Jux Afichua Siri ya Penzi Kwa Jack hadi V-money

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA


WAHENGA wanasema utamu wa ngoma uingie ucheze mwenyewe, hivyo hivyo raha na karaha ya mapenzi anayajua ni yule ambaye yupo kwenye uhusiano.

Asikuambie mtu, kipenda roho hula nyama mbichi, muulize Juma Jux atakuambia uhalisia wa msemo huo baada ya kuingia mapenzini na msanii maarufu wa filamu nchini, Wolper ambapo alikuwa hasikii wala haambiwi na mtu.

Jux anajua raha na karaha ya mapenzi na jamaa akipenda anapenda kweli, safari yake katika mapenzi imekuwa ndefu, akitoka na mastaa mbalimbali kama Wolper, Vanesa na wengineo

JUX, WOLPER WAKUTANA HARUSINI

Jux ni muwazi katika uhusiano wake lakini wapo wengi ambao ukiwauliza wanachofahamu kuhusiana na uhusiano wa mkali huyo wa muziki wa R&B na Wolper, watakwamba hawajawahi hata kusikia kama wawili hao waliwahi kuwa wapenzi.

Ili kujua zaidi, huyu hapa Jux mwenyewe anafunguka:


“Watu wengi wanadhani mpenzi wangu wa kwanza maarufu ni Jackline Patrick, si kweli, nilianza na Jackline Wolper, nilidumu naye miaka miwili baada ya mimi kwenda chuo China ndio aliingia katika uhusiano mwingine,” anasema na kuongeza:

“Nakumbuka Wolper nilikutana naye kwenye harusi ya dada yangu na tukabadilishana namba za simu na kujikuta tunaingia kwenye uhusiano. Sababu za Wolper kuamua kuingia kwenye uhusiano mwingine na kunisahau mimi nadhani ni ushawishi wa fedha.”

ELIMU YAWATENGA

“Nilichagua kwenda nchini China kwasababu nilikuwa na ndoto ya kuwa mfanyabiashara, lakini naweza kusema ndio ulikuwa mwanzo wa kumpoteza aliyekuwa mpenzi wangu,” anasema.

“Kitendo cha mimi kusafiri tu nilikuwa napata taarifa za Wolper kutumia vitu vya gharama kama kuendesha magari ya bei ghali zaidi, nikimuuliza ananiambia ananunua mwenyewe kutokana na kazi yake ya filamu. Kwa kuwa nilimkuta akiwa maarufu nikawa naamini, lakini baadaye mwenyewe aliamua kuniambia ukweli.

“Aliniambia kuna mtu kampata lakini yupo naye kwasababu ya fedha hana upendo naye, mimi nikamjibu siwezi kuwa naye katika uhusiano akiwa tayari ameingia kwenye uhusiano mwingine na mtu mwenye uwezo kwani hawezi akawa anampa fedha tu bila kuhitaji vitu vingine.”

JUX ANA SIRI NZITO

Umaarufu wa msanii Jux uliongezeka zaidi baada ya aliyekuwa mpenzi wake Jackline Patrick kukamatwa na dawa ya kulevya China akiwa katika harakati ya kuzisafirisha. Jux amefunguka siri nzito na namna walivyokutana na mwanamke huyo.

“Baada ya kuamua kuachana na Wolper niliingia katika uhusiano na Jack, ambaye nimekaa naye miezi nane tu tangu tumeanza uhusiano. Huwezi kuamini mimi nilikuwa sifahamu lolote kuhusiana na tukio alilokutana nalo,

“Nilikutana na Jack nchini China tukapendana na tulikaa miezi nane nyumba moja aliniaga kuwa anakuja Tanzania na nilikuwa katika kipindi cha mitihani ili nirudi nyumbani likizo, nikakubaliana naye kuwa acha atangulie mimi nitamkuta baada ya kumaliza mtihani.

“Baada ya siku mbili alipoondoka nilijaribu kumtafuta kwenye simu nilikuwa simpati baadaye mwenyewe alinipigia kwa namba ngeni na kujitambulisha kuwa yeye ni Jack na amekamatwa na dawa za kulevya lengo lake lilikuwa ni mimi kuifahamisha familia yake kuwa amepatwa na tatizo hilo.

“Baada ya taarifa hiyo alinikatia simu na sikuwa na muda wa maswali yoyote, niliachwa katika wakati mgumu sana, sikuwa na kitu cha kufanya, nakumbuka nilimpigia mtoto wa balozi wa China, ambaye ni rafiki yangu alinithibitishia hilo,” anasema.

HUYU NDO ALIANZISHA PENZI

Marehemu Pancho Latino alikuwa ni muandaaji wa muziki, ambaye alikutwa amefariki mwaka jana kwenye bahari ya kisiwa cha starehe cha Mbudya jijini Dar es Salaam.

Kutokana na ukaribu na wasanii hao, Jux bado anamkumbuka mshkaji wake wa zamani.

“Nakumbuka baada ya kuthibitishiwa kuwa Jack ni kweli amekamatwa na ‘unga’ nilikaa wiki moja tu China na kurudi Tanzania, nilipofika Uwanja wa Ndege Julius Nyerere ndio nilikutana na picha za Jack akiwa amezibwa sura na kuhusishwa na kukamatwa na dawa.

“Pancho ndio mtu pekee ambaye alikuwa ananiondoa kwenye mawazo ya mpenzi wangu kusafirisha dawa za kulevya bila ya mimi kufahamu kwani muda wote alikuwa ananipeleka katika mawazo ya kutunga mashairi na kuimba,”

“Siku nimeenda studio aliniambia kuna msanii wa kike anamfahamu japo anaimba Kinyamwezi, pia anaweza ‘kuimba Kizungu’ lakini anafaa kufanya kazi na mimi na ikafanya vizuri. Niliomba anionyeshe picha. Aliponionyesha tu nilimpenda na nilitamani kuimba naye, lakini kitu kimoja nilichokuwa nacho akilini ni je atakubali?

“Pancho pia alinikatisha tamaa kuwa sitaweza kufanikisha hilo, lakini kutokana na kumuelewa nililazimisha ili niweze kufanya naye kazi. Nashukuru tulifanikisha hilo na ndio ukawa mwanzo wa kuingia katika uhusiano mara baada ya kufahamiana na kubadilishana namba.

VANESSA YUKO KWENYE RELI

“Uhusiano wangu na Vannesa ndio uhusiano ambayo ulidumu kwa muda mrefu sana zaidi ya uhusiano wangu mwingine wowote. Ninachoweza kusema ni kwamba umenijenga na kuniimarisha.

“Vanessa ni mwanamke ambaye anaamini katika uwezo na kujiamini. Si mwanamke ambaye anakubali kudidimizwa tofauti na wengi. Alinifanya nijikute nakuwa katika uhusiano wenye levo moja. Mimi najua na yeye anajua. Kitu kikitokea tunakosoana na kueleweshana.

“Kwenye uhusiano, mwanamke au mwanaume kuna kujishusha, kuwa juu ya mwingine, kuharibu, kukusoa na kadhalika, alinifundisha hivyo vitu na vimenijenga na napenda kuwashauri wanaume wenzangu kuwa ni muhimu kumpa uhuru mwanamke.

“Vanessa ni mtu anayejiamini sana alinifundisha kumpa nafasi mwanamke. Kwenye mapenzi anakuwa huru na wewe. Anaweza kukwambia kabisa ulivyovaa sio na ukamsikiliza na sio kama wengine ambao wamekuwa wakiwapiga wake zao au wapenzi wao pale wanaposhauriwa.

VANESSA SI RAHISI AISEE

Kwenye uhusiano wanaume wamekuwa wakiamini kuwa wanawake ni rahisi endapo wakifuatwa na wanaume na ni rahisi kushawishiwa ili kuweza kuingia kwenye mapenzi. Kwenye hili Vanessa amewakingia kifua wanawake wengi na limethibitishwa na Jux.

“Vanessa sio mtu rahisi. Sio kwenye uhusiano tu, hata kwenye kazi zake za muziki, hilo ni lazima niliweke wazi na nililiheshimu kupitia kwa mwanamke huyu.

“Nakumbuka nilikuwa nimetoka China, akili yangu ikiwa haina kitu kingine cha kufikiria zaidi ya muziki ili kujitoa katika mawazo ya Jack.

“Pancho Latino mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi ndio mtu wangu wa karibu ambaye alinikutanisha na Vanessa na kuniunganisha naye kupitia kazi yangu ya muziki. Alikuwa anamuelewa sana mwanadada huyo, akinisisitiza kuwa ni msanii mzuri, lakini natakiwa kuchukua muda kumpata ili nifanye naye kazi.

“Nilitumia zaidi ya miezi mitatu kumshawishi ili anisaidie nifanye naye kazi. Kabla yangu aliyefanikiwa kumnasa ni Ommy Dimpoz ambaye alifanya naye kazi na ikafanya vizuri zaidi kwenye tasnia ya muziki huu.

“Baada ya kuona Ommy kafanikiwa nilimsisitiza Pancho na mimi aniunganishe naye nakumbuka kuna siku nilikuwa nimetoka nyumbani naenda studio, nikapigiwa simu kuwa Vanessa yupo na tulipoonana ndio ulikuwa mwanzo wa mimi na yeye kufahamiana na kukubali kufanya kazi na mimi,” anasema.

BONGE LA TOZI KISA VANESSA

Jux ndiye msanii anayeonekana nadhifu zaidi kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya kutokana na namna anavyovaa na kupendeza. Unajua nini kipo nyuma yake? Mwenyewe anafunguka:

“Kwa namna moja au nyingine naweza kuweka wazi kuwa Vanessa amechangia mimi kuonekana nadhifu zaidi mbali na kwamba usafi na kupendeza ni kitu kilichokuwa katika damu yangu tangu zamani.

“Siku ya kwanza naenda kuonana na Vanessa kwenye studio ya Pancho nilibeba marashi kwenye gari yangu. Niliposhuka kwenye gari tu nilijipulizia lengo ni kutaka kuonekana bora kwa mwanadada huyo ambaye baada ya kumuona tu naye alistuka nakuinuka kunikumbatia.

“Vanessa ni mzuri na naamini kila mwanaume aliye kamilika anatamani kuwa naye.

“Nakumbuka kila tukipanga kutoka nilikuwa najikuta tunavaa sare bila ya kupeana taarifa hii ilinionyesha kwamba ni mwanamke smati na mimi natakiwa kuwa hivyo.”.

KISA TREY SONGZ

Ujio wa muimbaji supastaa wa Kimarekani, Trey Songz, kwenye msimu wa Coke Studio Afrika nchini Kenya ulizua balaa.

Vanessa alionyesha ukaribu na nyota huyo mkubwa wa muziki na picha zikazagaa wakiwa wamekumbatiana huku uvumi ukiwahusisha wawili hao kimapenzi. Jambo hilo liliripotiwa kutomfurahisha Jux.

“Kuna kipindi cha nyuma niliachana na Vanessa kwa muda wa miezi nane sababu ilikuwa ni picha.

“Nakumbuka nilikuwa na rafiki zangu sihitaji kuwataja, Vee alikuwa nje ya nchi kufanya tamasha, akapiga picha na msanii mkubwa akaiposti katika ukurasa wake wa Instagram na rafiki zangu walipoiona wakawa wananijaza upepo ‘picha gani hizi?’,”

“Nililibeba kama lilivyo na kumtumia meseji kwanini ameposti picha ya aina hiyo? Kwa ustaarabu wake akaniuliza. ‘kwani ina shida gani? Si nipo kwenye tamasha? Niifute?’ Nilichomjibu ufute ili iweje wakati tayari umeiposti kwenye mitandao na kila mtu ashaiona?,

“Nakumbuka Vee alikuwa bado hajamaliza kutumbuiza katika tamasha hilo. Hakufanya vizuri kutokana na nilichomwambia.

“Aliporudi alinikuta bado nipo juu kwa hasira, sitaki kumsikiliza na kumwambia kuwa kama sitakiwi kuuliza vitu kuhusu yeye basi aniache. Vee alikuwa na jibu moja tu ‘IT’S OK’ na kuondoka zak.

“Mimi kwa kuamini kuwa napendwa na nitatafutwa tu zilipita siku mbili sijatafutwa, mimi ndio niliamua kumtafuta. Nakumbuka nilimtumia meseji, hakujibu. Nilipiga hakupokea na ndio niliamua kumfuata na kumuomba msamaha. Alichonijibu hahitaji kuchezewa hisia zake na wala hakunielewa,

“Marehemu Ruge ambaye ndiye alikuwa mlezi wangu, ndiye aliyetupatanisha baada ya kuandaa tamasha la ‘Fiesta’. Nakumbuka ilikuwa Mwanza, alitupa wazo la kuimba pamoja jukwaani. Tuliimba kwa hisia na ndiyo ulikuwa mwanzo wa kurudiana tena.

“Ndani ya miezi nane ambayo hatukuwa pamoja, Vanessa aliingia kwenye uhusiano mpya ambao niliuvunja baada ya kurudiana naye baada ya kuanza kuposti picha tukiwa pamoja, ndipo mwanaume aliyekuwa naye aliamua kupiga simu na kumporomoshea matusi Vee. Hicho ndio kilikuwa chanzo cha kurudi katika himaya yangu tena, kwani nilitumia udhaifu wa huyo mwanaume kuwa mwanamke hatukanwi.”

Vanessa baadaye aliwahi kuzungumzia kuhusishwa kwake na Trey Songz akikana kuwa na uhusiano yake.

Alisisitiza kwamba alikuwa ni mtu aliyefahamiana naye kabla ya kukutana naye kwenye Coke Studio hivyo alikuwa akifurahi naye kama rafiki tu.

HAKUNA MAPENZI TENA

Sasa ni rasmi Vanessa na Jux hawapo katika uhusiano tena ni baada ya wawili hao kila mmoja kuthibitisha kwa wakati wake kitu ambacho kimemkera Jux na kuamua kuweka wazi uhusiano yake mapya.

“Unajua tangu mimi na Vee tumeachana ni kama miezi tisa au nane. Tulikubaliana kufanya siri kutokana na brandi yetu ikiwa ni sambamba na mashabiki wetu walivyokuwa wanakubali uhusiano wetu.

“Hivi karibuni alikuwa anahojiwa kuhusiana na mapenzi yetu akafunguka kuwa tumeachana. Sijajua lengo lilikuwa nini, sitaki kumsemea japo nahisi alikuwa anajisafisha kwa uhusiano wake mpya, ndio mwanzo wa kuachana kwetu kufahamika, ila alisapraiz.

“Ni vitu vingi tumevificha nikajiuliza ilikuwaje kaamua kusema ukweli?

“Nakumbuka kuna tamasha tulilolifanya hivi karibuni tulikuwa tayari tumeachana kila mmoja alilala chumba chake japo lilikuwa ni la pamoja ni watu wachache walijua tumelala chumba tofauti yote ni makubaliano, lakini ikaja ikawa tofauti.

ANASA KIFAA KIPYAA

“Mimi siku zote mtu ninayempenda hasa msichana huwa namuandaa. Katika miezi tisa ya kuachana na Vee ndani ya miezi minne ndio nilianza kumuandaa huyo na nilimwambia kila kitu kuhusu Vee alinielewa.

“Mimi napenda, sina kiki nikiwa na mtu sijifichi, lakini nililifanya hilo kwa huyu. Nilifanya siri, nilimnyima kujiamini lakini baada ya Vanessa kuamua kufunguka kuachana na mimi ndio niliamua kumuweka wazi.

“Nilimfanyia kama zawadi kumleta Tanzania kuja kuangalia wanyama kwani ndio kitu alikuwa anatamani kukiona, hasa chui, simba na wanyama wengine, hivyo baada ya kuhitimu chuo alikaa wiki moja akaja.

“Baada ya kuja Tanzania nikaona ndio nafasi ya kuposti picha zake na kumuonyesha nampenda sana na kiukweli nikimpenda mtu napenda ajione yeye ni wa kipekee kwangu.

“Sijafanya hivyo kumuumiza Vanessa, hapana, nimefanya kutokana na kushindwa kuficha uhusiano wangu na kama ni kumuumiza sio sasa kwani nilishawahi kwenda Singapore kwenye sherehe ya mdogo wake mpenzi wangu wa sasa na tulipiga picha nyingi nzuri lakini nilikuwa namkataza asiposti kwasababu ya heshima yangu kwa Vee,” anasema
----

Utamu wa audio book ya SIRI YA PADRE NA MKE WANGU hauna mfano, sikiliza Sehemu ya 1 bure, Sehemu ya 2 Tsh 2000 tu

Nusu ya mapato ni kwa ajili ya wagonjwa wasiojiweza, Lipia uburudike huku ukitoa sadaka Safi,ni www.makapedia.com au bofya kitabu hapo chini:



 

-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad