Mengi Atolea Ufafanuzi Juu ya Ujumbe wa Uchochezi Unaosambazwa Kwa Njia ya Simu Juu Yake

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA

Hivi karibuni nimeshuhudia kusambazwa kwa taarifa mbalimbali kupitia ujumbe mfupi wa simu (sms) na mitandao ya jamii zikinihusisha na tuhuma mbalimbali.

Napenda kuufahamisha umma kwamba taarifa zote zilizotolewa kupitia njia hizo ni za uongo, chuki, na uzushi. Kilichonisikitisha sana ni kuona kuwa uzushi huo unachochea kuifarakanisha jamii yetu kwa misingi ya ukabila jambo ambalo ni hatari kwa umoja na mshikamano ambao Tanzania tumejitahidi sana kuujenga, na mtu yeyote anayediriki kuleta uchochezi wa kikabila hastahili kuwa kiongozi wa ngazi yoyote katika taifa letu.

Mimi ni miongoni mwa Watanzania walio mstari wa mbele wanaomuunga mkono Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusisitiza kuwa rasilimali za asili zilizopo nchini ni mali ya Watanzania na ni lazima wawe wamiliki wakuu wa rasilimali hizo ikiwa ni pamoja na gesi asilia. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema mwaka 1974 katika andiko lake la “Ujamaa ni imani” ukurasa wa 31, kwamba: “madini au mafuta yalio chini ya ardhi, n.k. vitu hivi ni mirathi ya wananchi wote”.

Katika miaka ya hivi karibuni dhana hii ya Watanzania kuwezeshwa na kumiliki uchumi wa nchi yao imetambuliwa na Serikali na Chama tawala kama ifuatavyo:

Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 inasema kwamba:


Aya ya 1.5 TAFSIRI YA WANANCHI


“Walengwa wa Sera ya Uwezeshaji ni Wananchi. Makampuni ya Wananchi ni yale ambayo yamesajiliwa Tanzania ambayo walengwa wanamiliki asilimia isiyopungua hamsini ya hisa zote za makampuni hayo. Sera ya Uwezeshaji itajumuisha wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi na wafanyabiashara katika sekta mbalimbali na makundi mengine.”



Aya ya 3.1 DIRA

“Uwezeshaji wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ni sehemu ya Dira ya maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025. Kufikia wakati huo, sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania inatarajiwa kumilikiwa na Watanzania wenyewe.


Aya ya 4.1.2 TAMKO LA SERA


“Jitihada za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi nchini ni muhimu ziendane na ukuaji wa uchumi unaojumuisha na kunufaisha Watanzania wengi, kuongeza vipato vyao pamoja na kuinua hali zao za maisha.”

Nayo Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 (National Economic Empowerment Act, 2004) katika utangulizi inasema:

“Economic empowerment is a central means for bringing about economic growth and social justice among our people that is necessary for the promotion of peace, tranquility and social stability that has characterized our society.”

Tafsiri yake ni kama ifuatavyo:

“Uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi ni njia kuu ya kukuza uchumi na kuleta haki miongoni mwa jamii, mambo ambayo ni ya lazima katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano, ambayo ni tunu ya asili ya jamii yetu.”

Chama tawala, CCM katika “Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020” kimetamka kwamba:


Aya ya 84 UWEZESHAJI WA WANANCHI KIUCHUMI


‘’Chama Cha Mapinduzi katika sera zake za msingi kama zilivyoainishwa katika Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini na Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka 2000-2010, kimetamka bayana kwamba, mkakati mkuu wa uwezeshaji wa kiuchumi wa wananchi ni ule unaohakikisha kwamba wananchi wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu ama mmoja mmoja, kwa kupitia vyama vyao huru vya ushirika wa aina mbalimbali au kwa kupitia makampuni ya wananchi ya ubia ambamo maelfu ya wananchi watanunua hisa”



Aya ya 103


“Wakati umefika wa kuweka mazingira bora ya upendeleo kwa Watanzania, kama inavyofanyika katika nyanja za kimataifa kwa mfano katika utoaji wa kandarasi za ujenzi, manunuzi n.k. Kuwapendelea Watanzania katika ajira na biashara nchini ni njia mojawapo ya kuwawezesha kiuchumi.”

Kwa msingi huo nimekuwa nikiishawishi Serikali kutekeleza sera na sheria ya uwezeshaji ili kuwashirikisha Watanzania kikamilifu katika uchumi wa Taifa, na kwa sasa hasa katika uchumi wa gesi asilia, ili kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu.

Jitihada zangu zimekuwa zikipingwa na kiongozi wa moja za Wizara za Serikali na amekuwa akitumia mbinu na visingizio mbalimbali. Naamini kwamba usambazwaji wa uzushi unaofanyika sasa ni mwendelezo wa mbinu hizo chafu. Mtanzania yeyote hastahili kuwa kwenye uongozi katika ngazi yoyote kwa staili ya kudharau na kutukana Watanzania akidhani kwamba kwa kufanya hivyo atajijengea umaarufu. Jambo ambalo Watanzania wengi wanajiuliza ni kwamba ujeuri tunaoushuhudia unatokana na ulevi wa madaraka au ulevi wa fedha ama vyote viwili?

Rai yangu kwa Watanzania ni kupuuza uzushi unaosambazwa, na kwamba wasikubali kuondolewa kwenye hoja ya msingi ya kutaka kujua namna serikali yao itakavyotekeleza sera na sheria ya uwezeshaji ili kuhakikisha kuwa inawashirikisha katika mchakato mzima wa uchumi wa gesi asilia, kuanzia hatua ya utafutaji na uchimbaji (up-stream) hadi uchakataji na usambazaji (midstream and downstream).

Na kwa wale wanaotumiwa na kiongozi huyo ningependa kuwasihi wawe na uzalendo na mapenzi kwa nchi yao na wakatae kutumiwa kwenye mambo ya uongo yasiyo na tija kwa taifa letu.

Kinachonipa faraja katika juhudi zangu za kutetea maslahi ya Watanzania ni maneno ya Mhe. Rais Dkt. Kikwete aliyoyasema mnamo mwaka 2009 kwamba:

“Midomo ya Wanadamu imeumbiwa kusema na wakati mwingine wanasema wanachokifikiria wao hata kama huo siyo ukweli, lakini watauamini, wataueneza uongo huo na watakuhukumu kwa uongo wao.”


Dkt Reginald Mengi
28 Mei, 2014
-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. mbona me cjaupata uo ujumbe, we mzee uctafute kick mamamaaeeee

    ReplyDelete
  2. Kwendraaaa uko

    ReplyDelete

Top Post Ad