.

9/12/2021

Mtoto Ampa Vanessa Utajiri wa Kutisha

KATIKA orodha itakayotoka ya mastaa waliotengeneza utajiri wa kutisha hasa wale wa kike barani Afrika kwa mwaka 2021, tarajia kuliona jina la staa aliyejizolea mashabiki wengi kabla ya kusimama kupitia muziki nchini Tanzania, Vanessa Hau Mdee almaarufu V-Money, Gazeti la IJUMAA lina ripoti kamili.


UTAJIRI WA VANESSA MARADUFU
Mitandao mbalimbali barani humo inasema kuwa, baada ya kutangaza kwamba anatarajia kupata mtoto wa kiume na staa wa sinema, muziki na mitindo nchini Marekani, mwenye asili ya Nigeria, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi’, basi utajiri wake utapanda maradufu.

 

Jumanne ya wiki hii (Septemba 7, 2021), kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii zenye mamilioni ya wafuasi, Vanessa na Rotimi walitangaza rasmi kupata baraka hiyo ya mtoto kwa mahojiano maalum yanayopatikana kwenye jarida maarufu nchini Marekani la People.Wawili hao waliweka wazi mapenzi yao mwaka 2019 ikiwa ni miezi michache tangu Vanessa aachane na aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu ambaye ni staa wa muziki nchini Tanzania, Juma Mussa ambaye wengi humtambua kama Jux.

 

Vanessa aliachia picha mbalimbali zikimuonesha akiwa mjamzito anayekaribia kabisa kujifungua na kuandika; “Zawadi kubwa kuliko, asante Yesu kwa kutuchagua, kutuheshimisha…tuna furaha sana…”Kwa upande wake, Rotimi aliandika; “Zawadi kubwa imekuwa ni wewe, umebadilisha maisha yangu na sasa tumeungana milele kumlea mtoto wetu.“Naomba mtoto wetu awe na moyo wako, akili na imani yako, ninaahidi kukulinda wewe na mtoto wetu kwa kila nilichonacho…”


UTAJIRI WA VANESSA KABA YA MTOTO
Kwa mujibu wa mitandao hiyo, kabla ya taarifa hizo za kutarajia kupata mtoto, Vanessa alitajwa kuwa na utajiri
unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 1 (zaidi ya shilingi bilioni 2.2 za Kitanzania).Utajiri huo unajumuisha thamani ya mambo yote aliyojihusisha nayo kabla ya hapo kama utangazaji katika Kituo cha MTV cha Afrika Kusini, mitindo, kuwa Jaji wa Shindano la East Africa Got Talent (2019) na muziki ambao ndiyo umemlipa kwa kiasi kikubwa kuanzia shoo na mauzo ya muziki wake kwenye mitandao mingi ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki akiwa na mamilioni ya views au viewers (wasikilizaji na watazamaji) ambazo zinamuingizia mamilioni ya pesa.Mbali na vyanzo hivyo, pia amekuwa na madili kadhaa ya ubalozi na matangazo yanayomuingizia pesa za kutosha huku akimiliki podcast yake (huduma inayowawezesha watu kusikiliza redio kwa njia za intaneti katika mifumo kama MP3 na mingineyo ya sauti) inayokwenda kwa jina la Deep Dive With Vanessa Mdee.


MAMILIONI YA JARIDA
Inafahamika kwamba, jarida lililomhoji Vanessa la People Magazine ni jarida maarufu mno nchini Marekani ambapo hununua mahojiano maalum ya mastaa wakubwa kwa mamilioni ya pesa hivyo ni wazi kwamba, mwanamama huyo amevuta mkwanja wa kutosha na kuingia kwenye orodha ya mastaa wakubwa wa kiwango cha dunia.

 

People Magazine ni jarida linalochapa nakala milioni nne kwa wiki na kwa mwaka, hupata makadirio ya wasomaji zaidi ya milioni 50 duniani kote.Kuna habari kuwa, jarida hilo likishafanya mahojiano na staa mkubwa au kuwa na habari ya kijamii au udaku maalum, huziuza kwa mamilioni ya pesa kwa vyombo vingine mbalimbali vya habari duniani.Jarida hilo ndilo lilinunua haki ya kuuanika ujauzito wa Vanessa katika nyakati zake za mwisho kuelekea kujifungua kila chombo kilichoripoti kiliwasiliana na People Magazine.

 

VANESSA ASOMWA NA MAMILIONI
People Magazine husomwa na watu milioni 2.2 kwa siku, wakati mtandao wake hutembelewa na watu milioni 218 kwa siku hivyo Vanessa ameingia kwenye rekodi ya kusomwa na watu wengi zaidi duniani hivyo kuongeza walaji wa huduma zake kuanzia muziki na ongezeko la mashabiki, jambo ambalo litamuongezea kupiga mkwanja.

 

VANESSA NA ROTIMI
Mwaka 2019, wakati Vanessa anatangaza kuwa kwenye uhusiano na Rotimi, baadhi ya watu walimcheka wakiamini kwamba, mtu sahihi kwake alikuwa ni Jux, lakini mwanamama huyo hakujali.Hata hivyo, watu walikuja kuanza kuamini penzi la wawili hao baada ya jamaa huyo kumvisha Vanessa pete ya uchumba.

 

Sasa kinachosubiriwa ni harusi ya nyota hao wawili ambao wamekuwa wakionesha mapenzi yao kwenye mitandao ya kijamii. Rotimi amezaliwa kule New Jersey nchini Marekani, lakini wazazi wake wanatokea nchini Nigeria na Vanessa amezaliwa Arusha nchini Tanzania, lakini kwa sasa wawili hao wanaishi maisha ya kifahari kwenye mjengo wa maana huku mwanamama huyo akimiliki ndinga kali aina ya Range Rover alilonunuliwa na jamaa huyo huko Atlanta nchini Marekani.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL, BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
Share:

0 Blogger:

Post a Comment

New Video - Wana Wanywe Pombe

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger