Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

CHADEMA yadai polisi kuzingira ofisi kikao cha ndani 
ZAIDI ya askari 10 baadhi yao wakiwa na silaha za moto wamedaiwa kuzingira ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Mbeya, katika kikao cha ndani cha viongozi wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA).

Tukio hilo limetokea jana na kuzua taharuki ikiwa imebaki siku moja Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kufanya mkutano na wadau wa vyama vya siasa kwa lengo la kuondoa misuguano kati ya vyama hivyo na Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei, alisema hana taarifa za tukio hilo na wala hajatuma askari yeyote kwenda kwenye ofisi za chama hicho.

"Sijatuma wala kuagiza mtu kwenda huko kwa hiyo kama kuna mtu ambaye amekwenda kivyake vyake atajua mwenyewe," alisema Kamanda Matei.

Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Mbeya, Elizabert Mwakipesile, akizungumza na gazeti hili alisema jana saa 4:00 asubuhi wakati wakijiandaa na kikao, magari mawili ya polisi yalifika katika ofisi zao zilizopo eneo la Kadege, jijini Mbeya, moja lilisimama upande wa kushoto na jingine kulia huku baadhi ya askari wakiwa na silaha za moto.


 
Alisema, baadhi ya askari walishuka chini hali iliyozua hofu kwa kuwa vikao vya ndani vinaruhusiwa kama kawaida.

"Tulivyoona hayo magari ya polisi wakati tukiwa bado nje ya ofisi ilibidi tukawasiliana na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote, ambaye alituambia tuingie ndani ya ofisi tuendelee na kikao kama kawaida na kuahidi atakuja eneo la tukio," alisema.

Mwakipesile alisema kikao hicho ambacho kilikuwa ni cha uratibu BAWACHA kwa lengo la kufanya tathmini zoezi la usajili wa wanachama kwa mfumo wa kidigitali kiliwakutanisha wenyeviti na makatibu wa majimbo saba ya uchaguzi ya mkoa huo.

Hata hivyo, alisema baada ya polisi kuzingira ofisi hizo,  saa moja baadaye waliondoka na kikao kikaendelea kama kawaida.

Alilitaka Jeshi la Polisi kuacha kuingilia shughuli za kisiasa kwa kuwa vikao vya ndani vya chama vinaruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Naye Joseph Mwasote, maarufu China, alisema anasikitishwa na mwenendo usiofaa wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya wa kufuatilia na wakati mwingine kuzuia mikutano ya ndani ya chama.

 HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWA APP YA UDAKU SPECIAL, DOWNLOAD HAPA KUZISOMA HATA KAMA HUNA BUNDLE

 Udaku Special Blog

Post a Comment

0 Comments