Sakata la Vyeti Feki ..Ikulu Yatupa Mpira kwa Waziri Huyu..Kuhusu Vyeti vya Makonda Amefunguka Haya Mazito..!!!

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA


WAKATI uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma unakamilika leo, Ikulu imemtwisha mzigo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuwa ndiye mhusika mkuu wa suala hilo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Machi 20, mwaka huu na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurian Ndumbaro, uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma pamoja na namba za mitihani kwa watumishi wa umma ulioanza Machi 12, mwaka jana, utakamilika rasmi leo.

Katika tangazo hilo, Dk. Ndumbaro anaeleza kuwa uhakiki huo haujalenga kumkoma mtumishi wa umma bali kuhakikisha kunakuwa na watumishi wenye sifa stahiki na kitaaluma na kitaalamu ili kutoa huduma zilizo bora na kwa weledi kwa wananchi.

"Serikali inasisitiza kuwa mtumishi wa umma atakayeshindwa kutumia muda uliotolewa kuwasilisha nakala za vyeti au namba za mitihani kwa wale waliopoteza, atakuwa amejiondoa mwenyewe katika ajira serikalini," linaeleza tangazo hilo ambalo Florence Temba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Utumishi, aliithibitishia Nipashe kuwa ni lao.

Alipoulizwa na Nipashe kama uhakiki huo unawahusu pia wateule wa Rais, Temba alisema ni kwa watumishi wote wa umma, lakini akadai kuwa vyeti vya wateule wa Rais vinahakikiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi.

Nipashe ilipomtafuta Simbachawene kuzungumzia suala hilo, alidai masuala ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wote wakiwamo wateuliwa unafanywa na Wizara Nchi, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

"Utumishi ndiyo wanaofanya hiyo kazi ya uhakiki na utunzaji wa taarifa zote za watumishi na wateuliwa, hivyo siwezi kujibu hilo suala," alisema Simbachawene.

Kutokana na majibu hayo ya Simbachawene, Nipashe ilimtafuta tena Temba ambaye alisisitiza kuwa wanaohakikiwa na wizara yao ni watumishi wa umma na kwamba vyeti vya elimu na kitaalamu vya wateule huwa wanavipeleka kwenye mamlaka husika za uteuzi.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana mchana kuhusu uhakiki wa vyeti vya elimu na kitaalamu vya wateule wa Rais, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, alisema Simbachawene ndiye anayepaswa kuzungumzia uhakiki huo.

"Muulize huyo huyo Simbachawene. Vyeti vinahakikiwa huko huko Tamisemi. Simbachawene yuko Ofisi ya Rais Tamisemi ambako mambo ya uhakiki (kwa wateule) yanafanyikia huko," alisema Msigwa.

Jitihada za Nipashe kutaka kuzungumza na Simbachawene jana hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kutopokewa na hakujibu ujumbe mfupi wa maandishi tuliomtumia kuhusu suala hilo.

Kwa miaka mingi, ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha upotevu wa mabilioni ya shilingi kutokana na malipo ya watumishi hewa.

Kutokana na changamoto hiyo, Machi 12, mwaka jana, serikali ya awamu ya tano ilielekeza kufanyika kwa uhakiki wa watumishi hewa kwa kukagua vyeti vya kazi wanavyotumia ili kuwe na usimamizi na uwajibikaji.

Juni 22, mwaka jana, Rais John Magufuli akatangaza kusitisha ajira serikalini ili kuhakiki watumishi wote wa umma.

Kutokana na uamuzi huo, nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali vya likizo ya bila malipo vilisitishwa kwa muda hadi uhakiki utakapokamilika.

Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, baada ya kusitishwa kwa ajira, taarifa zilisambazwa katika halmashauri zote na idara za serikali kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na wizara Juni 13, jana kusitisha ajira hadi pale uhakiki utakapokamilika.

Kutokana na uamuzi huo, ajira 71,496 zilizokuwa zimepangwa kutolewa mwaka huu wa fedha na serikali kwenye sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya na viwandani hazijatolewa, huku zikiwa zimebaki siku 91 kabla ya kumalizika kwa mwaka wa bajeti.

Kwa mujibu wa Temba, sekta ya elimu mwaka huu ilitarajiwa kuwa na ajira mpya 28,957, afya 10,870, kilimo 1,791, mifugo 1,130, huku maeneo mengine ambayo hayakutajwa, yakitarajiwa kuwa na ajira 28,748.

Ofisa huyo wa serikali aliiambia Nipashe kuwa hadi kufikia Agosti 2016, watumishi 839 walikuwa wamefikishwa kwenye mamlaka za kiuchunguzi likiwamo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kutoa maelezo kabla ya kufikishwa mahakamani kutokana na kunufaika kwa kujipatia fedha kupitia watumishi hewa.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani Novemba 5, 2015, serikali yake imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kukomesha vitendo vya ufisadi vikiwamo hivyo vya kuwapo kwa malipo ya kila mwezi yanayokwenda mifukoni mwa maofisa wachache wasio waaminifu badala ya fedha hizo kuelekezwa katika shughuli nyingine za maendeleo.

Credit - Nipashe
----

Love Story ya NJIA PANDA,Ni Kali mnoo Jamani.

Kusikiliza au kusoma mwendelezo wake Tembelea www.makapedia.com kisha bofya palipoandikwa NJIA PANDA kila siku saa moja kamili jioni BURE au bofya HAPA

Pia Bofya HAPA kujiunga na what's app channel yetu,tukukumbushe kila siku.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad