo Mlimani City jijini Dar es Saalam kuimarsha ulinzi.

Tangu kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kutekelezwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia na kusababisha vifo vya watu 67 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa, nchi za Afrika Mashariki zimeanza kuchukua tahadhari kubwa katika kukabiliana na vitendo hivyo.

Tanzania Daima Jumapili jana lilishuhudia msafara mkubwa wa magari uliokuwa ukiingia katika jengo lenye maduka mbalimbali ya biashara la Mlimani City yakifanyiwa upekuzi wa kina, huku madereva wakitakiwa kuteremka na kuyaacha tupu.

Aidha, baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo waliovalia vifaa maalumu walikuwa wakivipitisha chini ya magari yaliyoingia katika jengo hilo kwa umakini wa hali ya juu tofauti na siku za nyuma ambazo watu waliingia na kutoka bila kukaguliwa.

Mmoja wa kiongozi wa ukaguzi huo ambaye ni raia wa kigeni, alionekana kuwa makini na kuwataka wateja wote walioingia na magari yao ndani ya eneo hilo kuyaweka pembeni ili yafanyiwe upekuzi.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa madereva, Juliaus Janco alisema kuwa ni vyema utaratibu huo ukawekwa katika kila jengo lenye msongamano wa watu ili kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea, hasa katika kipindi hiki cha uwepo wa magaidi.

Alisema kuwa pamoja na baadhi kuonekana kukerwa na utaratibu huo, lakini wanapaswa kuelewa kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hofu iliyojengeka sasa, hasa watu wanapoingia katika majengo kama hayo.

Katika hotuba yake ya juzi, Rais Jakaya Kikwete pia aligusia tukio hilo la kigaidi la Kenya akisema kuwa anafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu wengi nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama.

“Ni hofu ya msingi kwani Agosti 8, 1998, Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha,” alisema.

Alisema kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali.

“Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa,” alisema.

Rais aliongeza kuwa baada ya tukio la Kenya, vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Kwamba pamoja na kujizatiti hawawezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.

“Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.

“Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao,” alisema.

Pia aliwataka waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). Kwamba anajua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.

Kenya yataja watuhumiwa ugaidi

Wakati huohuo, habari kutoka Nairobi, Kenya zinasema kuwa nchi hiyo imetoa majina ya watu wanne ambao inasemekana walifanya shambulio dhidi ya jengo la maduka la Westgate wiki mbili zilizopita.

Watu ambao wote ni wanaume, walionekana kwenye picha za kamera za usalama zilizopatikana Westgate baada ya jengo hilo kushikiliwa na Al-Shabaab kwa siku nne.

Msemaji wa jeshi aliwataja watu hao kuwa ni Abu Baara al-Sudani, Omar Nabhan, Khattab al-Kene na Umayr.

Taarifa zinasema kuwa wawili kati yao wana uhusiano na al-Qaeda na mmoja ana uhusiano na wapiganai wa al-Shabaab ambao walikiri kuhusika na shambulio la Westgate.
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad