Askofu Gwajima ashangaa ujenzi wa reli badala ya uchimbaji chuma

 AJIRA ZA UHAKIKA NJE NJE, BONYEZA HAPA



MBUNGE wa Kawe, Askofu Dk. Josephat Gwajima (CCM) leo Jumatatu amesema licha ya kwamba ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) lilikuwa wazo zuri lakini Serikali ilitakiwa kuanza kuchimba chuma ambayo ndio malighafi inayotumika katika ujenzi wa reli hiyo ili kuokoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2.2 (Sh trilioni 5.1) zilizotumika kununua chuma nje ya nchi.

Aidha, amesema inashangaza kuona ugunduzi wa madini ya chuma na makaa ya mawe huko Liganga na Mchuchuma mkoani Njombe ulifanyika katika karne ya 18 lakini Serikali za awamu zote sita hazijayachimba madini hayo hadi yanafikia ukomo wa matumizi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Askofu Dk. Gwajima ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Mei, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara ya uwekezaji, viwanda na biashara kwa mwaka 2022/2023.

Aidha, ameenda mbele zaidi na kufafanua kuwa kilichosababisha serikali za awamu zote kushindwa kuyachimba madini hayo ni Taifa kutokuwa na maono, dira wala mipango ya muda mrefu kuanzia miaka 50 hadi 100.


 
“Nitoe takwimu ya uingizaji wa chuma Tanzania, mwaka 2018 tumeingiza chuma ya thamani ya dola za Marekani milioni 401.2, mwaka 2019 – dola milioni 491.9, mwaka 2020 –dola milioni 423.4, mwaka 2021 – dola milioni 700.80 na mwaka 2022 – dola milioni 235.7.

“Kwa miaka mitano tumelipa fedha ya kigeni kutoka Tanzania kwenda nje kwa ajili ya chuma, dola za Marekani bilioni 2.2. Kwa mtu yeyote mwenye akili, anayejua kuzitumia jambo hili hawezi kuliruhusu kufanyika kama chuma ipo hapa Tanzania,” amesema na kuongeza;

“Tumeanza na ujenzi wa reli ya kisasa… ilikuwa wazo zuri, lakini kwenye ujenzi wa reli malighafi nyingi inayotumika ni chuma, ilikuwaje tukaanza kujenga reli kwa kuagiza chuma kutoka nje badala ya kuchimba chuma chetu ndio tukajenga reli?”

Ameendelea kuhoji ni kitu gani kinatokea hadi kipaumbele cha kwanza kinakuwa cha mwisho na cha mwisho kinakuwa cha kwanza?


“Kinachotusumbua ni kukosa maono ya Taifa, mipango ya Taifa na dira ya Taifa, simlaumu mtu yeyote,” amesema.

Askofu Gwajima ambaye alianza mchango wake kwa kutahadharisha kwamba atagusa watu lakini si kwa ubaya bali kwa masilahi ya nchi, amesema kama kungekuwa na maono ya Taifa juu ya viwanda maana yake kungekuwepo maono ya muda mrefu yanayoelezea juu ya chuma kilichopo Tanzania.

“Tusingekuwa tumeanza na ujenzi wa reli, tungekuwa tumeanza na fedha ya kuchimba chuma ili kije kitengeneze reli zetu tungeokoa mabilioni ya shilingi.


 
“Jambo hili linaonekana kama ni ujinga kama kufukuza upepo lakini nchi nyingi zilizoendelea zina maono ya muda mrefu, hakuna nchi iliyoendelea kwa muda wa miaka mitano au 10, nchi huwa zinaendelea kwa kuweka maono ya miaka mingi ili wanafunzi na wasomi wanaione nchi kwa mbali,” amesema.

Wakati akiendelea na mchango wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Elibariki Kingu (CCM) alimpa Askofu Gwajima taarifa kuwa Taifa kuna mahali liliteleza kwani ilifuta Tume ya Mipango ambayo ingetengeneza mipango ya miaka 50 ijayo.

Aidha, Askofu Gwajima alipokea taarifa hiyo na kuongeza kuwa kuna mkataba wa kimataifa wa Paris ambao umeweka ukomo wa matumizi ya makaa kuwa mwaka 2030.

“Tangu yamegunduliwa karne ya 18 mpaka yanataka kufikia ukomo hatujayatumia bado, tunaweza kuita hiki kitu gani! kwamba Mungu amewawekea mlima wenye chuma na moto wa kuyeyusha hicho chuma palepale lakini hamuwezi kuitumia mpaka unafikia ukomo 2030, jambo hili hatutakiwi kuliruhusu kwa dakika, sekunde moja lakini tumefika hapa kwa kukosa maono,” amesema.


Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango
Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba naye amempa taarifa Askofu Gwajima kwamba Serikali za awamu zote zilikuwa na maono na dira ndio maana dira ya 2025 iliyotungwa kipindi cha Rais mstaafu Benjamini Mkapa inatumika hadi sasa.

Dk. Mwigulu amesema dira hiyo ambayo inafikia ukomo, sasa wapo kwenye maandalizi ya kutengeneza nyingine hivyo si vizuri kuidharau Tanzania kwani nchi nyingi jirani hunakili dira na maono ya Taifa.

Aidha, Askofu Gwajima alimjibu Dk. Nchemba kwamba kwa taarifa yake amethibitisha Taifa halina mpango wa muda mrefu kuanzia miaka 50 hadi 100 badala yake uliopo unaishia 2025.

“Sidharau kilichofanyika na serikali wala simshambulii mtu yeyote kwani mahala tulipo ni pazuri lakini tungekuwa mipango juu ya hili tungekuwa tumeanza na kuchimba chuma chetu ili kitumike kwenye reli, hii fedha dola za Marekani bilioni 2.2 ingekuwa imebaki hapa nchini,” amesema.


-------------------

NAFASI ZA AJIRA 

JIUNGE NA AJIRA YAKO TELEGRAM GROUP HAPA

INTERNSHIP VACANCIES

GOVERNMENT VACANCIES

NGO'S VACANCIES 

GOODLUCK

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad