4/19/2022

JICHO LA MWEWE: Simba watalia msimu huu, Yanga msimu ujao 
NIKASIKIA mahala Azam FC wanapambana kumrudisha kipa wao wa zamani, Aishi Manula. Wameweka pesa nyingi mezani.

 Ukiwa shabiki wa Simba taarifa hii inashtua. Ukiwa kiongozi wa Simba taarifa hii inashtua zaidi. Watalazimika kuweka pesa nyingi mezani kumbakisha Aishi.
Halafu nilidhani suala la Joash Onyango lisingekuwa na utata. Nilikosea. Nilidhani Yanga wangeridhika na mabeki wao wa kati, Dickson Job na Bakari Mwamunyeto. 

Nilikuwa nimekosea. Nasikia na wao wanataka kuleta ukorofi katika suala la Onyango. Mkataba wake kama ilivyo kwa Manula naye unamalizika mwisho mwa msimu huu.

Nimejaribu kufikiria. Simba watakumbana na gharika kubwa la matumizi ya pesa mwishoni mwa msimu au kuanzia sasa mpaka mwishoni mwa msimu. Wanaweza kujikuta wakitumia shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutengeneza kikosi chao cha msimu ujao.

Kwanza wanalazimika kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuwabakisha wachezaji waliopo. Nadhani kinaweza kuwa kiasi kikubwa zaidi cha pesa kuwahi kutumika kwa ajili ya kuwabakisha wachezaji waliopo kabla ya kuanza kutazama nje na kuleta wachezaji wapya. Kundi kubwa la mastaa linamaliza mikataba yake.

Hassan Dilunga, Joash Onyango, Aishi Manula, Bernard Morrison, Meddie Kagere, Rally Bwalya, Kennedy Juma, Chris Mugalu wote wanamaliza mikataba yao kwa wakati mmoja. Kila mchezaji atadai chake na nadhani kila mchezaji atadai kiasi kikubwa.

Inawezekana kila mchezaji akajikuta anatumia mkataba wa Clatous Chama kama kipimo cha yeye kujipatia mkataba mnono klabuni. Bahati nzuri kwao wachezaji wote hawa wanaingia katika vikosi vya timu mbili kubwa nyingine zenye pesa nchini, Yanga na Azam. Itakuwa habari ngumu kwa watu wa Simba kama klabu hizi zitataka wachezaji wake.

Lakini hapo hapo Simba najua wanataka kwenda sokoni kununua mastaa. Baada ya Yanga kuimarika na kuwa na uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa msimu huu, Simba watataka kukichangamsha kikosi na kununua mastaa kwa ajili ya michuano ya ndani na ile ya kimataifa. Na wanajua kwamba Yanga pia watataka kukiimarisha kikosi chao.

Eneo la kwanza ambalo Simba lazima wataingia sokoni kwa pesa nyingi ni eneo la ushambuliaji. Hawajaridhishwa na walichokiona kwa John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu msimu huu. Swali linalobaki kichwani ni kama watamuongezea mkataba Mugalu au wataleta mshambuliaji mwingine.

Lakini Simba pia wanaweza kwenda sokoni kununua mlinzi wa kati wa kigeni kwa sababu kuna asilimia kubwa wakaachana na mlinzi wao wa Ivory Coast, Sergi Wawa Paschal ambaye wanaamini kwamba wakati wake wa kucheza soka katika kiwango cha juu umepita na nafasi yake imekwenda moja kwa moja kwa Enock Inonga ambaye amekuwa akicheza na Onyango.

Upande wa Yanga kasheshe hili watakutana nalo msimu ujao. Msimu huu wanaweza kupumua na kupambana kwa wachezaji wachache, lakini msimu ujao watakuwa na maisha magumu. Kwa kuanzia Fiston Mayele atakuwa anamaliza mkataba wake klabuni hapo. Hauwezi kujua kitakachotokea.

Khalid Aucho, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Djuma Shaban, wote hawa watakuwa wakimaliza mikataba yao. Kwa sasa Yanga wanaweza kupumua kwa sababu wanajua watakuwa na mastaa hawa katika mechi za kimataifa ambazo wanaweza kushiriki kwa sababu wanakaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Yanga watalazimika kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuwabakisha mastaa hawa kwa sababu moja kwa moja wameingia katika kikosi chao cha kwanza msimu huu na kuibadili timu kwa kiasi kikubwa. Hili ndio tatizo au faida ya Yanga miaka ya karibuni. Kila mchezaji anaingia na umuhimu moja kwa moja.

Mchezaji ambaye sina uhakika kama atakuwa klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu au mwishoni mwa msimu ujao ni Herritier Makambo. Amerudi Yanga na mguu mbaya. Ameshindwa kuonyesha makali yake kama yale ambayo aliyaacha wakati anaondoka klabuni miaka mitatu iliyopita.

Simba na Yanga wamejikuta katika mateso haya ya kuwabakiza mastaa wake kwa pesa nyingi ndani ya muda mfupi kutokana na tabia ya kutoa mikataba ya muda mfupi kwa mastaa wake. Umekuwa utaratibu wa nchi nzima, klabu zote. Mikataba ni ya miaka miwili tu. Mpaka sasa tumeshindwa kupata jibu kwanini mkataba lazima uwe wa miaka miwili.

Inawezekana kuna sababu mbili. Sababu ya kwanza ni wachezaji wenyewe kufurahia mikataba ya aina hii. Wanajua ndani ya miezi 24 ijayo watapa pesa nyingine nyingi za kusaini mkataba mpya (signing-on fee). Wanaamini kwamba wakisaini mikataba mirefu basi signing-on fee itachelewa.

Lakini na klabu nazo zinaonekana kufurahia hali hii. Zinapatwa na hofu na kiwango cha mchezaji. Wanahisi wanaweza kumpa mchezaji mkataba wa muda mrefu halafu kiwango chake kikaishia njiani. Mchezaji atawabana na mkataba wake pindi wakimwambia kwamba hawamuhitaji tena.

Mfano ni kama ilivyojitokeza kwa Makambo. Waliamini kwamba walikuwa wamelamba dume lakini haikuwa hivyo. Na hata mwishoni mwa msimu huu wanaweza kutamani kuachana naye lakini lazima Makambo atawabana kwamba ana mkataba.

 Watalazimika kutoa kiasi kikubwa cha pesa kuvunja mkataba wake.
Lakini naamini kimoyomoyo wanatamani kama wangempa Mayele mkataba mrefu. Hata hivyo, wakati wanampa mkataba wa muda mfupi hawakujua kile ambacho Mayele angeweza kuwapa mpaka sasa. Hii ndio karata tatu ya mkataba mfupi kwa wachezaji wapya.

Tatizo letu tunaelekeza zaidi macho na masikio yetu kwa wachezaji wapya badala ya kuwa bize na wachezaji mastaa waliopo. Hata mashabiki nao wameiga tabia hii hii. Huwa hawasisimki wakisikia mchezaji kaongeza mkataba, wanasisimkwa wakisikia kuna kifaa kipya kinakuja klabuni.


Kuwa wa kwanza kutoa maoni


HABARI HIZI ZA UDAKU ZINAPATIKANA KATIKA APP YA UDAKU SPECIAL, IDOWNLOAD>> HAPA BURE 

Share:
Loading...

0 Blogger:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © UDAKU SPECIAL | Powered by Blogger