Ticker

6/recent/ticker-posts

 .

Kocha wa Taifa Stars Afunguka Baada ya Kichapo cha Mbwa Mwizi "Tulijiamini Sana Ndio Maana Tukapoteza Mchezo"
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kim Paulsen amesema kuwa kikosi chake kilijiamini zaidi hadi kupelekea kupoteza mchezo wao wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya timu bora ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo wa mzunguko wa tano wa Kundi J, Taifa Stars ikiwa nyumbani ilipoteza kwa kipigo cha bao 3-0 dhidi ya kikosi cha Kocha Héctor Cúper na kupoteza kabisa matumaini ya kupata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano (Play Off) yenye timu 10 ya kufuzu Kombe la Duniani 2022 nchini Qatar.

Kocha Paulsen baada ya mtanange huo amesema Wachezaji wake walijiamini zaidi katika mchezo licha ya kucheza na timu bora barani Afrika iliyo katika nafasi nzuri kwenye viwango vya Kimataifa, amesema Wachezaji hao walijiamini na hawakuwa makini na kupelekea kufungwa bao 3-0.

“Kama mnavyojua kwenye mchezo wa soka, ukijiamini sana unaadhibiwa kama ukifanya makosa. Tumeingia kipindi cha kwanza tumefanya kosa dakika ya Sita, tumeadhibiwa, tumeenda mapumziko tumerudi tumefanya kosa lingine tumeadhibiwa tena, tulijaribu kucheza kwa nidhamu, kushambulia kwa shinikizo lakini hatukuweza kutumia nafasi”, amesema Paulsen.

Kocha Paulsen amesema hajafurahishwa na kipigo hicho kutoka kwa timu ya DR Congo katika mchezo muhimu wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022, akitaja sababu hiyo kubwa ni kujiamini kupita kiasi kwenye mtanange huo.

“Tumejifunza kila mchezo, lazima ucheze kwa tahadhari, tumeona mchezo wa leo na tumepata maswali na majibu ya safari yetu ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, maana yake ni kwamba ukijiamini sana hutakiwi kufanya makosa”, ameeleza Kocha Paulsen.

Taifa Stars itasubiri kukamilisha ratiba ya Kundi J na timu ya taifa ya Madagascar mchezo utakaopigwa nchini humo, Novemba 14, 2021, huku nafasi kubwa ya kufuzu hatua inayofuata ikiwa kwa timu ya taifa ya Benin wenye alama 10 na DR Congo wenye alama 8, huku Taifa Stars ikiwa na alama 7 na Madagascar alama 3 pekee.

Katika hatua nyingine, Paulsen amesema anaamini Taifa Stars itakuwa bora zaidi baadae, miaka ijayo endapo Wachezaji wengi watapata nafasi ya kucheza Soka la kulipwa nje ya Tanzania, na huenda wakasaidia timu yao ya taifa kufuzu Michuano hiyo mikubwa duniani kwa baadae.


Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kim Paulsen akizungumza baada ya mchezo wao dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilipoteza mchezo huo kwa bao 3-0 ikiwa ni mchezo wa Kundi J wa kuwania kufuzu Michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar

 HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWA APP YA UDAKU SPECIAL, DOWNLOAD HAPA KUZISOMA HATA KAMA HUNA BUNDLE

 Udaku Special Blog

Post a Comment

0 Comments