.

7/27/2021

Shahidi amtaja JPM kesi ya kina Sabaya
 
SHAHIDI wa sita wa Upande wa Jamhuri, Bakari Raibu Msangi (38), ametoa ushahidi mahakamani akidai aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) katika tuhuma za kuvamia duka la Mohamed Saad na kupora baadhi ya vitu na mali, lilikuwa agizo la Hayati Dk. John Magufuli.

Shahidi huyo ambaye ni Diwani wa Sombetini jijini Arusha (CCM), alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Msangi alidai kuwa alipofika katika duka la Saad, alimkuta Sabaya kwenye duka hilo na kwamba mshtakiwa huyo alihoji sababu za diwani huyo kuwatetea watu aliowaita wahujumu uchumi.

Shahidi huyo alidai Ole Sabaya alimweleza kuwa alikwenda dukani huko kwa agizo la Hayati Rais Magufuli, kwa kuwa wamiliki wa duka hilo walikuwa wanafanya biashara kinyume cha sheria.

"Sabaya aliniambia kuwa mimi nawatetea wahalifu ambao ni wahujumu uchumi, watakatishaji wa fedha na wanafanya biashara bila ya kutoa risiti, najaribu kumzuia wakati ameagizwa na Rais John Magufuli," alidai Msangi.


 
Shahidi huyo pia alidai aliwekwa chini ya ulinzi na Sabaya kisha kuporwa fedha kiasi Sh. 390,000.

Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Silvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38), wote wakikabiliwa na kesi ya jinai namba 105, yenye mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Shahidi huyo wa sita alidai mahakamani huko kuwa ni mfanyabiashara anayefanya shughuli zake katika Mtaa wa Pangani, Kata ya Kati na ni mkazi wa Kata ya Sombetini jijini Arusha.


Akihojiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Tumaini Kweka, shahidi huyo alidai mbali na shughuli ya biashara, yeye ni mwanasiasa na Diwani wa Sombeni.

Msangi alidai kuwa Februari 9, mwaka huu, akiwa katika majukumu yake ya kikazi, majira ya saa 11:30 jioni, alipigiwa simu Ali Saad Hajirini.

Alidai aliambiwa Ole Sabaya alikuwa dukani kwa kaka yake (Mohamed Saad) na amewapiga sana watu waliokuwa dukani huko.

"Nilimwambia nitakwenda kuangalia kuna tatizo gani kwa kuwa Sabaya namfahamu na nilipofika karibu na duka hilo niliona watu wengi wakiwa wanashangaa kinachoendelea dukani.


 
"Kulikuwa na watu wawili hapo nje ya duka wanaonifahamu, mmoja alinitahadharisha nisiende huko kwa kuwa nitakufa kwa kuwa Sabaya yupo huko anapiga watu, nilimjibu 'ngoja niende, acha aniue'.

"Nilipofika karibu na hilo duka, niliwakuta watu wawili wameshika bastola na wamejifunika kwa kofia kufunika sehemu za macho na uso, niligonga mlango wa geti mara tatu haukufunguliwa. Kwa kuwa ulikuwa umerudishiwa nusu niliufungua na kuingia ndani," alidai.

Shahidi huyo alidai kuwa alipoingia ndani, watu wawili waliokuwa wameshika bastola, walifunga mlango kwa nje na alipoingia ndani ya duka alikuta mtu mmoja amewekwa chini ya ulinzi kwa kulazwa kifudifudi sakafuni.

Alidai kuwa kutoka geti la kuingilia hadi dukani, ndani kuna umbali kama wa mita sita na kuna taa kubwa ambazo zilikuwa zimewashwa.


"Niliposogea karibu na kaunta, nilikuta kundi la watu wengi wamesimama hapo, akiwamo Sabaya, msaidizi wake Silvester Nyengu, dada mmoja mwenye lafudhi ya kikenya alikuwa amepigishwa magoti na wengine sikuweza kuwatambua na walikuwa kama watu 10.

"Pia wengine niliowatambua ni Hajirini, Numan na mtu mwingine mmoja ambaye sikumtambua, walikuwa wamelazwa chini na mimi nilimsogelea Sabaya, alikuwa ameshika mkanda wa kiunoni nikamsalimia nikamwambia 'Sabaya habari yako' mara tatu lakini hakuitikia.

"Alikuwa akijitutumua kwa kupandisha mabega juu na mmoja wa walinzi wake waliniambia 'kwani hufahamu jina la mkuu?'" Alidai.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kukataliwa salamu, Sabaya aliwaambia walinzi wake wamweleze jina lake kwamba anaitwa General Lengai Ole Sabaya na anapomsalimia anapaswa kuonyesha utii.

"Nilitii agizo kwa kumwita General Lengai Ole Sabaya, hapo aliridhika na kufurahia sana huku akijipiga kifua akisema naam naam na aliitikia kwa kunguruma huku akijitengeneza.


 
"Muda siyo mrefu kupita aliniuliza kwamba nimefuata nini hapo dukani huku akisema nimekwenda kuwatetea Answary wenzangu na nilimjibu kwamba nilikwenda kufahamu ndugu zake wana shida gani," alidai.

Alidai kuwa baada ya hapo alihoji sababu ya Sabaya kutoka wilayani kwake (Hai) kwenda kufanya kitendo hicho Arusha wakati Arusha kuna viongozi na mamlaza za kiserikali ikiwamo polisi, TRA na TAKUKURU.

Alidai baada ya kumwambia maneno hayo, Sabaya alikasirika sana na wakati akijitengenezea aliona bastola kiunoni na wakati huo walinzi wake walikuwa tayari wameshamzunguka kila kona.

"Wakati General Sabaya alipokuwa amechukia, walinzi wake walinizunguka aliwaagiza wanisachi (kupekua), na baada ya hapo walinipiga kipigo kizito," alidai na kuongeza kuwa aliporwa Sh. 390,000 na simu ya mkononi.

"Nilimwomba Sabaya asiniue kwa kuwa mke na mtoto wangu walikuwa ni wagonjwa, alinijibu hata kama anafahamiana na mdogo wangu (Juma Raibu), kiherehere changu ndiyo kimeniponza kwa kwenda pale,

"Baada ya kipigo kizito aliagiza walinzi wake wanifunge pingu mikononi na miguuni huku wakiendelea kunipiga nikiwa nimeegemea kaunta hadi nilipoteza fahamu na baada ya muda nilipata fahamu na nilipoamka nilimwomba maji mmoja wa walinzi kwa kuwa nilihisi kifo, lakini Sabaya aliagiza nisipewe maji huku akiniambia nisifuatilie mambo yake," alidai.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger