Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Simba SC, Yanga SC Kuna Kitu Mmejifunza
JUMAMOSI ya wiki hii, tunakwenda kushuhudia mchezo wa Ngao ya Jamii, ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa msimu wa 2021/22 katika soka hapa nchini. Mchezo huo utawakutanisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam, Simba SC dhidi ya walioshika nafasi ya pili, Yanga SC.

 

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi wa soka, utachezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar kuanzia saa 11:00 jioni.

 

Tukiwa tunaukaribia mchezo huo, timu zimekuwa kwenye maandalizi makali yakiwemo ya kujiandaa na msimu wa 2021/22 kwenye michuano mbalimbali. Katika kujiandaa huko, Yanga na Simba zimekamilisha matamasha yao ambapo walianza Yanga, kisha Simba.

 

Yanga walikuwa na Wiki ya Mwananchi, kilele chake kilifanyika Agosti 29, 2021, kisha Simba wao wakafanya Simba Day, Septemba 19, 2021. Yote yakifanyika Uwanja wa Mkapa.

 

Katika matamasha hayo, timu hizo zilicheza mechi za kirafiki, Yanga ikipambana na Zanaco kutoka Zambia ambapo wenyeji walipoteza kwa mabao 1-2. Simba wakawaalika TP Mazembe kutoka DR Congo, katika mchezo huo, pia wenyeji wakapoteza kwa bao 0-1.

 

Ukiangalia aina ya timu ambazo Simba na Yanga zimecheza nazo, zina historia nzuri kwenye michuano ya kimataifa kwa maana ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

TP Mazembe wametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu, huku Zanaco nayo ikishiriki mara kwa mara michuano hiyo, hivyo zina uzoefu mkubwa sana.

 

Kipimo cha Simba na Yanga dhidi ya timu hizo, ni sahihi kwao kuelekea msimu wa 2021/22 ambapo kufungwa kwao ni wazi makocha wao wameona wapi bado kuna shida na wanapaswa kufanyia kazi.

 

Tumeshuhudia Yanga baada ya kufungwa na Zanaco, wakacheza mechi kadhaa za kirafiki za ndani, huku wakijiandaa kukabiliana na Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Muda wa kurekebisha zaidi yale makosa yao, pengine ulikuwa mdogo, mwisho wa siku Yanga imepoteza nyumbani na ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Rivers na kuondoshwa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-0.

 

Awali kipigo kutoka kwa Zanaco, kiliwaamsha, walivyokuja kufungwa tena na Rivers, kinatakiwa kuwaamsha zaidi kabla ya kuanza kwa msimu ili kutimiza malengo yao.

 

Tukiachana na Yanga, Simba nao kufungwa kwao mbele ya TP Mazembe, iwe somo na kuona wapi bado kikosi chao kina mapungufu ili kufikia malengo yao. Simba ndiyo mabingwa watetezi wa makombe yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Jumamosi hii wanaingia kuanza kutetea taji lao la Ngao ya Jamii, kisha baada ya hapo ndipo mchakamchaka wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 unaanza rasmi.

 

Lakini pia, kuna ishu ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita Simba ilifika robo fainali, msimu huu malengo yao ni kufika nusu fainali.

 

Malengo hayo hayawezi kufikiwa kama hakutakuwa na mikakati madhubuti ambayo itawekwa na kipigo kutoka kwa TP Mazembe, kiwe chachu ya kufanya vizuri. Kwa matokeo haya ambayo mmeyapata, ni wazi Simba na Yanga kuna kitu mmejifunza, hivyo hamtarudia makosa.

 

Hii iwe somo kwa timu zingine pia, inapotokea kwenye mechi zenu za kirafiki mnazoendelea kucheza mmepoteza, mnapaswa kukaa na kuangalia wapi kuna shida, rekebisheni, ili msimu ukianza rasmi, muwe na matokeo bora.

 HABARI KAMA HIZI DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL KWA KUBONYEZA > HAPA

Post a Comment

0 Comments