Ticker

6/recent/ticker-posts

HISIA ZANGU: Inashangaza, tunatamani Fei akacheze nje halafu Msuva arudi


 
HUWA nacheka sana linapofika suala la wachezaji wetu kucheza nje ya nchi. Suala zima tunalitazama katika jicho la makengeza. Inategemea unataka nini kwa wakati huo. Hauzungumzii kile ambacho kinapaswa kuwa uhalisia. Wengi wanapuyanga tu.

Mara kadhaa nimewahi kuwasikia rafiki zangu wakiniuliza kwanini Fei Toto asiende kucheza nje. Huwa ninacheka tu. Mara nyingi hii huwa inatokea wakati Fei anapofanya vema, basi. Wakati mwingine huwa inatokea wakati tunapowahesabu wachezaji wa timu ya taifa wanaotoka nje ya nchi.

Tunahesabu kwa vidole tunagundua kwamba ni wachache tofauti na mataifa ya wenzetu. Baada ya hapo tunaanza kuulizana, kwanini Fei hachezi nje? Swali jepesi tu hili ingawa lina majibu mengi. Akacheze nje wapi? Ulaya, Asia au humu humu Afrika? Kwa mujibu wa Wikipedia Feisal ana miaka 24. Januari atatimiza miaka 25.

Feisal kwenda Ulaya ngumu. Wazungu wanakununua ili wakuuze. Hii kitu huwa inaitwa Resale value. Inabidi uwe na wasifu mkubwa kuweza kununuliwa moja kwa moja na timu za Ulaya ukiwa na umri huo. Wanakuhitaji mapema zaidi ili wakutengeneze. Kwa mfano, Samatta alikwenda Ulaya akiwa na miaka 23 kwa sababu wasifu wake ulikuwa mkubwa.


 
Alikuwa ametoka kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani. Hapo hapo alikuwa mfungaji bora wa michuano ya CAF na timu yake ilikuwa imetoka kuchukua ubingwa wa Afrika. Vinginevyo Feisal ana wasifu gani mzito wa kwenda Ulaya sasa hivi? Anaendaje moja kwa moja.

Nje ya Feisal tunayoizungumzia ni labda akacheze Afrika Kusini, Morocco, Misri na nchi ambazo zina ligi bora Afrika. Vinginevyo hili la Ulaya kwa Feisal halipo. Labda akacheze kwa timu za madaraja ya chini. Ujinga huu wa Feisal kucheza hapa mpaka miaka 24 unachangiwa na kila upande katika soka.

Kwa Feisal mwenyewe, amewahi kupania kucheza nje? Sidhani. Lakini nadhani pia hatukumuelewa Emmanuel Amunike wakati ule alipotuambia kwamba Feisal alikuwa na uwezo wa kucheza Barcelona. Amunike alikuwa anazungumzia kuhusu dhahabu maridhawa ambayo kama ingeoshwa ingeweza kucheza Barcelona. Alikuwa anazungumzia kama tungempika Feisal wa miaka 10.


Kuanzia hapo Feisal mwenyewe hajawahi kutamani. Kuanzia hapo hakuna mtu aliyemzunguka ambaye alimshauri vema. Kuanzia hapo rafiki yangu Mwigulu Nchemba aliona raha alipompeleka Yanga akitokea Singida United. Hata majuzi ameendelea kujisifu na kuona raha pale Bungeni baada ya Feisal kuifunga Simba. Kwanini wakati ule akiwa na miaka 19 tu asimtafutie timu nje?

Hata hivyo nawakumbusha tu kwamba licha ya uhodari wa Feisal lakini kucheza nje sio lelemama. Umewahi kuwaona viungo wangapi maridadi wanakuja kucheza uwanja wa Taifa na wanacheza soka lao hapa hapa Afrika? Kuna mambo mengi ambayo yanamfanya mchezaji kucheza nje. Upinzani huwa ni mkubwa.

Huyu Aziz Ki amepitwa kitu gani kikubwa na Feisal? Mbona bado yupo Afrika? Nawakumbusha kwamba ukiona mchezaji anacheza nje basi sio kitu lelemama. Tusisifiane sana hapa nchini tukadhani itakuwa rahisi kwa wachezaji wetu kucheza nje. Wakamuulize kwa kina Samatta.

Lakini hapo hapo tugeukie upande mwingine wa shilingi. Majuzi nilikuwa namtazama Simon Msuva akihojiwa mahala. Alidai kwamba ameshafuatwa na timu zote kubwa nchini ambazo zinawinda saini yake. Mpaka sasa Msuva hana timu na hana mwelekeo.


 
Mashabiki wanaposikia hivi wanashangilia kwamba timu zao zipo katika mbio za kuinasa saini ya Simon. Nakukumbusha tu kwamba hawa si Mashabiki wapya. Ni wale wale ambao tukikutana baa au katika vijiwe vya kahawa huwa wananiuliza kwanini Feisal hachezi nje. Wanasahau kwamba mada ni hii hii tu.

Wanamtaka arudi nyumbani mchezaji ambaye si ajabu kwa sababu ana takwimu bora zaidi katika timu ya taifa. Wanasahau kwamba mchango wake mkubwa unatokana na kujiendeleza vema kisoka kiasi cha kununuliwa na klabu bingwa ya Afrika Waydad Casablanca ya Morocco akitokea hapo hapo katika klabu ya Jifaa Jadida.

Wanasahau kwamba Simon ameimarika zaidi baada ya kwenda kucheza katika Ligi Kuu ya Morocco. Kule kwa Feisal wanaongelea aondoke, huku kwa Simon wanataka arudi. Wakati mwingine Watanzania huwa ni watu wa ajabu katika namna ya kushangaza.

Usisahau kwamba ni Watanzania hawa hawa walioshangilia baada ya kusikia Ibrahim Ajibu amekataa dili la kwenda TP Mazembe na badala yake akasaini Simba. Keshokutwa usishangae kuona wakiulizana kwanini George Mpole haendi kucheza nje ya nchi. Inategemea tu itakuwa wakati gani. Kuna wakati wa usajili na kuna wakati wa kuitwa kwa kambi ya timu ya taifa.


Mtanzania anayeelewa vema mahala tulipokwama hawezi kushangilia sana Msuva kurudi nchini. Hawezi kusuangilia Novatus Dismas kurudi kucheza nchini badala ya kuendelea kusonga mbele. Akitoka Israel inabidi aende akacheze Ufaransa au Ubelgiji. Lakini sisi huwa tunashangilia na hasa anaporudi Simba au Yanga.

Huyu huyu Kelvin John kuna watu watashangilia kusikia amerudi kucheza Simba au Yanga. Hakuna ambaye anaweza kuwaza kwanini ameshindwa kufuata nyayo za Mbwana Samatta kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Ili mradi amesaini timu yangu basi napiga hesabu za kufikia hatua ya makundi Ligi ya mabingwa wa Afrika.

Majuzi walikuja Algeria kutufundisha mpira. Baada ya mechi yetu dhidi yao kumalizika wote tulikubaliana kwamba wenzetu walikuwa katika kiwango kingine. Hakukuwa na maajabu mengi zaidi ya ukweli kwamba wenzetu wanacheza katika klabu maarufu Ulaya na sisi idadi kubwa ya vijana ni wa hapa hapa tu wanaocheza kila wikiendi dhidi ya Prisons au Mbeya City.

Hata hivyo kinapofikia kipindi cha usajili huwa tunasahau yote haya. Tunajikita katika kuzipenda klabu zetu zaidi kuliko taifa letu. Linapofika suala la timu ya taifa Kazi yetu kubwa ni kumshambulia Samatta kwamba hajitumi kama vile huwa anacheza peke yake uwanjani.

Ni kama vile Samatta anacheza sambamba na mastaa wenzake wa Ulaya katika jezi ya timu ya taifa. Lazima tukubaliane kumng’ata jongoo kwa meno. Tuache kuwepakwepa kulikopitiliza kutokana na mazingira ya wakati huo. Leo nimewapa mfano mdogo tu wa namna tunavyotofautiana suala la Feisal na Msuva.

Nafasi za Ajira Jiunge na Ajira Yako Telegram Group

 CLICK HERE


Post a Comment

0 Comments